Necta yatangaza matokeo kidato cha nne 2022, ufaulu waongezeka kiduchu
Bado idadi ya waliopata ufaulu mzuri wa daraja la I-III unaowapa fursa zaidi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu bado wapo chini ya nusu.
Dar es Salaam. Ubora wa ufaulu katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022 umeongezeka kiduchu baada ya wanafunzi 456,975, kati ya 520,558 waliofanya mtihani huo kupata madaraja ya I hadi IV kiwango ambacho ni sawa na asilimia 87.8% ya watahiniwa wote.
Kiwango hicho cha ufaulu, kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kimeongezeka kwa asilimia 0.49 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2021 ambapo asilimia 87.30 ya watahiniwa walifaufulu kwa madara la I hadi IV.
Kati ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo mwaka 2022, wasichana ni 243,285 sawa na asilimia 87.08 na wavulana ni 213,690 sawa na asilimia 88.6.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amas amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa ufaulu umepanda kwa asilimia 0.49. Picha|Esau Ng’umbi/Nukta.
Licha ya ufaulu huo kuongezeka kiduchu, bado watahiniwa waliopata daraja la I hadi III bado ni wachache zaidi wasiozidi hata nusu ya watahiniwa wote waliofanya mtihani huo Oktoba mwaka jana.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amas amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo Januari 29, 2023 kuwa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliopata watahiniwa wa shule unaonesha watahiniwa waliopata ufaulu mzuri daraja la I hadi III ni 192,348 sawa na asilimia 36.95.
Hii ina maana kuwa ni watahiniwa 37 tu kati ya 100 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamepata ufaulu mzuri unaowapa fursa zaidi ya kuendelea na elimu ya kidato cha tano au kwenda vyuo vya kati vinavyotoa vyeti na astashahada.
“Mwaka 2021 watahiniwa waliopata ufaulu mzuri kama huo walikuwa 173,422 sawa na asilimia 35.84 hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.11,” amesema Amas.
Kupata matokeo bonyeza hapa.