Serikali yakemea ukamataji holela wa bodaboda, bajaji
- Yasema ukamataji huo ni kinyume na taratibu.
Dar es Salaam. Serikali imekemea vitendo vya ukamataji holela wa vyombo vidogo vya usafiri ikiwemo bodaboda, bajaji na baiskeli wakati dereva anapobainika kufanya makosa ya barabarani.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, aliyekuwa akizungumza na madereva wa bodaboda na bajaji leo Januari 8, 2026 amesema ukamataji huo unazorotesha uchumi wa makundi hayo.
“Twende na utaratibu ule ule ambao tumekubaliana lakini pia kama tumekubaliana kwamba hili ni kosa na lina faini mpeni kitendea kazi chake ili akatafute fedha…
…Huna haja ya kushikiria kitendea kazi chake,” amesema Dk Nchemba katika kongamano la mwaka la wamachinga na madereva wa vyombo vidogo vya usafiri wa abiria jijini Dar es Salaam.
Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kutoa kauli hiyo, kwa madereva bajaji na boda boda nchini Tanzania.
Itaumbukwa Desemba 29, 2025, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko na kituo cha mabasi eneo la Bunju B, aliagiza kuwa magari, bajaji na bodaboda zishikiliwe na polisi pale tu zitakapobainika kuhusika na uhalifu wa kutumia silaha.
“Kama amebeba wauaji wa silaha na hiyo bodaboda ni dhamana basi ishikiliwe, imebeba dawa za kulevya ishikiliwe, lakini kama ni jambo la faini mpeni bodaboda yake akatafute hiyo faini awalipe,” alisema Dk Nchemba.
Pamoja na hayo amekemea kuwazungusha madereva kwenye masuala ya leseni au huduma nyingine akibainisha kuwa ni dalili ya uzembe na matumizi mabaya ya madaraka.
Mamalishe wakumbukwa
Akizungumzia upande wa mama lishe, Dk Nchemba amesema Serikali inatambua changamoto wanaozipitia ikiwemo za kusumbuliwa na mgambo pamoja na maafisa wengine wa usalama akihidi kuzitafutia suluhu.
“Nawaheshimu sana mama lishe. Natambua mchango wao na sitaki kuona wakisumbuliwa…
…Nawakitokea migambo wale wanaowasumbua sumbua akigusa sahani yako mwambie umegusa sahani ya mke wa Waziri Mkuu hapa,” amesema Dk Nchemba.
Katika hatua nyingine, Dk Nchemba amesema Serikali itaendelea kulinda maslahi ya Watanzania kwa kuhakikisha fursa za ajira zinawanufaisha wananchi wa ndani, huku ikichukua hatua dhidi ya wageni wanaokiuka sheria na kunyima Watanzania ajira.
Hayo yameungwa mkono na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ambapo amesema wizara yake itaongeza ushirikiano na wizara nyingine husika kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara, kurahisisha vigezo na kurasimisha wafanyabiashara wadogo wadogo ili waweze kupata fursa zaidi za kiuchumi.
Latest