Tanzania kuzalisha wahandisi wabobezi wa madaraja 11
- Watatoka miongoni mwa vijana waojenga daraja la JPM Mwanza.
- Watatumika katika miradi ya kimkakati.
- Aagiza ujenzi wa daraja hilo ukamilike kwa wakati.
Mwanza. Waziri wa Ujenzi na uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha unazalisha wahandisi 11 wa madaraja katika mradi wa ujenzi wa daraja la JPM Kigongo-Busisi mkoani Mwanza.
Wahandisi hao ni wanafunzi wa vyuo vikuu wa fani hiyo wanaofanya kazi katika mradi huo.
Professa Mbarawa ametoa maagizo hayo leo Desemba 15, 2021 alipotembelea daraja la JPM Kigongo-Busisi mkoani Mwanza na kueleza kuwa Serikali itatoa gharama zinazohitajika ili kupata watalam hao ambao watakuwa hazina kwa nchi na kusaidia katika miradi mingine ya kimkakati.
“Tuwape fursa vijana wa kitanzania wanaosoma elimu ya uhandisi katika vyuo vikuu nchini kufanya kazi na kujifunza kupitia mradi huu wa ujenzi wa daraja la JPM Kigongo- Busisi ambalo linajengwa kwa teknolojia ya kisasa,” amesema Mbarawa
Ujenzi wa daraja la JPM kwa sasa limefikia asilimia 34 na kwamba linatarajiwa kukamilika Februar 2024.
Hadi kukamilika, daraja hilo litagharimu zaidi ya Sh699.2 bilioni na litarahisisha huduma za usafiri kwa wakazi wa mikoa ya Mwanza, Gieta na nchi za maziwa makuu ikiwemo Uganda, Burundi na Rwanda.
Amesema ujenzi wa daraja hilo ni shule tosha kwa Watanzania hususani vijana wanaosoma vyuo vikuu na hawapati fursa ya kujifunza kivitendo katika miradi mikubwa ya Serikali.
“Nimeambiwa kuna vijana 11 nataka nione vijana wetu hapa kama 21 wawepo hapa wanafanya kazi kama kuwalipa Sh300,000 kila mwezi siyo tatizo hatuwezi kushindwa kuwalipa tumataka (daraja) lizalishe wahandisi wa madaraja 11 katika maisha yetu, tumejipanga naamini tukiweka mikakati vizuri tutatoa vijana wazuri hapa,” amesema Mbarawa.
Ujenzi wa daraja la JPM Kigongo-Busisi mkoani Mwanza ukiendelea. Picha| Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Uhitaji huo wa wahandisi wa madaraja makubwa ya majini na nchi kavu, unatokana na pengo lililoachwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanroads, marehemu Mhandisi Patrick Mfugale ambaye amehusika katika usanifu na ujenzi wa madaraja zaidi ya nchini.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza, Boniphace Mkumbo amesema watahakikisha maelekezo ya waziri yanafanyiwa kazi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kazi itakayofanyika iwe ya viwango kulingana na makubaliano ya mkataba wa mradi huo.
“Tathimini iko vizuri ingawa inaonekana kazi iko chini kwa asilimia 16 zilizobaki lakini sasa mkandarasi ameongeza wafanyakazi zaidi ya wale waliokuwepo,” amesema Mkumbo
Mkumbo amesema awali wakati daraja linaanza kujengwa kulikuwa na wafanyakazi 461 na sasa wapo 720, vifaa vimeongezwa na vinaendelea kufika kama mpango kazi ulivyo.
Latest