Mzazi, mlezi zingatia haya baada ya matokeo darasa la saba

October 17, 2019 9:05 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Baada ya mtoto wako kumaliza elimu ya msingi ni wakati wa kujipanga utakavyomuendeleza na elimu ya sekondari.
  • Zingatia uwezo wako kiuchumi, heshimu mamuzi ya mwanao na mtafutie shule inayotoa elimu bora.
  • Pata ushauri kwa watu wanaoijua vizuri sekta ya elimu ufanye maamuzi sahihi kwa ajili ya mtoto.

Dar es Salaam. Baada ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba kutoka yakiwa na habari njema kwa asilimia 81.5 ya watahiniwa kufaulu, wazazi na walezi  bado wana kibarua cha kuwaendeleza watoto wao katika elimu ya sekondari.

Wakati wazazi wakijipanga ni jinsi gani watawawezesha watoto wao kuingia kidato cha kwanza mwakani kwa ajili ya safari ya miaka minne ya elimu ya sekondari, yapo mambo muhimu ya kuzingatia ili kufanikisha azma yao.

Baadhi ya mambo hayo ni kipato, shule wanazopenda watoto wao waende na jinsi watakavyomudu gharama na mahitaji ya wanafunzi katika kipindi chote cha masomo. Kama wewe ni mzazi una mtoto aliyemaliza darasa la saba mwaka huu, basi hii inakuhusu:

Fahamu vipaumbele vya mwanao

Kufahamu ni masomo gani mwanao anapenda ni jambo muhimu kwani itakupa mwanga wa namna ya kumsaidia azidi kuyapenda na hata kupanga mikakati ya kuamsha mapenzi yake kwenye masomo mengine.

Unaweza kufanya hivyo kwa kuangalia madaftari yake, hata mwenendo wa matokeo yake utakueleza kupitia masomo aliyokuwa anafauru zaidi akiwa shule ya msingi na kumuwekea msisitizo anapoanza kidato cha kwanza mwakani.

Hii pia itakusaidia katika kumpatia mahitaji yake shule. Mfano, kama mwanao anapenda masomo ya sayansi, itakubidi umenunulie vitabu na vifaa vya kujifunzia masomo sayansi ili kumrahisishia safari yake ya kubobea katika taaluma ya sayansi. 

Tathmini hali yako ya kiuchumi

Japo watu husema “hakuna ajuaye kesho” lakini haijakuzuia kuweka mipango na kutathmini hali yako ya kiuchumi ukilinganisha na malengo ya kielimu uliyonayo kwa mtoto wako.

“Wazazi wengi huwapeleka watoto wao shule za gharama bila kufanya tathmini ya kipato chao na kama kipato hicho ni endelevu.

Mara nyingi wanapokwama wanawarudisha watoto wao shule za Serikali na “kudiscourage” (kuharibu) muenendo wao” amesema Verediana George mkazi wa Dar es Salaam ambaye kwa 2020, mwanaye anatazamia kuingia darasa la sita.

Mpeleke mtoto wako shule unayoweza kumudu kulipa ada lakini iwe inatoa elimu bora inayoweza kumsaidia mtoto kutimiza malengo yake. 

Wakati mwingine inahitaji kujitoa zaidi ya uwezo ili kumtengenezea mstakabali mzuri mtoto wako. 

Kufahamu ni masomo gani mwanao anapenda ni jambo muhimu kwani itakupa mwanga wa namna ya kumsaidia azidi kuyapenda na hata kupanga mikakati ya kuamsha mapenzi yake kwenye masomo mengine. Picha|Mtandao.

Fanya utafiti wa shule kabla ya kumpeleka mtoto wako

Ni muhimu kufanya utafiti wa kina kuhusu shule unayopenda mtoto wako asome, angalia mazingira na ufundishaji wake lakini inafanya vizuri katika matokeo ya mitihani kitaifa?

Yote hayo ni muhimu ili kuhakikisha, gharama utakazotumia kumsomesha zilete matunda yaliyokusudiwa. 

Mdau wa masuala ya uchumi na utawala kutoka kampuni ya DMA Africa. Haika Mjema ambaye ni mama wa watoto wawili amesema katika kuhakikisha mwanaye anajiendeleza kielimu anazingatia ufaulu wa shule kwa mfululizo wa miaka kadhaa, idadi ya waalimu na mazingira ya shule.

Unaweza kuyapata yote haya kwa kufanya utafiti hata kwa njia ya mtandao au kwa kuulizia kwa ndugu jamaa na marafiki.


Zinazohusiana:


Usimchagulie mwanao masomo ya kusoma

Kwa mujibu wa Mjema, matokeo ya kumlazimisha mtoto asome masomo anayotaka mzazi siyo mazuri kwa sababu hawezi kuwa furaha na anaweza asitimize ndoto zake.

Kumlazimisha mtoto kusoma masomo ambayo hayawezi, hayapendi inaweza kumfanya kuwa mtumwa hapo mbeleni akiwa kazini na hivyo kukosa furaha na kazi yake na hata kuharibu utendaji wake wa kazi.

“Endeleza anachokipenda. Ukimlazimisha ataishia kufanya kazi asiyoipenda” amesma Mjema.

Hata hivyo, ni muhimu kumuongoza vema mtoto katika njia sahihi ya elimu huku ukimuonyesha faida na hasara ya maamuzi anayofanya kwa kila jambo analofanya akiwa masomoni.

Epuka kufuata mkumbo

Wapo majirani zako, jamii inayokuzunguka, ndugu na hata marafiki watakaofikiria tofauti tofauti kuhusu elimu ya mtoto wako.

Ni vema kusikiliza ushauri wao lakini mwenye maamuzi ni wewe kuhusu jinsi utakavyofanikisha upatikanaji wa elimu bora ya mtoto wako. Wapo watakaokatisha masomo ya watoto wao kwa sababu nyingi ikiwemo uchumi na zingine. 

Mzazi bora ni yule anayefikiria mazuri kwa mwanaye. Ni muhimu kufanya maamuzi sahihi na ni dhahiri kuwa maamuzi hayo unayafahamu kwani ni maamuzi ya kumsomesha mwanao. Urithi mzuri kwa mtoto wako ni elimu bora. 

Endelea kupata dondoo muhimu kupitia ukurasa huu kwani “yanayokuhusu” ndiyo kitu tunachosimamia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW