Msukumo binafsi: Njia rahisi ya kuacha uvutaji wa bidhaa za tumbaku
- Baadhi ya wadau wameshauri matumizi ya sigara za kielektroniki ili kuacha sigara za kawaida.
- Wataalam wa afya wamesema sigara hizo bado zina madhara kwa afya ya binadamu.
- Msukumo binafsi na dhamira ya dhati ndiyo inayoweza kumsaidia mtu kuacha matumizi ya tumbaku.
Dar es Salaam. Kutokana na madhara ya matumizi ya tumbaku na ugumu uliopo wa kuacha matumizi ya bidhaa zake, mjadala umeibuka miongoni mwa wadau wa njia zipi zitumike ili kuwasaidia watumiaji wa bidhaa hizo kuacha kuzitumia.
Baadhi ya njia hizo ni pamoja na matumizi ya sigara za kielektroniki (E-cigarattes) na njia asilia za mtu binafsi kupunguza matumizi ya bidhaa za tumbaku hadi atakapoacha kabisa.
Hata hivyo, bado watumiaji wa bidhaa za tumbaku zikiwemo ugoro na sigara wameendelea kuwa na sintofahamu kwani baadhi ya njia zilizopendekezwa, bado hazifanyi kazi hata walipojaribu kuzitumia.
Mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Jumanne Mtakashari (29) ambaye ni mvutaji wa sigara amesema sigara za kielektroniki (e-cigarette) zinazoaminika kama mbadala wa sigara za kawaida hazipatikani kwa urahisi ikilinganishwa na sigara za kawaida.
“Nikitaka sigara si naenda kwenye kibanda cha Mangi tu hapo, sasa ladha za sigara hizo hadi niende kwenye maduka makubwa, niichaji na mengineyo. Tabu yote ya nini?,” amehoji Mtakashari.
Mara nyingi, watumiaji wa bidhaa za tumbaku huendelea kuzitumia bidhaa hizo kutokana na kiambata cha “nicotine” kinachopatikana kwenye zao hilo, jambo linalowafanya kuendelea kuwa mateja wa bidhaa hizo na kuwaweka katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya.
Sigara za kielektroniki zinaondoa baadhi ya madhara kwa kuwa zinaitenga “nicotine” na vitu vingine vikiwemo karatasi na majani ambavyo ndiyo chanzo cha moshi unaosababisha madhara makubwa yakiwemo matatizo ya moyo. Picha| Istok.
Wakati baadhi ya watu wakipendekeza sigara za kielektroniki kama njia mbadala ya tumbaku, wataalamu wakiwemo madaktari wamesema sigara hizo kwa kiasi fulani zinapunguza madhara anayoyapata mtumiaji lakini siyo suluhisho la kuacha kuvuta sigara.
Daktari kutoka kliniki ya kimataifa ya Dar es Salaam (IST clinic), Dk Bernadette Kleczka amesema sigara za kielektroniki zinaondoa baadhi ya madhara kwa kuwa zinaitenga “nicotine” na vitu vingine vikiwemo karatasi na majani ambavyo ndiyo chanzo cha moshi unaosababisha madhara makubwa yakiwemo matatizo ya moyo.
“Hizi zinapunguza madhara ya mvuta sigara kwenda kwa mtu ambaye yupo karibu naye. Hazina moshi ambao ni mbaya kwa jirani,” Dk Kleczka ameieleza Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Hata hivyo, daktari huyo amesema kumekuwepo na ripoti zilizoonyesha kuwa bado sigara hizo zinasababisha madhara kwenye mapafu.
“Kuliibuka ugonjwa wa mapafu unaosababishwa na E-ciggaretes nchini Marekani. Hata hivyo, sigara hizo bado hazina madhara makubwa ikilinganishwa na sigara za tumbaku,” amesema Dk Kleczka.
Zinazohusiana
- Tumbaku: ‘Rafiki wa mashaka’ anayeiweka Tanzania njia panda
- Kwanini vijijini wanaongoza matumizi ya tumbaku Tanzania?
- Tumbaku inavyohatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni 2 Tanzania
Licha ya kuwa baadhi wanaona kuwa e-cigarrate ni mbadala, wataalamu wengi wa afya wanashauri watumiaji kuachana kabisa na matumizi ya tumbaku kwa awamu ili kutoathirika zaidi na uraibu.
Unawezaje kuacha kutumia bidhaa za tumbaku?
Bila shaka wapo watu ambao wamejaribu kuacha kutumia sigara na bidhaa zingine za tumbaku lakini wameshindwa kufanya hivyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mazoea ambayo yamegeuka kuwa tabia.
Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani (GATS) ya mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Ofisi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanziabar (OCGS) imeeleza kuwa miezi 12 kabla ya kufanyika utafiti huo, asiliami 76.8 ya wavutaji walipanga kuachana na uvutaji wa tumbaku lakini ripoti hiyo haijasema kama waliacha.
Pia, utafiti huo unaeleza kuwa asilimia 36.5 ya wavutaji wa tumbaku waliotembelea vituo vya afya nchini ndani ya miezi 12 kabla ya utafiti walishauriwa kuacha kutumia bidhaa hizo kwa sababu ya madhara yanayoweza kuwapata.
“Tumbaku inasababisha uteja na hivyo ni muhimu kuimarisha mifumo ya kutoa huduma za afya kuhimiza watu kupunguza matumizi ya bidhaa hizo,” imesomeka sehemu ya ripoti ya GATS.
Naye mkazi wa Jijini Dar es Salaam Reighn Lotfin ambaye anatumia sigara mara moja moja amesema anawafahamu marafiki zake ambao wamejaribu kuacha kuvuta sigara na wakashindwa.
“Wote waliacha kwa sababu mama, baba, mjomba, jamii imewaambia waache kuvuta sigara. Hawakuamua kuacha. Muda kidogo tu walirudi kwenye matumizi” amesema Lotfin.
Lotfin amesema anawafahamu ambao walidhamiria kuacha sigara kutoka moyoni na walifanikiwa kwa kupunguza matumizi na baadaye kuacha kabisa.
“Hauwezi kukata matumizi ya sigara au bidhaa za tumbaku “Paap” kwa asilimia mia.
“Ninafahamu kuna vitu vinaitwa “Nicotine bars” na “Nicotine patches” ambazo mtu akitaka kuacha sigara anapewa atumie. Zipo za kubandika mwilini na zingine za kutafuna. Anakuwa anaacha taratibu,” amesema Lotfin.
Binti huyo ameeleza kuwa, “Nicotine bars” na “Nicotine patches” ni bidhaa ambazo zinakuwa na dawa (drug) ya nicotine ambazo mtu akizitumia, anapata msisimko kama aupatao akivuta sigara.
“Nicotine bars” na “Nicotine patches” ni bidhaa ambazo zinakuwa na dawa (drug) ya nicotine ambazo mtu akizitumia, anapata msisimko kama aupatao akivuta sigara. Pucha| FEPblue.org.
Naye mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Beno Nkwama ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kuacha kuvuvuta sigara au kutumia bidhaa za tumbaku ni maamuzi binafsi.
Pale mtu anapopata sababu ya kwanini anatakiwa kuacha sigara, ndipo maamuzi hayo huwa rahisi kufanyika.
“Kwa wenzetu (mataifa ya nje) wanakuwaga na vikundi kwa ajili ya kuelimishana (theraphy groups) na kupeana mbinu ambazo wamezitumia kuachana na matumizi ya sigara. Kwa huku kwetu sijawahi kuvisikia lakini vikundi hivyo vitasaidia sana watu,” amesema Dk Nkwama.
Amesema pale mtu anapopata uzoefu kutoka kwa mwenzake ambaye amefanikiwa kuacha, inampa moyo kuwa na yeye anaweza.
Nacho Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia magonjwa (CDC) cha nchini Marekani kimeeleza kuwa, unaweza kuanza kupunguza matumizi ya sigara na bidhaa zingine za tumbaku kwa kuwa na mpango mkakati kwa kuweka ratiba na kudhibiti mshawasha binafsi kwa kujihusisha na vikundi vya mazoezi na kufanya matembezi ya muda mrefu.
Latest