Rais Samia: Taasisi ya Sayansi za Bahari kukuza uchumi wa buluu
- Asema maendeleo yanapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii inayokizunguka, hususan kupitia ajira, biashara na shughuli za kijamii zitakazoongeza kipato cha wananchi.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kunatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa buluu.
Kiongozi huyo wa nchi aliyekuwa akizungumzana wahudhuriaji wa uzinduzi wa majengo ya taasisi hiyo katika kampasi ya Buyu, Zanzibar, leo Januari 8, 2026 amebainisha kuwa uwepo wa chuo hicho utakuza uchumi wa jamii za pembezoni hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.
“Uchumi wa buluu ni nguzo muhimu katika kukuza pato la taifa na kuongeza fursa za ajira, hivyo uwekezaji uliofanywa katika taasisi hiyo utaisaidia nchi kuchochea uchumi jumuishi” ameongeza Rais Samia.
Kauli ya Rais Samia inakuja wakati ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewekeza nguvu kubwa katika kukuza uchumi wa buluu unaotegemewa na mamia ya wakazi wa kisiwa hicho.
Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024, Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na uchumi huo ikiwa masuala ya utafiti, uhawilishaji wa teknolojia na uwezeshaji wa watalaamu utafanyika kikamilifu.
Huenda ujenzi wa kampasi hiyo ya UDSM visiwani Zanzibar ikafanikisha baadhi ya masuala hayo ikiwemo kutoa kozi za muda mfupi kwa jamii inayozunguka chuo hicho kama alivyosisitiza Rais Samia,
“Taasisi inapaswa kuwa kichocheo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Buyu na maeneo ya jirani…hususan kwa wananchi wa maeneo yananyozunguka chuo ambao tayari wanajishughulisha na shuhuli za bahari.” amesema Rais Samia.
Mbali na kusisitiza hilo Rais Samia amesema kuwa kuwa Taasisi ya Sayansi za Bahari imeendelea kuwa mhimili muhimu katika tafiti zinazohusiana na uvuvi endelevu, hifadhi ya mazingira ya bahari, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kukuza utalii wa bahari.
Ameongeza kuwa tafiti na maarifa yatakayozalishwa katika taasisi hiyo yatasaidia kufanya maamuzi bora ya sera yanayolinda rasilimali za bahari, huku yakiongeza tija na kipato cha wananchi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Ananginsye amesema ujenzi wa chuo hicho kumeongeza idadi ya wanafunzi watakao kudahiriwa chuoni hapo.
Profesa Anangisye amesema kuwa kwa sasa chuo hicho kinauwezo wa kuhudumia wanafunzi 472 kutoka wanafunzi 172 waliokuwa wakihudumiwa hapo awali, sawa na ongezeko la wanafunzi 300.
Latest