Ndugulile ataja muelekeo wa uongozi wake WHO, asema jimbo lake halipo wazi

September 3, 2024 1:05 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Aweka vipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya na maandalizi ya kukabiliana na majanga.
  • Apewa miezi sita ya kujiandaa, kuanza kazi rasmi Februari au Machi 2025.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Dk Faustine Ndugulile amesema katika uongozi wake ataweka vipaumbele katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya barani Afrika na kuhakikisha bara hilo linajiandaa vema kukabiliana na majanga makubwa ya kiafya yanayojitokeza kama Uviko 19 pamoja na Mpox.

Nchi nyingi za Bara la Afrika bado zinakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya hususan katika maeneo ya vijijini jambo linalosababisha vifo au ulemavu jambo linalorudisha nyuma juhudi za maendeleo.

Dk Ndugulile aliyekuwa anatoa salamu za shukrani mara baada ya kushinda nafasi hiyo juma moja lililopita bungeni jijini Dodoma leo Septemba 3, 2024 amewaambia wabunge kuwa ataimarisha ushirikiano kati ya WHO na mashirika mbalimbali ikiwemo mabunge ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa huduma za afya.

“Lakini tunakwenda kuimarisha mashirikiano ya taasisi mbalimbali ambazo zinafanyika katika bara la Afrika…katika uongozi wangu mabunge ya Afrika yatakuwa ni sehemu ya kazi ambazo nitakuwa nazifanya nikiwa kiongozi…Tunakwenda kuiboresha WHO kuhakikisha inakuwa imara na kusimamia sekta ya afya katika bara la Afrika kuhakikisha nchi zinanufaika kutokana na nafasi hii,”amesema Dk Ndugulile.

Dk Ndugulile anayetarajiwa kuanza kazi Februari au Machi 2025 atahudumia nchi 47 katika Bara la Afrika zenye zaidi ya watu bilioni 1.5 kwa miaka mitano ambapo huenda akachaguliwa tena iwapo atafanya vizuri katika awamu ya kwanza.

Kiongozi huyo anakuwa wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuchukua kijiti hicho kutoka kwa Dk Matshidiso Moeti ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2014. 

Jimbo lake haliko wazi 

Licha ya kuwashukuru Watanzania na wote walioshiriki kumpigia kampeni iliyomuwezesha kushinda kiti hicho Ndugulile ametumia nafasi hiyo kuutangazia umma kuwa bado ataendelea kuwepo nchini kwa muda wa miezi sita zaidi akijiandaa na nafasi hiyo hivyo jimbo lake la Kigamboni bado halipo wazi.

“Kituo changu cha kazi kitakuwa Congo Brazzaville, utaratibu ulivyo unapewa miezi sita ya kujipanga hivyo natarajia kuanza kazi mwishoni mwa Februari au Machi 2025, wale waliokuwa wanahoji Jimbo la Kigamboni lipo wazi jibu ni hapana! Bado niponipo na wananchi wangu wote waliniunga mkono na walikuwa na dua zao pia.” amesema Dk Ndugulile.

Akizungumzia namna alivyojinadi wakati wa kugombea amesema miongoni mwa mambo aliyogusia ni pamoja na namna Afrika inavyohitaji kuwa na uongozi imara na wenye maono kuhakikisha bara linaweza kufanikiwa, inahitaji mtu mwenye uwezo wa masuala ya kitaaluma, uongozi na sifa zingine.

Katika kinyang’anyiro hicho wagombea wengine walikuwa ni pamoja na Dk Boureima Hama Sambo (Niger) Dk N’da Konan Michel Yao (Cote d’Ivoire), Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).

Dk Ndugulile alitangazwa kuwa mshindi Jumanne Agosti 27, 2024 baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 wakiipigia Senegal, saba (Niger) na nchi saba zikiipigia Rwanda.

Katika matokeo ya jumla ya mzunguko wa pili Dk Ndugulile alipata kura 25, Senegal 14 na Niger kura sita.

Dk Ndugulile ambaye ni mwanateknolojia, mtunga sera, mwanasiasa na mwakilishi wa wananchi, aliwakilisha Tanzania baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwania kinyang’anyiro hicho.

Aidha, Dk Ndugulile, aliyewahi kuwa Waziri wa zamani wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano amekuwa Mbunge wa Kigamboni tangu mwaka 2010 huku akishikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye sekta za afya kutokana na uzoefu wake wa kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks