Ndalichako aziwashia moto halmashauri mafao ya wastaafu

July 29, 2022 5:57 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Azitaka kuwasaidia wastaafu kupata mafao yao kwa wakati.
  • Akemea tabia ya kutowasilisha michango ya wafanyakazi.

Mwanza. Serikali imeziagiza halmashauri nchini kuhakikisha zinawasilisha michango ya wafanyakazi wao ili kuwasaidia wastaafu kupata mafao yao kwa wakati pale wanapostaafu.

Akizungumza jijini Mwanza Julai 28, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema halmashauri zote zinatakiwa kuwasilisha michango ya watumishi wao kwa kuwa hilo ni takwa la kisheria.

“Ninaziagiza hizi halmashauri kuhakikisha zinawasilisha michango ya watumishi wake kwa wakati ili kuwasaidia wanapostaafu waweze kulipwa mafao yao,” amesema Prof Ndalichako.

Amesema halmashauri zinaposhindwa kuweka mafao ya wafanyakazi wao kwa wakati wanasababisha wastaafu wadai fidia hizo kwa zaidi ya miaka minne.

Ametaja sababu za watumishi wengi kuchelewa kupata mafao yao ni kutokana na kukosekana michango yao katika mifuko ya jamii.

“Wastaafu wengi wanapata shida kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo halmashauri na sekta binafsi kushindwa kuwasilisha michango yao kwenye mifuko ya jamii,” amesema Prof Ndalichako.

Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako amezitaka sekta binafsi kutochelewesha michango ya wafanyakazi wake katika mifuko ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) jambo ambalo litaondoa usumbufu kwa wastaafu  kulipwa mafao yao.

Amebainisha miongoni mwa malalamiko ya wastaafu hao ni pamoja kupunjwa mafao yao na mtumishi anayestaafu kulipwa kidogo ikilinganishwa na mshahara wa mwisho aliokuwa akiupata kabla ya kustaafu.

Amesema iwapo hali itaendelea kuwa hivi kuna haja ya kubadilisha sheria ili kuwabana waajiri kuhakikisha mtumishi anapostaafu kazi analipwa mafao yake huku watumishi wanaolipwa mafao yao na hazina, Profesa Ndalichako amesema  wizara yake haihusiki nao na kwamba wale wanaomhusu atahakikisha kila mstaafu analipwa mafao yake na michango inawasilishwa kwenye mifuko kwa wakati.

Haindo Ngowi ni mmoja wa wastaafu ambaye alikutana na Waziri Ndalichako ambapo amesema wastaafu wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo ucheleweshaji wa mafao.

Ametaja shida zingine wanazokutana nazo ni pamoja na kupunjwa mafao yao huku akisema suala lao linatakiwa kufanyiwa kazi badala ya kusubiri mpaka waziri akutane nao.

Mstaafu mwingine, Benjamini Makabala ameiomba Serikali kushughulikia mapema matatizo ya  wastaafu kupitia mifuko yao na siyo kusubiri  mpaka serikali kutangaza muda wa kuwasaidia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW