Namna ya kupata mtoto wa jinsia unayotaka

June 30, 2025 5:36 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kutumia kalenda ya mzunguko wa hedhi wa mwanamke na mkao wakati wa tendo. 
  • Njia yoyote ya kupanga jinsia ya mtoto inalenga kuathiri uwezekano wa mbegu fulani kufanikisha safari yake kuelekea kwenye yai.
  • Kabla ya kutumia njia hizo, wanandoa wapate ushauri wa mtaalam wa masuala ya uzazi. 

Dar es Salaam. Neema Gervas (43) ni mama wa watoto watatu. Wote ni wa kike lakini ameishi na kiu ya muda mrefu ya kupata mtoto wa jinsia tofauti. 

“Nilipoona nimepata wa kwanza wa kike, na wa pili pia wa kike, nikasema sasa natamani wa kiume,” anaeleza Neema kwa sauti ya upole. 

Hakuwa na tatizo na watoto wa kike, bali alitamani kuweka uwiano wa jinsia katika familia yake.

Neema hakuwa mbali na wanawake walio katika hali kama yake. Alitafuta ushauri wa mtaani, alisikiliza hadithi za wengine, lakini hakuwahi kuchukua hatua ya kitaalamu au kisayansi kufanikisha suala lake. 

Suala la kutamani kuwa na mtoto wa jinsia fulani sio tatizo, swali kuu ni Je, inawezekana kupanga jinsia ya mtoto kabla ya kushika ujauzito? Na kama inawezekana, kwa namna gani? Picha | Parent Club

“Niliamua kuomba tu ushauri, nikaamini labda safari hii nitapata wa kiume,” anasema. Hata hivyo, matarajio hayo yaligeuka tena kuwa mtoto wa kike jambo alilolikubali kwa moyo wa upendo na ridhaa.

Waswahili husema ‘kitanda hakizai haramu’ na mtoto ni mtoto, hakuna mtoto mbaya. 

Neema ni moja kati ya wanawake wengi wenye matamanio na shauku ya kupanga jinsia ya watoto wao kwa sababu mbalimbali ikiwemo kusawazisha uwiano wa watoto wa kiume na wa kike katika familia zao, au hisia binafsi.

Suala la kutamani kuwa na mtoto wa jinsia fulani sio tatizo, swali kuu ni Je, inawezekana kupanga jinsia ya mtoto kabla ya kushika ujauzito? Na kama inawezekana, kwa namna gani?

Nini huamua jinsia ya mtoto?

Dk Festas Mpojoru kutoka Hospitali ya Kintonka iliyopo jijini Dar es Salaam anaeleza kuwa njia yoyote ya kupanga jinsia ya mtoto inalenga kuathiri uwezekano wa mbegu fulani kufanikisha safari yake kuelekea kwenye yai.

Mtaalm huyo wa masuala ya uzazi anasema kuwa kitaalamu mbegu za mwanaume ndizo zinazobeba siri ya jinsia ya mtoto. 

Mbegu hizo hubeba kromosomu X au Y. Kromosomu X inapokutana na yai la mama, mtoto wa kike huzaliwa (XX), na kromosomu Y inapokutana na yai, mtoto wa kiume huzaliwa (XY).

Kromosomu X inapokutana na yai la mama, mtoto wa kike huzaliwa (XX), na kromosomu Y inapokutana na yai, mtoto wa kiume huzaliwa (XY).

Anasema wanaume hawatakiwi kuwalaumu wanawake inapotokea wanazaa watoto wa jinsia moja kila mara kwani mbegu za baba ndio zinaamua jinsi ya mtoto. 

Nini kinaweza sababisha matokeo ya jinsia aina moja

Mbali na kuwa mbegu za baba ndio huamua jinsia ya mtoto anayezaliwa, zipo sababu zinazoweza kusababisha mbegu hizo kuleta matokeo ya aina moja.

Dk Mpojoru anaweka wazi kuwa matumizi ya muda mrefu ya pombe, sigara au madawa ya kulevya husababisha mbegu kuwa dhaifu na kusababisha matokeo ya kupata mtoto wenye jinsia moja pekee.

Matumizi ya muda mrefu ya pombe, sigara au madawa ya kulevya husababisha mbegu kuwa dhaifu na kusababisha matokeo ya kupata mtoto wenye jinsia moja pekee. Picha | Canva

“Kwa mfano kama baba anatumia sana pombe na sigara kuna uwezekano mkubwa akawa anapata sana watoto wa jinsia ya kike kwa sababu kwa kawaida Kromosomu Y ambayo ndiyo inaamua jinsia ya mtoto kuwa wa kiume ni dhaifu sana kwaiyo inaathiriwa na vitu kama hivyo,” anaeleza Dk Mpojoru.

Tabia ya mbegu na jinsia ya mtoto

Kwa upande wake Dk Landrum Shettles, mtaalamu wa biolojia ya uzazi, katika uchunguzi wake wa masuala ya uzazi na matokeo ya jinsia ya mtoto amegundua mbinu inayolenga kusaidia wanandoa kuathiri jinsia ya mtoto wao kabla ya kushika mimba. 

Njia yake, ambayo imeelezewa kwa undani katika kitabu chake “How to Choose the Sex of Your Baby” inategemea dhana ya utofauti wa tabia ya mbegu za kike na mbegu za kiume.

Mbegu za kiume zina kasi zaidi lakini ni dhaifu, wakati mbegu za kike hazina kasi lakini ni zenye nguvu zaidi. Picha | BBC

Dk Shettles anaeleza kuwa mbegu za kiume zina kasi zaidi lakini ni dhaifu, wakati mbegu za kike hazina kasi lakini ni zenye nguvu zaidi. 

“Mbegu zinazozalisha mtoto wa kiume ni za kasi, ndogo, na zina maisha mafupi kuliko zile zinazozalisha mtoto wa kike.” anasema Dk Shettles.

Katika uchunguzi wake anaeleza kuwa muda wa tendo la ndoa kwa kulinganisha na wakati wa kupevuka kwa yai la mwanamke (ovulation) unaweza kuongeza uwezekano wa kupata jinsia unayokusudia.

Kalenda inasaidia?

Kwa lugha rahisi Dk Shettles anashauri matumizi ya kalenda ya mzunguko wa hedhi ya mwanamke kuwa ufumbuzi au njia inayoweza kutumika kuamua jinsia ya mtoto utakaye mzaa kabla ya kushika ujauzito.

Anapendekeza kwa wanaotamani kupata mtoto wa kiume, kushiriki tendo la ndoa karibu sana na wakati wa ovulation (siku za hatari katika kalenda ya mzunguko wa hedhi kwa mwanamke). 

Kutokana na kasi ya mbegu ya kiume, kushiriki tendo la ndoa siku za hatari katika mzunguko wa hedhi kunaipa nafasi kubwa sana mbegu hiyo kulifikia yai la mwanamke kwa haraka na kurutubisha kabla ya mbegu ya kike kufika ambayo kitabia haina kasi.

Matumizi ya kalenda ya mzunguko wa hedhi ya mwanamke yanaweza kuwa ufumbuzi au njia inayoweza kutumika kuamua jinsia ya mtoto utakaye mzaa kabla ya kushika ujauzito. picha | Canva

Kwa wanaotamani mtoto wa kike, Dk Shettles anashauri kushiriki tendo la ndoa siku mbili hadi tatu kabla ya kuingia siku za hatari katika mzunguko wa hedhi. Dk. Shettles anaeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mwanamke kushika ujauzito katika siku hizo

Hii itaipa nafasi mbegu ya kike kusubiri yai litolewe na kulirutubisha wakati mbegu za kiume zote zina uwezekano wa kuwa zimeshakufa kwa wakati huo.

Je, mkao wakati wa tendo la ndoa husaidia?

Dk Shettles pia amesisitiza umuhimu wa mkao wakati wa tendo la ndoa na mazingira ya uke kama moja ya vitu vinavyoweza kuathiri jinsia ya mtoto atakaye zaliwa. 

Utafiti wake unaeleza kuwa uingizaji wa uume wa kina kwenye uke wakati wa tendo la ndoa husaidia kupata mtoto wa kiume kwa kuweka mbegu karibu na seviksi, ambapo mazingira yake siyo ya asidi na yanafaa zaidi kwa mbegu za kiume.

Mkao wakati wa tendo la ndoa na mazingira ya uke ni moja ya vitu vinavyoweza kuathiri jinsia ya mtoto atakaye zaliwa. Picha | Baby Center UK

Kwa upande mwingine, uingizaji wa juu juu wa uume kwenye uke wa mwanamke unapendekezwa kwa wale wanaotamani mtoto wa kike, kwani huweka mbegu mbali na seviksi, katika mazingira yenye asidi ambayo yanaweza kuathiri mbegu za kiume.

Je, matokeo yakoje ?

Dk Shettles amedai kuwa kiwango cha mafanikio ya mbinu alizofafanua ni asilimia 75 au zaidi kwa wale wanaotafuta mtoto wa kike, na asilimia 80 kwa wale wanaotafuta mtoto wa kiume.

Hata hivyo, tafiti za kisayansi zinaonyesha matokeo tofauti kuhusu ufanisi wa mbinu ya mwanasayansi huyo. Tafiti zingine zinaunga mkono madai yake, wakati nyingine hazionyeshi uhusiano wa moja kwa moja kati ya muda wa tendo la ndoa na jinsia ya mtoto. 

Ingawa mbinu ya Shettles imekuwa maarufu miongoni mwa wanandoa wanaotamani kuchagua jinsia ya mtoto wao, wataalamu wa matibabu wanashauri kuwa inapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari. 

Njia hii si ya uhakika kwa asilimia 100, hivyo wanandoa wanashauriwa kushauriana na mtaalamu wa afya wanapofikiria mbinu za kuchagua jinsia ya mtoto wanayetaka azaliwe.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks