Nani kumrithi Moremi Soko la Hisa Dar?
- Ni baada ya bosi huyo kutangaza kuondoka DSE.
- Amefanya kazi na kampuni hiyo kwa miaka tisa.
- Mchakato wa kumpata bosi mpya waanza.
Dar es Salaam. Baada ya kulitumikia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa miaka tisa kama Afisa Mtendaji Mkuu, Moremi Marwa anaachia nafasi hiyo huku akiliacha soko hilo likiwa limeimarika zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi ya DSE iliyotolewa Juni 20, 2022, Moremi anaondoka katika nafasi hiyo baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
“Tangu 2013, Moremi amekuwa na jukumu muhimu katika maendeleo, mabadiliko na mafanikio ya Soko la Hisa kupitia uongozi wake wa kutia moyo,” imeeleza taarifa ya DSE iliyotolewa na Mwenyekiti wa bodi, Dk Ellinami Minja.
Bodi hiyo imesema Moremi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika masuala ya masoko na fedha amekuwa nguzo muhimu ya kukua na kuimarika kwa soko hilo la hisa Tanzania lenye kampuni 29.
“Tutamkosa na tunamtakia kila la heri katika majukumu yake mapya,” amesema Dk Minja.
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
Kabla ya kujiunga na DSE, Moremi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni dhamana Tanzania (TSL) ambapo ameacha alama muhimu katika soko hilo hasa kufanya mabadiliko makubwa ya uendeshaji na ukuaji wa mtaji.
Taasisi ya Academy For Cultural Diplomacy ya Ujerumani imemtaja bosi huyo kuwa ni mwanamageuzi kwa sababu katika uongozi wake aliitoa DSE kutoka katika kupata hasara hadi kuwa kampuni inayojiendesha kibiashara ambayo imejiorodhesha katika Soko la Hisa.
“Mabadiliko haya yanajumuisha ubunifu mpya, nafasi za kimkakati (ndani ya mfumo uliopanuliwa wa kufadhili uwezeshaji wa kiuchumi na ushirikishwaji wa kifedha), na ufanisi katika uwekaji miundombinu ya kielektroniki,” imeeleza taasisi hiyo.
Wakati wa kikao chake cha dharura kilichofanyika Juni 17 mwaka huu, Bodi ya Wakurugenzi ya DSE ilimteua Mary Mniwasa, Mkuu wa Ushauri wa Kisheria kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa DSE.
Mniwasa atahudumu katika nafasi hiyo mpaka atakapopatikana mkurugenzi mtendaji mkuu mpya.
“Tutawajulisha wadau wetu kwa wakati muafaka mara mchakato utakapokamilika,” ameeleza Dk Minja.
Latest