Mradi wa matenki ya mafuta TPA kupunguza uhaba, bei ya mafuta Tanzania

February 27, 2024 4:45 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mpaka kufikia mwaka 2026 jumla ya matenki 15 yenye ujazo wa metriki tani 420,000 yatajengwa.
  • Yatapunguza bei ya mafuta, mfumuko wa bei na muda mrefu wa kusubiri mafuta bandarini.

Dar es Salaam. Huenda watumaji na wauzaji wa mafuta ya vyombo vya moto pamoja na mafuta ya ndege nchini Tanzania wakapata ahueni siku za usoni mara baada ya Mamlaka ya Bandari (TPA) kutia saini mkataba wa ujenzi wa matenki makubwa ya mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

Ujenzi huo unafanywa na Wizara ya Uchukuzi chini ya TPA ambapo mpaka kufikia mwaka 2026 inatarajiwa jumla ya matenki 15 yenye ujazo wa metriki tani 420,000 kukamilika.

Mkurugenzi wa TPA,  Plasduce Mbossa aliyekuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa miundombinu hiyo leo  Februari 26, 2024 jijini Dar es Salaam amesema kupitia mradi huo bei ya mafuta itapungua nchini.

“Mamlaka inaamini utekelezaji wa mradi huu utapunguza bei ya mafuta yanayoingizwa nchini, utapunguza malalamiko miongoni mwa wafanyabiashara lakini pia utaimarisha upatikanaji wa mafuta nchini…,” amesema Mbosa.

Ujenzi huo wa matenki ya kuhifadhia mafuta unakuja wakati kukiwa na ahueni kiduchu katika bei ya mafuta ya vyombo vya moto pamoja na mafuta ya taa Tanzania.

Ahueni ya mafuta ilianzia mwezi Oktoba 2023 ambapo ilipungua kutoka Sh3,281 kwa lita moja iliyokuwa mwezi Septemba 2023 hadi kufikia Sh3,051 kwa lita ya petroli mwezi Februari 2024 kwa jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi:Waliofariki kwa ajali mkoani Arusha wafikia 25


Katika kipindi hicho hicho mafuta ya dizeli nayo yalipungua kutoka Sh3,448 kwa lita hadi Sh3,029 iliyopo hivi sasa huku mafuta ya taa yakipungua kutoka Sh2,943 hadi Sh2,840.

Mbali na kupungua kwa bei ya mafuta, mradi huo wa ujenzi wa matenki utasaidia kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi ambao hupaa sambamba na kupanda kwa bei ya mafuta.

“Mradi huu unaweza kupunguza mfumuko wa bei na kuleta nafuu kwa wananchi wa kawaida, hii inatokana na ukweli kwamba kupanda kwa bei ya mafuta kunasababisha kupanda kwa bei nyingine,” ameeleza Mbosa.

Aidha, matenki hayo yatapunguza muda wa upakuaji mafuta katika meli kutoka siku 11 hadi siku 3 huku uhifadhi wa mafuta nchini ukiongezeka  zaidi kutoka siku 15 ambapo mafuta yalikuwa yakihifadhiwa na kampuni binafsi.

Wawakilishi wa kampuni ya MGD waliopewa kandarasi ya kujenga matenki ya mafuta na wawakilishi wa TPA wakitia saini mkataba wa ujenzi.Picha|TPA

Wananchi changamkieni fursa

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi  Prof. Makame Mbarawa aliwaambia wahudhuriaji wa hafla hiyo kuwa kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa nyingi za biashara kwa wakazi wa Dar es Salaam hususan wanawake na vijana.

“Ni matumaini yangu kuwa vijana watakaopata fursa ya kuajiriwa wakati wa utekelezaji wa mradi huu watajenga ujuzi na utaalamu zaidi katika fani zao ambao watazitumia katika miradi mingine itakayotekelezwa hapo baadae,” amesema Prof. Mbarawa.

Sambamba na hilo, Mbarawa amezitaka TPA, Wizara ya Uchukuzi na Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kusimamia mradi na kuzuia vitendo vyote vya ubadhilifu vinavyoweza kufanyika wakati wa mradi huo ili kuwezesha ufanisi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW