Nape: Wawekezaji jengeni viwanda kupunguza bei za simu janja Tanzania
- Waziri Nape asema bado simu hizo zinauzwa kwa bei ya juu kwa sababu zinaagizwa nje ya nchi.
- Ni asilimia 27 ya Watanzania ndiyo wanatumia simu janja.
- Asema ujenzi wa viwanda utapunguza bei ya simu hizo.
Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa simu janja wakaongezeka Tanzania zitakapoanza kuuzwa kwa bei nafuu, ikiwa wawekezaji watakubali kujenga viwanda vya kutengeneza simu nchini.
Simu janja (smartphones) ni miongoni mwa kifaa muhimu ambacho hutumia intaneti kurahisisha mawasiliano na kuperuzi mtandaoni ili kupata taarifa na kujifunza.
Pia simu hizo zimekuwa zikirahisisha biashara na huduma jumuishi za kifedha na kuokoa muda ambao watu wanatumia kwenda benki.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewakaribisha wawekezaji kutoka Canada kuja kuwekeza katika viwanda vya utengenezaji wa simu janja hapa nchini.
“Eneo ambalo tulitamani kama Serikali kupata wawekezaji ni eneo la upatikanaji wa simu janja (smartphones na tablets) ili ziwe bei nafuu na watu waweze kumudu kununua,” amesema Nape leo Mei 26, 2022 alipokutana na Katibu wa Mambo ya Nje wa Canada, Robert Oliphant.
Wawili hao wamejadili masuala mbalimbali ya habari na teknolojia ya habari ikiwemo kubadilisha uzoefu wa kikazi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Zinazohusiana
- Jinsi ya kubaini kamera zilizofichwa kwenye nyumba ya kupanga, chumba cha hoteli
- Namna ya kupima ugonjwa wa rimoti kwa kamera ya simu
Simu bado zinauza kwa bei ya juu
Kutokana na Tanzania kutokuwa na viwanda vya kutengeneza simu janja, Nape amesema imesababisha vifaa hivyo kuwa na gharama ya juu na kuwazuia Watanzania kuweza kumiliki simu hizo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, ni asilimia 27 tu ya Watanzania ndiyo wanaomiliki simu janja na asilimia inayobaki wanamiliki simu za kawaida, kutokana na gharama ya simu janja kuwa ya juu.
“Sasa imefika wakati simu janja zizalishwe hapa nchini, ili bei iwe ya chini na kila Mtanzania aweze kupata kifaa hicho, na hata huduma ikiboreshwa ina maana watu wengi watapata hiyo huduma,” amesisitiza Nape.
Licha ya wanaomiliki simu janja kuwa chini ya theluthi moja ya Watanzania, watumiaji wa intaneti wanazidi kuongezeka kila mwaka, ambapo hadi Aprili 2022 walikuwa milioni 29.9 kwa mujibu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Katibu wa Mambo ya Nje wa Canada, Robert Oliphant amesema kuwa ili Tanzania iweze kuwa na mawasiliano ya uhakika inatakiwa kuweka vipaumbele eneo la nishati, maendeleo pamoja na watu wenye ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano.
Latest



