Mtanzania ateuliwa naibu mkurugenzi mtendaji wa UNEP

December 28, 2022 6:10 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Kabla ya kujiunga na UNEP mwaka 1994, Elizabeth  Mrema alifanya kazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania kama mshauri na wakili mwandamizi wa kisheria. Picha | UN News.


  • Ni Elizabeth Mrema kutoka Tanzania.
  • Alikuwa katibu mtendaji wa sekretarieti ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bayoanuai (CBD).
  • Ana Shahada ya Uzamili ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, Halifax, Canada.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) António Guterres ametangaza uteuzi wa Elizabeth Mrema kutoka nchini Tanzania kuwa naibu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP). 

Guaterres kupitia taarifa iliyotolewa Disemba 27, 2022 na msemaji wake mjini New York Marekani amesema Mrema atamrithi Joyce Msuya kutoka Tanzania aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa katibu mkuu msaidizi wa masuala ya kibinadamu na naibu mratibu wa misaada ya dharura katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya Kibinadamu  (OCHA). 

Guterres amesema Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mashirika wa UNEP, Sonja Leighton-Kone ataendelea kuwa kaimu naibu mkurugenzi mtendaji hadi Mrema atakaposhika nafasi hiyo. 

Tangu mwaka 2020, Mrema amehudumu kama katibu mtendaji wa sekretarieti ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bayoanuai (CBD) yenye makao yake makuu mjini Montreal, Canada.  

Pia aliwahi kuwa kaimu katibu mtendaji wa sekretarieti ya CBD na mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria wa UNEP huko Kenya, pamoja na kuwa katibu mtendaji wa sekretarieti ya mkataba wa sekretarieti ya wanyama wanaohama yenye makao yake makuu mjini Bonn, Ujerumani. 

Guterres amesema akiwa na tajriba ya zaidi ya miongo miwili ndani ya UN, Mrema analeta uzoefu mkubwa katika sheria ya kimataifa ya mazingira na utungaji sera, utekelezaji wa programu za mazingira na maendeleo endelevu na ujuzi wa kina katika usimamizi na uongozi wa michakato ya kimataifa ya mazingira. 

Kabla ya kujiunga na UNEP mwaka 1994, Mrema alifanya kazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania kama mshauri na wakili mwandamizi wa kisheria.  

Wakati akiwa wizarani, aliwahi pia kuwa mhadhiri wa masuala ya sheria ya kimataifa ya umma na diplomasia ya mikutano katika Kituo cha Ushirikiano wa Masuala ya Nje na Diplomasia cha Tanzania. 

Mrema ana Shahada ya Uzamili ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, Halifax, Canada, Stashahada ya Uzamili ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia kutoka Kituo cha Ushirikiano wa Masuala ya Nje na Diplomasia cha Tanzania na Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam (UDSM). 

Baada ya tangazo hilo la uteuzi, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen amempongeza Mrema ambapo kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema “Pongezi zangu za dhati kwa mfanyakazi mwenzangu Bi. Mrema kutoka Tanzania ambaye ameteuliwa kuwa naibu mkurugenzi mtendaji wa UNEP. Ninatarajia kwa hamu kufanya kazi na Elizabeth wakati tunasaka kuzidisha hatua kwa ajili ya watu na sayari yetu.” 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

Nukta TV