Msimu wa baridi kuwanufaisha wavuvi Tanzania

June 9, 2020 9:14 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • TMA yasema joto katika bahari ya Hindi katika msimu huo litakuwa juu ya wastani.
  • Hali hiyo itaongeza tija katika shughuli za uvuvi katika ukanda wa Pwani. 
  • Wananchi wakumbushwa kutumia maji vizuri ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza. 

Dar es Salaam. Wavuvi wa Tanzania wanaotumia bahari ya Hindi wametakiwa kujipanga kuongeza kasi ya uzalishaji wa samaki kutokana na hali ya joto la bahari linalotarajiwa katika msimu wa kipupwe ulioanza mwezi huu wa Juni. 

Msimu wa kipupwe ambao ni miezi ya Juni hadi Agosti (JJA) huwa ni kipindi cha baridi, ukavu na upepo kwa maeneo mengi nchini Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi amesema kutokana na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani, wanatarajia ongezeko la tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu huu.

“Kwa ujumla katika kipindi cha Juni, Julai na Agosti 2020 hali ya joto inatarajiwa kuwa ya kawaida hadi juu kidogo ya kiwango cha kawaida katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani. Hali hiyo inamaanisha uwepo wa vipindi vichache vya baridi ikilinganishwa na wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya Juni-Agosti katika maeneo hayo,” amesema Dk Kijazi. 

Hali hiyo ya hewa katika ukanda wa Pwani ambao uko katika mwambao wa bahari ya Hindi utawafaidisha wavuvi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Tanga kwa sababu samaki watazaliana kwa wingi. 

Katika msimu wa mwaka huu, Dk Kijazi amesema vipindi vya upepo unaovuma kutoka kusini-mashariki na mashariki (Matlai) vinatarajiwa katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya mwambao wa pwani hususan mwezi Agosti, 2020. 

Vipindi vya upepo wa Matlai vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa Pwani. 

Uvuvi katika bahari ya Hindi ni miongoni ma shughuli zinazowapatia wananchi wa ukanda huo kipato. Picha| K15 Photo. 

Huenda mabadiliko hayo ya hali ya hewa yakachangia katika kuwapatia wavuvi uhakika wa chakula, lishe, kuongeza kipato, fedha za kigeni na kupunguza umaskini katika maeneo yao.

Katika mwaka 2019, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.71 ya Pato la Taifa na ilikua kwa asilimia 1.5 licha ya kuwa samaki wanapatikana kwa wingi nchini. 

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kuwa wingi wa samaki katika maji ya Tanzania umeongezeka kutoka tani milioni 2.8 mwaka 2018/2019 hadi kufikia tani milioni 3.3  mwaka 2019/2020. 

Hata hivyo, mwaka 2019/2020 wavuvi walivua kiasi cha tani 392,933, jambo linalodhihirisha kuwa bado kuna kazi kubwa katika uboreshaji wa sekta ya uvuvi nchini hasa matumizi ya teknolojia ya kisasa. 


Soma zaidi: 


Wananchi waonywa matumizi ya maji

TMA imesema katika msimu wa kipupwe, hali ya ukavu na upepo inaweza kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine. 

Hivyo, Jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa.

“Kwa ujumla vipindi vifupi vya upepo mkali wa Kusi na hali ya ukavu inatarajiwa katika maeneo mengi,” amesema Dk Kijazi. 

Mwelekeo wa hali ya hewa uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya hewa katika maeneo makubwa.

Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Enable Notifications OK No thanks