Mzazi au muoaji: Nani alipe mahari?

March 5, 2023 12:52 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

  • Asilimia 50.7 ya Watanzania wanasema wazazi wanapaswa kuwalipia mahari watoto wao.

Dar es Salaam.  Zaidi ya nusu ya Watanzania wanapendekeza kuwa wazazi wanapswa kuwalipia mahari vijana wao wanaotaka kuoa, ripoti mpya ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza. 

Ripoti ya Utafiti wa Taasisi za Kijamii na Jinsia (SIGI) ya mwaka 2021 iliyotolewa hivi karibuni na NBS imeeleza kuwa asilimia 50.7 (Watanzania watano kati ya 10) ya Watanzania wanafikiri kuwa wazazi ndiyo wenye jukumu la kumtolea mahari kijana anayeoa.

Hata hivyo, asilimia 48.4 ya Watanzania wanafikiri hilo ni jukumu la mtu anayeoa na siyo wazazi.

Wakati kukiwa na maoni yanayokaribiana kuhusu mtu wa kulipa mahari, ripoti hiyo inaeleza kuwa baba wa binti anayeolewa ndiye mwenye nafasi kubwa ya kupanga kiwango cha mahari kinachopaswa kutolewa kutoka upande wa muoaji.

Utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano wa Shirika la Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (OECD) na Kituo cha Maendeleo na Wanawake wa Umoja wa Mataifa (UN Women Tanzania) umeeleza kuwa asilimia 46.1 ya Watanzania wanafikiri baba wa binti anayeolewa ndiye mwamuzi wa mwisho kuhusu suala la mahari huku asilimia 43.2 wakisema wazazi wote wawili (baba na mama) wana haki ya kupanga mahari.

Licha ya baba kupewa nafasi kubwa ya kupanga mahari, Watanzania nane kati ya 10 wanafikiri wazazi wote wawili wana haki ya kupokea mahari ya binti yao anayeolewa huku asilimia 13 wakisema anayeolewa ndiye apokee mahari.

 

Vipi kuna ulazima wa kutoa mahari?

SIGI inaeleza kuwa asilimia 92 ya idadi ya watu wanakubali au wanakubali kabisa kuwa

ndoa inahitaji mahari huku Watanzania saba kati ya 10 wanakubaliana au wanakubaliana sana kuwa ikiwa mtu atalipa mahari kwa mkewe inamaanisha kuwa anaweza kuwa na udhibiti kamili juu yake. 

“Asilimia ya watu ambao wanakubali au wanakubali kabisa kuwa ndoa inahitaji mahari ni kubwa zaidi Zanzibar (asilimia 99.8) kuliko Tanzania Bara (asilimia 91.8) na asilimia ya watu wanaokubali au wanakubali sana kuwa ikiwa mwanaume analipa mahari kwa mkewe inamaanisha kuwa anaweza kuwa na udhibiti kamili juu yake iko juu Tanzania

Bara (asilimia 74.1) kuliko Zanzibar (asilimia 44),” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Wewe unafikiri mahari ni lazima?

Enable Notifications OK No thanks