Miundombinu, madini vyachangia ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.1 mwaka 2023 Tanzania

June 13, 2024 7:35 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mwaka 2024 uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua  kwa kasi ya asilimia 5.4 kutoka kasi ya asilimia 5.1 iliyorekodiwa mwaka jana.
  • Ukuaji huo unatarajiwa kuchochewa na  maboresha ya mazingira ya biashara na uwekezaji.

Dar es Salaam. Uchumi wa Tanzania ulikua kwa kasi ya asilimia 5.1 mwaka 2023 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 ukichagizwa zaidi uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji. 

Kiwango hicho cha ukuaji wa uchumi ni kikubwa kuwahi kurekodiwa tangu Tanzania iathiriwe na athari za ugonjwa wa Uviko-19 ulioathiri mataifa mengi duniani. Kwa miaka zaidi ya 10 kabla ya Uviko-19 mwaka 2020, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakua kwa kasi ya asilimia 6 hadi 7.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo amewaeleza wabunge jijini Dodoma kuwa Pato halisi la taifa kwa mwaka 2023 lilifikia Sh148.3 trilioni kutoka Sh141.2 trilioni mwaka 2022 sawa na ukuaji wa silimia 5.1.

“Ukuaji huo ulichangiwa na jitihada mbalimbali za Serikali ikiwemo mikakati ya kukabiliana na vita kati ya Urusi na Ukraine pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji,” amesema Prof Mkumbo bungeni Dodoma leo, Juni 13, 2024. 

Waziri huo amesema ukuaji huo pia ulichagizwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe na kuongezeka kwa mikopo kwenye sekta binafsi iliyochochea shughuli za kiuchumi.

Uchumi wa Tanzania unategemea zaidi shughuli za kilimo, madini na utalii ambao umeendelea kuimarika ndani ya miaka mitatu ya hivi karibuni.


Soma zaidi:Kasi ya mfumuko wa bei yang’ang’ania kiwango cha Aprili 2024


Katika hotuba yake, Prof Kitila amesema katika mwaka 2024 wanatarajia uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi ya asilimia 5.4 kutoka kasi ya asilimia 5.1 iliyorekodiwa mwaka jana.  

Ukuaji wa uchumi wa mwaka 2024 unatarajiwa kuchochewa na maboresha ya mazingira ya biashara na uwekezaji, uwekezaji zaidi kwenye kilimo na kuchochea ujenzi wa viwanda vitakavyozalisha bidhaa zitakazopunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. 

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitekeleza hatua mbalimbali za kuboresha uchumi ikiwemo kuwekeza zaidi kwenye miradi ya nishati na usafirishaji na kuhamasisha ujenzi wa viwanda ili kupunguza utegemezi wa kuingiza bidhaa kutoka nje.

Mapema Machi mwaka huu Benki ya Dunia ilieleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa himilivu licha athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi zinazoendelea kuzikumba nchi nyingi duniani. 

Benki hiyo ilieleza katika ripoti yake ya 20 ya hali ya uchumi wa Tanzania (Tanzania Economic Update) kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.1 mwaka 2023 kutoka asilimia 4.6 wa mwaka 2022 kutokana na maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji ambao ulisaidia kupunguza athari za mafuriko na ukame. 

“Wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua, ukuaji wa hivi karibuni unaonyesha kuwa umejikita zaidi katika sekta ambazo zinaajiri watu wachache sana kutoka kwenye kaya na kupunguza jitihada za kuondoa umaskini,” ilisomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Enable Notifications OK No thanks