Ndege za ATCL kuanza safari za Pemba
- Serikali yasema safari hizo zitaanza 2023/24.
- Sababu ni kuongezeka kwa abiria katika kisiwa hicho.
Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) linarajia kuanzisha safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda katika kisiwa cha Pemba, Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kuongeza ushindani katika sekta ya anga nchini na kuongeza wigo wa biashara ya kimataifa.
Kwa muda sasa, ndege za ATCL zimekuwa zikisafirisha abiria na mizigo kwenda Unguja, Zanzibar na siyo Pemba, jambo linaweza kuwa linaikosesha fursa ya kufaidika na mapato katika kisiwa hicho.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema ndege za ATCL zitaanza kusafirisha abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Pemba mwaka wa fedha wa 2023/24.
“Shirika letu la ATCL litaanza safari zake mwaka wa fedha wa 2023/24,” amesema Mwakibete leo Mei 16, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa Shaurimoyo, Ally Juma Mohammed aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuanzisha safari za ndege kuelekea Pemba.
Katika swali lake, Mohammed amesema kwa sasa katika kisiwa cha Pemba kuna ongezeko la watu wanaohitaji usafiri wa ndege, hivyo ni muhimu wakafikiwa.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
Kuanza kwa safari za ndege Pemba kutarahisisha safari za abiria na kuongeza wigo wa biashara kati ya Zanzibar na Tanzania ikizingatiwa kuwa kisiwa hicho kinasifika kwa uzalishaji wa viungo na kina vivutio mbalimbali vya utalii zikiwemo fukwe kwa ajili ya watalii.
Tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021, amekuwa akilifanyia mabadiliko makubwa shirika la ATCL ikiwemo kulipunguzia mzigo wa madeni, kuliwezesha kujiendesha kibiashara ikiwemo kuongeza safari za ndani na nje ya nchi ili kufaidika na fursa za kibiashara za sekta ya anga.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mwakibete, mwaka 2016 kabla ya Serikali kuanza utekelezaji wa mpango wa kuifufua ATCL, shirika hilo lilikuwa linadaiwa Sh141.7 bilioni za watoa huduma mbalimbali wa ndani na nje.
Hadi Aprili 2022, Serikali imelipa madeni Sh127.1 bilioni kati ya madeni hayo.
Latest



