Ni kweli wachawi wapo? Tazama filamu hii
- Ni filamu ya “Witches” ambayo dhima yake ni kuelimisha watoto juu ya kujiamini.
- Filamu hii imejaa nguli wa kuigiza akiwemo Anne Hathaway na Chris Rock.
Dar es Salaam. Endapo unawaza nini ufanye ili kutumia muda wako na mtoto wako wikiendi hii, basi usiwaze kwani Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ipo kwa ajili ya kurahisisha maisha yako.
Kutumia muda wako na mtoto wako wikiendi hii, unaweza kumpeleka katika kumbi za sinema kuangalia filamu ya “Witches” ambayo inaweza kumjenga kujiamini katika shughuli zake.
Iko hivi, Hero Boy (Jahzir Kadeem) amefiwa na wazazi wake na hivyo, njia pekee aliyobaki nayo ni kuishi na bibi yake Grandma (Octavia Spencer). Siyo rahisi.
Grandma anachukua muda mwingi sana kumtoa Hero Boy kwenye huzuni za msiba wa wazazi wake na kumchangamsha kwa namna moja ama nyingine.
Hata hivyo, siku zote furaha yako haifurahiwi na watu wote na kwa Hero Boy na bibi yake, furaha yao inamtesa sana jirani yao ambaye ni miongoni mwa wanachama wa umoja wa wachawi au kwa lugha iliyopanda ndege, “Witches”.
Baada ya mwanachama huyo kufikisha habari kwa wakuu wake, chama kizima kinaamua kuanza safari ya kuwawinda watoto wote ili wageuzwe kuwa panya na kama ilivyo kuwa kwa watu wengi, panya hukimbizwa na kupigwa na mafagio hadi auwawe.
Hilo ndilo lilikuwa lengo la mchawi mkuu, Grand High Witch (Anne Hathaway). Kuwabadili watoto wote kuwa panya na kisha wazazi wafanye kazi ya kuwauwa ili dunia ibaki bila viumbe wenye furaha ya kweli.
Njia ya kuwabadisha watoto hao ni kwa kuweka dawa zake kwenye vitu ambavyo watoto hupenda sana vikiwemo pipi na peremende.
Mpango wake unafanikiwa na Hero Boy pamoja na rafiki yake Bruno Jenkins, wanabadilishwa kuwa panya ambao safari yao inakuwa na mushkeri huku wakikwepa kupigwa na mafagio na kuponea chupuchupu kwenye mitego ya panya inayowekwa kwa ajili yao.
Soma zaidi:
- Zingatia haya kabla ya kuchagua rangi ya nyumba yako
- Vimbwenga vya babu na mjukuu havijawahi kumuacha mtu salama
- Unavyoweza kukabiliana na vipele vinavyotokana na kunyoa ndevu
Somo atakalopata mtoto wako
Ni pamoja na kutokukata tamaa kama inavyoonyeshwa na Hero Boy na rafiki yake Bruno.
Watajifunza kuthamini familia na kuwapenda watu waliobaki kwa ajili yao.
Itawaelezea kwa namna yake kujiandaa na ulimwengu na pia kutokuogopa matatizo.
Filamu hii iliyojaa burudani na matukio ya kukukonga moyo ilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1987 na mwaka huu, imekuja kwa namna nyingine. Itazame na utuandikie kupitia kurasa zetu za kijamii ipi imekubamba zaidi.