Mkanda wa gari unavyookoa maisha kwa dereva na abiria

January 13, 2023 8:52 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Watajwa kuepusha vifo na majeraha makubwa kwa asilimia 50.
  • Ni kosa kisheria kuendesha gari bila kufunga mkanda.

Dar es Salaam. “Nafahamu rafiki zangu ambao waliokoa maisha yao kutokana na kujifunga mkanda wa gari, mimi sijawahi kupata ajali lakini huwa nafunga mkanda muda wote ninapoendesha,”  

Ni Michael Mkanila, dereva wa daladala za Buza-Makumbusho Jijini Dar es Salaam akielezea umuhimu wa kufunga mkanda wa gari hususani kwa dereva, jambo ambalo amekuwa akilifanya kwa muda wa miaka sita tangu alipoanza kazi ya udereva.

Kufunga mkanda wa gari, si kitu ambacho watu wote wanaoendesha wanaweza kufanya, baadhi yao hutoa sababu mbalimbali za kutokufunga kama joto,  kubanwa na wengine husema hakuna askari.

Umuhimu wa mkanda wa gari ulizifanya mamlaka za sheria nchini Tanzania  kutunga kanuni inayomtaka dereva na abiria wa kiti cha mbele kuhakikisha wamefunga mkanda huo kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 kifungu cha 39, kifungu kidogo cha 11.

“Hakuna mtu anayeruhusiwa kuendesha gari  isipokuwa mtu huyo na yeyote aliyeketi  kiti cha mbele katika gari hilo amejifunga mkanda wa usalama, “ inasomeka sheria hiyo.


Soma zaidi:


Kwa nini ufunge mkanda?

Inspekta Noah Mwakyoma kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ni muhimu kwa dereva kufunga mkanda kwani anatakiwa awe na kitu kilichomshika ili aongoze gari vyema.

“Barabara zetu zimetofautiana, kuna maeneo yana miinuko na mabonde pamoja na mashimo, ule mtikisiko unaweza kusababisha ukawa unayumba na usukani au kukanyaga mafuta bila uwiano na mwisho ukajikuta unapoteza muelekeo,” anasema Ispekta Mwakyoma.

Inspekta Mwakyoma amesisitiza kuwa athari za kutokufunga mkanda ni kubwa zaidi pale inapotokea ajali kwa gari kugonga au kupinduka kwani dereva pamoja na abiria wanaweza kutoka nje au kuanguka kutegemeana na kasi ya chombo kwa wakati husika.

Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani nchini Marekani inakadiria kuwa kufunga mkanda wa gari hupunguza uwezekano wa vifo kwa abiria waliokaa kiti cha mbele kwa asilimia 45 na kupunguza uwezekano wa kupata majeraha makubwa kwa asilimia 50.

Ni kosa kisheria

Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa kanuni inayomtaka dereva na abiria kufunga mkanda ni kosa kisheria endapo itabainika mtu amekiuka kanuni hiyo na hivyo ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“Mtu yoyote ambaye yupo siti ya mbele ya gari na hajafunga mkanda atahesabiwa amefanya kosa na atapigwa faini ambayo ni Sh30,000, “ anasema Inspekta Mwakyoma.

Wadau wa usalama barabarani wanashauri Serikali ifanye mabadiliko ya sheria ili iwe lazima kwa watu wote waliopo kwenye gari kufunga mkanda. 


Tangazo:


Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW