Neema ya BoT: Ufahamu mkoba wa ahueni wa kukabiliana na Corona Tanzania
- Miongoni mwa ahueni hizo ni kuruhusu benki na taasisi za fedha kujadiliana na wakopaji juu ya namna ya urejeshaji bora ya mikopo itakayopunguza maumivu.
- Kiwango cha miamala mtandaoni chaongozwa hadi Sh5 milioni kutoka Sh3 milioni.
- Zipo ahueni kwa benki ili kuongeza ukwasi na kuchagiza ukopeshaji wa mikopo wenye riba nafuu.
Dar es Salaam. Ili kukabiliana na madhara ya kiuchumi yatokanayo na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua mbalimbali kupunguza makali ikiwemo kuziruhusu benki kujadiliana na wakopaji wao juu ya urejeshaji mikopo ili kupunguza maumivu.
Gavana wa BoT Prof Florens Luoga ameeleza leo kuwa hatua hizo za kisera zilipitishwa na kamati ya sera ya bodi ya benki hiyo iliyokutana Mei 8 mwaka huu.
“Lengo la hatua hizi ni kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha na upatikanaji wa huduma za fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi,” amesema Luoga katika taarifa iliyotolewa na BoT mapema Mei 12.
Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na benki hiyo ni kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa BoT na benki nchini kutoka asilimia saba (7) hadi asilimia sita (6) kuanzia Juni 8 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Prof Luoga hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ukwasi katika sekta ya benki Tanzania.
Hii ni mara ya pili kwa BoT kushusha kiwango hicho ndani ya mwaka mmoja ili kuzisaidia benki kuwa na ukwasi zaidi.
Zinazohusiana:
- BOT: Marufuku kurusha hovyo noti
- BOT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania
- BoT yaaeleza sababu za kutumia jeshi kukagua maduka ya kubadilishia fedha Arusha
Benki hiyo pia imeshusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa benki kuu kutoka asilimia saba (7) hadi tano (5) kuanzia Jumanne Mei 12.
“Hatua hii itawezesha kuongeza wigo wa benki kukopa kutoka benki kuu kwa riba nafuu na hivyo kupunguza riba ya mikopo kwa wateja,” amesema.
Sanjari na hatua hizo, Prof Luoga amesema wameamua kuongeza unafuu kwenye dhamana na hati fungani za Serikali zinazotumika na benki kama dhamana wakati wa kukopa kutoka benki hiyo.
Katika uamuzi huo, unafuu utapatikana kwa kupunguza kiwango cha dhamana kutoka asilimia 10 hadi asilimia tano kwa dhamana za muda mfupi na kutoka asilimia 40 hadi asilimia 20 kwa hati fungani kuanzia Mei 12, 2020.
“Hatua hii itaongeza uwezo wa benki kukopa kutoka benki kuu kwa unafuu zaidi kuliko ilivyokuwa awali,” amesema bosi huyo wa BoT.
Kwa muda mrefu kumekuwa na maoni ya wadau mbalimbali nchini ya kuitaka BoT kuchukua hatua za kutoa ahueni kwa Watanzania wanaoelemewa na mikopo na masaibu mengine ya kiuchumi katika kipindi hiki kigumu cha COVID-19 huku baadhi wakishauri benki ziahirishe kwa muda urejeshaji wa mikopo iliyochukuliwa na wateja wao.
Has been any #COVID19 intervention from BOT and TRA? Any stimulus package & tax relief? Dona county should do better.
— Thabit Jacob (@ThabitSenior) March 20, 2020
Katika suala hilo la mikopo kwa wakopaji, Prof Luoga ameziagiza benki na taasisi zote za fedha nchini kutathmini kwa kina athari zinazotokana na COVID-19 kwenye urejeshaji wa mikopo, kujadiliana na wakopaji namna ya kurejesha mikopo na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo kwa kadri itakavyoonekana inafaa.
“Benki Kuu itatoa unafuu kwa mabenki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi bila upendeleo,” amesema.
Katika kuongeza matumizi ya huduma za kifedha mtandaoni, BoT imeziagiza kampuni zinazotoa huduma za kifedha mtandaoni kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka Sh3 milioni hadi Sh5 milioni.
Pia, kampuni hizo zinatakiwa kuongeza kiwango cha ukomo wa akiba kwa siku kutoka Sh5 milioni hadi Sh10 milioni.
Prof Luoga amesema benki hiyo itaendelea kufanya tathmini ya athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 katika sekta mbalimbali za uchumi na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari za madhara hayo.