Mikakati kuongeza uzalishaji wa pamba 2021-22

August 26, 2021 11:16 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Itatumbulisha njia mpya ya upandaji mbegu yenye tija.
  • Iitamuwezesha mkulima kuzalisha pamba hadi kufikia kilo 2,000 kwa ekari moja.
  • Wakulima wataongeza uzalishaji na mapato.

Mwanza. Huenda wakulima wakaongeza uzalishaji wa pamba msimu ujao wa 2021/22, baada ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kuja na mikakati ya  kuboresha kilimo cha zao hilo ikiwemo kutoa mbegu bora.

 Akizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz), Mkurugenzi wa Huduma na Usimamizi wa zao hilo kutoka TCB,  James  Shimbe amesema  wamekuja na mikakati hiyo baada ya kuona tija ya zao hilo nchini imekuwa ndogo tofauti na mataifa mengine yanayozalisha pamba.

Mikakati hiyo ni pamoja na kutambulisha namna ya upandaji wa mbegu kwa sentimita 60 kwa mstari na sentimita 30 kwa shimo. 

Vipimo hivyo vipya vya upandaji pamba vitamuwezesha mkulima kuzalisha pamba hadi kilo 2,000 kwa ekari moja.

“Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na taasisi za utafiti TARI Ukiliguru na ile ya  Ilongo Morogoro zimekuwa zikifanya kazi kwa juhudi kubwa kuendesha utafiti wa vipimo sahihi vya kupanda pamba ambavyo vitawezesha mkulima kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo,” amesema Shimbe.

Kwa mujibu wa Shimbe vipimo hivyo vitaanza kutumika katika msimu wa kilimo unaokuja wa 2021/22 na hivyo kuchangia ongezeko la uzalishaji wa pamba nchini.

Mabadiliko hayo ya vipimo yatamuongezea mkulima idadi ya miche kutoka 22,222 ya awali alipokuwa anatumia vipimo vya sentimeta 90 kwa sentimeta 40 hadi kufikia miche 444,400 kwa kutumia vipimo vipya kwa ekari moja.

“Ongezeko hilo la idadi ya mimea kwa ekari, mkulima atarajie kuongeza uzalishaji mara mbili ya uzalishaji wa awali ambapo ekari moja ya pamba itamwezesha kupata kilo 2,000 kutoka kilo 1,000 kwa ekari, ” amesema. 

Amesema  mkulima atakayepanda pamba kwa kuzingatia vipimo hivyo  atanufaika  kipato mara mbili ya kipato alichokuwa akipata wakati wa upandaji wa awali.

“Hivyo tutaweza kuona mkulima huyu ananufaika kwa upande wa kipato na kukuza kiwango chake cha uchumi iwapo atazingatia kikamilifu kanuni,” amesema. 

Kwa mikakati hiyo, TCB imelenga kukuza uzalishaji kutoka wastani wa tani 300,000 hadi kufikia tani milioni 1 ifikapo 2025.

Pamba: Dhahabu nyeupe. Picha| TCB.

Tangu uzalishaji wa pamba uanze hapa nchini mwanzoni mwa karne 20, uzalishaji wa juu kabisa ulifikiwa msimu wa 2005/2006 ambapo jumla ya tani 376,000 sawa na marobota 700,000 ilizalishwa.

Kiwango hicho cha uzalishaji kwa mujibu wa Shimbe hakijafikiwa au kuvukwa kwa muongo mmoja na nusu uliopita. 

Uzalishaji wa zao hilo umekuwa wa kupanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kutozingatia kanuni za kilimo bora cha pamba. 

Mataifa mengi duniani ikiwemo Misri wanazalisha kilo 2,000 kwa ekari wakati Tanzania inazalisha kilo 300 kwa ekari.

Huenda mikakati iliyoanzishwa na TCB ikawahamasisha wakulima kujitokeza kwa wingi msimu ujao kulima pamba ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakipata tija kidogo.

Wakulima wameiomba Serikali iwasaidie hasa kuwapatia mbegu bora, pembejeo na fedha ili kuongeza uzalishaji na kupata kipato kwa ajili ya kuendesha familia.

Masanja Manota ni mkulima wa zao la pamba Kijiji cha Usagara mkoani Mwanza anasema changamoto inayomkabili ni ukosefu wa mbegu na viuatilifu vinavyouzwa kwa wakulima kwa gharama ya juu. 

Anasema ni vyema TCB ikawakopesha wakulima viuatilifu hivyo na mbegu kupitia vyama vya ushirika ili ziwasaidie. 

“Ni kweli wakulima wengi hawajishughulishi na zao hilo kama miaka ya nyuma kutokana na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mbegu bora,  viuatilifu na wakati mwingine kuzidi kwa mvua, ” amesema Masanja.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW