Mtandao wa Baidu kuvitangaza kimataifa vivutio vya utalii Tanzania
- Vitaanza kutangazwa katika mtandao huo wa China Septemba mwaka huu ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea Tanzania.
- Tayari wataalam wa kampuni ya Baidu wapo nchini kupiga picha za vivutio.
- Watatengeneza makala za uzuri wa Tanzania na kuzionyesha duniani.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Thomas Mihayo, amesema kuanzia sasa vivutio vya Tanzania vinaanza kuonekana katika mtandao wa Baidu wa China, ikiwa ni hatua ya kuongeza mapato na idadi ya watalii kutoka nchi hiyo wanaokuja nchini kila mwaka.
Tanzania imepata fursa hiyo baada ya kuchaguliwa kuingia katika mradi wa kampuni ya Baidu wa “Wander Planet” unaohusisha upigaji wa picha jongevu na mnato wa vivutio vya utalii Tanzania ili kuweza kuvitangaza katika mtandao huo wenye wafuasi zaidi ya milioni 700.
Jaji Mihayo aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 1, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema kuwa utengenezaji wa makala na picha mbalimbali kutoka katika vivutio vya hapa nchini vitaweza kuongeza watalii kutoka China kwani picha hizo zitaonekana kwa watumiaji wa mtandao huo.
“Safari hii timu ya wataalam 11 kutoka katika kampuni kubwa za kimtandao nchini humo (Baidu) waliwasili nchini Agosti 22,2019 na kutembelea baadhi ya maeneno ya vivutio vya utalii hapa nchini kwa lengo la kupata picha jongevu na mnato ili kutangaza vivutio hivyo kwenye soko la utalii wa zaidi ya watu milioni 700 wanaoufuatilia mtandao huu wa Baidu”, amesema Jaji Mihayo.
Lengo la TTB ni kuiwezesha sekta ya utalii kupata watalii wengi kutoka China wanaokuja kuitembelea Tanzania kutokana na kuona vivutio vitakawekwa kwenye mtandao wa Baidu kuanzia Septemba 2019 na kuendelea.
Mihayo amesema kuwa kati ya nchi saba duniani Tanzania imeibuka kuwa nchi ya kwanza katika mradi huo na ndiyo nchi pekee kutoka bara la Afrika na nchi zingine zinazolengwa na mradi huo ni kutoka mabara ya Amerika, Asia na Ulaya.
“Takwimu za Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) zinaonesha kuwa China ni nchi ambayo ina soko kubwa la utalii duniani, mwaka 2018 Wachina milioni 130 walisafiri nje ya nchi huku Tanzania ikipokea watalii 32,773 idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watalii hao kutoka China kwenda nchi zingine, kwa hiyo juhudi hizi zinafanyika ili kuliteka soko la China kwenye sekta hii muhimu,” amesema Jaji Mihayo.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Tanzania yaangazi masoko 18 kukuza utalii duniani
Wakiwa nchini wataalam hao wa mambo ya picha jongevu na mnato walipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini ikiwemo mji wa kihistoria Bagamoyo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Makumbusho ya Oldvuai Gorge, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ziwa Manyara, mji wa Mwanza na Zanzibar.
Kiongozi wa msafara huo kutoka kampuni ya Baidu, Jin Xiaping amesema wamekuja Tanzania ili kuona jinsi gani wataweza kutekeleza mradi huo wa kupiga picha jongevu na mnato na sasa wamefanya kazi yao, kwa hiyo kuanzia Septemba hii wataweza kuweka kwenye mtandao wao wa Baidu na kutangaza uzuri wa Tanzania kwenye soko la utalii China.
“Wataalam hawa 11 kila mmoja ana zaidi ya wafuasi milioni mbili kwenye mitandao ya kijamii, kwa hiyo wamepiga picha jongevu, mnato na wataandika makala mbalimbali ili kuziweka kwenye mitandao yao na kuwezesha wafuasi wao kufahamu vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania,” amesema Xiaping.
Latest