Nguvu ya uharibifu waliyonayo nzige waliovamia Kenya, Uganda
- Wanaweza kuzingira eneo lenye ukubwa wa kilomita moja na kula kwa siku moja chakula kinachowatosha watu 35,000 na kusababisha uhaba wa chakula.
- Wanaweza kusafiri kwa zaidi ya kilomita 150 kwa siku na husafiri ka makundi.
- Wasipodhibitiwa wanaweza kusababisha janga la njaa na uharibifu wa mazao.
Dar es Salaam. Wakati nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania zikiendelea na jitihada za kupambana na uvamizi wa nzige, Umoja wa Mataifa (UN) umesema wadudu hao wanaweza kuzingira eneo lenye ukubwa wa kilomita moja na kula kwa siku moja chakula kinachowatosha watu 35,000 na kusababisha uhaba wa chakula.
Janga la nzige limeendelea kuliathiri eneo la Pembe ya Afrika hasa Ethiopia, Kenya na Somalia, lakini sasa wameripotiwa pia kuingia Uganda, huku Sudan Kusini na Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo katika tahadhari.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali inafuatilia kwa karibu suala la nzige wa jangwani, maafisa na wataalamu wapo katika Mikoa ya Kaskazini ukiwemo Kilimanjaro ambako imepakana na Kenya,nchi ambayo tayari imeshambuliwa na wadudu hao.
“Tumejiandaa kwa dawa na ndege mpaka sasa tuna ndege mbili katika hatua hii ya awali, Wataalamu wetu wapo Wilaya zote za mipakani kutoa Elimu na kufanya uchunguzi kwa taarifa yoyote tunayopata hasa pale Wananchi wanapotoa taarifa yoyote ile,” amesema Bashe katika ukurasa wake wa Twitter jana (Februari 11, 2020).
— Hussein M Bashe (@HusseinBashe) February 10, 2020
Sifa za nzige hao wa jangwani
Hata hivyo, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura (OCHA), Mark Lowcock amezitaka jumuiya za kimataifa kushikamana na kupambana janga hilo ili kuzuia madhara ya wadudu hao hasa uharibifu wa mazao.
“Wimbi moja la nzige waliozingira ukubwa wa kilometa moja ambalo linajumuisha nzige milioni 40 hadi milioni 80, wanaweza kula kwa siku moja chakula ambacho kinatosheleza kulisha watu 35,000,” amesema Lowcock.
Amesema wimbi la nzige hao limevuka mpaka na kuingia Uganda huku Tanzania ikitakiwa kuwa katika hali ya tahadhari kwa sababu iko karibu na nchi hizo.
“Kama mjuavyo nzinge ni wadudu wa kale sana ambao uhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na uvamizi wao unaweza kusambaratisha kabisa mazao na malisho haraka sana,” amesema.
Akitolea mfano uvamizi wa nzige hao Kaskazini Mashariki mwa Kenya amesema wimbi moja la nzige lilikadiriwa kuwa ni la ukubwa wa kilometa 2, 400 na nzige hao wanaweza kula chakula ambacho kinaweza kulisha watu milioni 84 kwa siku.
“Nzige hao siyo tu kwamba wana njaa lakini wanasafiri haraka sana, nzige hao hawahusiki na masuala ya uhamiaji, au kuhitaji pasi za kusafiria na wala hawaheshimu mipaka ya kimataifa.
Nzige hao wa jangwani ambao wana urefu wa kidole cha mwanadamu huruka kwa makundi makubwa makubwa wakitafuta lishe.
Zinahusiana:
Shirika la IGAD , limeripoti kwamba kundi moja la nzige huenda linashirikisha wadudu zaidi ya milioni 150 kwa mraba na husafiri kupitia upepo na wanaweza kusafiri kwa zaidi ya kilomita 150 kwa siku.
Lowcock amesema uvamizi wa wimbi la nzige katika Pembe ya Afrika mbayo tayari ilikuwa umeghubikwa na changamoto zingine kama ukame, njaa, mafuriko na machafuko yanayoendelea hivyo imekuwa janga baada ya janga.
Jumuiya ya kimataifa inastahili kushikamana ili kuepusha janga hili ikiwa ni pamoja na kulisaidia shirika la chakula na kilimo FAO ambao linahitaji dola milioni 76 (Sh175.6 bilioni) kupambana na janga la nzige.