Migogoro ya binadamu na tembo inavyotokomezwa kwa pilipili, oili chafu-2
- Pilipili na oili chafu hupakwa kwenye vitambaa na kuwekwa kwenye fensi ya shamba.
- Pia vilipuzi na mavuvuzela yenye milio hutumika kuwadhibiti tembo wasiingie wenye mashamba ya wakulima.
- Serikali yasema itaendelea kushirikiana na vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kuondoa migogoro ya binadamu na wanyama.
Rufiji. Kutokomeza migogoro baina ya binadamu na tembo linaweza kuonekana ni jambo dogo tu kwa baadhi ya watu wasiofahamu masuala ya wanyamapori.
Lakini kiuhalisia ni bonge la shughuli kiasi cha kufanya wataalamu wa wanyamapori kubuni mbinu mpya kila siku kuhakikisha kuwa binadamu na tembo hao hawadhuriki katika jitihada za kutatua migogoro hiyo.
Idara ya Wanyamapori ya Rufiji kwa kushirikiana na Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Duniani (WWF Tanzania) na taasisi ya Parks Foundation wamebuni njia nne za kupunguza migogoro ya tembo na binadamu.
Pilipili, oili zinavyotumika kufukuza tembo
Mhifadhi wanyamapori katika Halmashauri ya Rufiji, Mwarami Mpunde anasema kwa sasa wanatumia uzio wa pilipili (Chilli fence) kwa kuchukua pilipili na oili chafu ya vyombo vya moto inayopakwa kwenye vitambaa halafu inazungushwa eneo la shamba.
“Tembo akija katika hilo eneo, akisikia tu harufu ya pilipili inamchoma machoni, kwa hiyo inakuwa shida kwake unarudi alikotoka,” anasema Mhifadhi huyo na kuwa mbinu hiyo imewasaidia wakazi wa kijiji cha Ngarambe ambao mwaka wa 2019/2020 wamevuna zaidi tani 20 za mahindi, mafanikio ambayo ilikuwa ni vigumu kuyapata kipindi cha nyuma.
Askari wanyamapori wakishirikiana na wataalam kutoka WWF Tanzania kufunga vitambaa vyenye oili na pilipili kwenye uzio wa waya ili kuzuia tembo kuingia kwenye mashamba ya wakulima katika kijiji cha Ngarambe wilayani Rufiji. Picha|WWF Tanzania.
Vuvuzela inamkimbiza tembo
Vilevile wanatumia vilipuzi (sunder flash) na mavuvuzela yenye sauti ambapo tembo wakiingia shambani wanapigiwa na wanakimbia kurudi hifadhini, licha ya kuwa baadhi ya tembo hawaogopi kwa sababu hiyo milio wameanza kuizoea.
“Lakini tunatumia tochi ambazo zina mwanga mkali ambazo zililetwa na WWF Tanzania. Hizo tochi na pilipili tayari zinatumika sana Ngarambe,” anasema Mpunde.
Wakati Ngarambe wakifaidika na mbinu hizo, wenzao wa vijiji vya Mloka na Ngorongu ambako madhara ya tembo yako juu bado hawana la kufanya zaidi ya kusubiri WWF Tanzania na halmashauri kupata fedha ili kuwapelekea vifaa hivyo vitakavyosaidia kudhibiti tembo kijijini kwao.
Vilipuzi na mavuvuzela yanayotumika kuwafukuza tembo wasiingie kwenye mashamba na makazi ya watu wilayani Rufiji. Picha|WWF Tanzania.
Kibarua bado kigumu
Ni dhahiri kuwa mbinu hizo zimeleta tija lakini tembo nao hubuni njia mpya ili kukwepa maeneo ambayo yamewekwa uzio wa pilipili na kufika kule wanakotaka kwenda.
“Tumefanikiwa kuzuia sehemu moja ya kupata mazao ya wakulima, hilo limeleta tija lakini siyo kumzuia tembo kuja maeneo ya mashamba, hilo limeshindikana,” anasema Mhifadhi huyo wa daraja la tatu.
Mabadiliko ya tabia za tembo dhidi ya mbinu za kuwadhibiti na changamoto za vitendea kazi yakiwemo magari na vifaa kuwawezesha watendaji ni mambo yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kukabiliana na wanyama hao.
Mtaalam wa Usimamizi wanyamapori kutoka WWF Tanzania, Richard Katondo anasema mbinu za kufukuza tembo zinazotumika Rufiji ziko kwenye majaribio ili kutafuta suluhisho la kudumu la uharibifu unaofanywa na wanyama hao.
Hadi sasa wamewawezesha wakulima 30 katika kijiji cha Ngarambe kutumia mbinu hizo kukabiliana na madhara ya tembo.
Kuhusu kupanua huduma hiyo hadi katika vijiji vingine ikiwemo Mloka, anasema inategemeana na upatikanaji wa fedha za kununulia vifaa kwa sababu kwa sasa vifaa vya kuwadhibiti tembo vinatolewa na WWF Tanzania.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania – 1
Hata hivyo, WWF tayari imepeleka tochi Mloka ikiwa ni hatua ya awali kutumia mbinu zingine kudhibiti tembo hao waharibifu.
“Kwa sasa tunajaribu mbinu nyingine ya mizinga ya nyuki ambayo wakulima wataweka kwenye mashamba yao ili tembo wakisikia sauti za wadudu hao wakimbie,” anasema Katondo na kubainisha kuwa mizinga hiyo itatumika pia kuwaingizia kupato wakulima.
Pia WWF Tanzania inashirikiana kwa karibu na Serikali kutoa vifaa, mafunzo, kuwajengea uwezo askari wanyamapori na wananchi hasa wanaoishi karibu na hifadhi ya Nyerere ili kukabiliana na wanyamapori wakiwemo tembo.
Mikakati ya Serikali
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dk Stephen Nindi ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa Serikali iko katika mchakato wa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi kwa jamii zote zinazozunguka hifadhi za Taifa ili kuondoa migogoro ya wanyamapori na binadamu ikiwemo uvamizi unaofanywa na tembo kwenye mashamba ya wakulima.
“Mpango huu utazingatia mambo mengi ikiwemo ikolojia ya wanyama na rasilimali za vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kuhakikisha ardhi inatumiwa vizuri kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika,” anasema Dk Nindi.
Mpango huo utaenda sambamba na kuundwa kwa mfumo maalum utaokakikisha wanavijiji wanaoishi karibu na hifadhi wanashirikishwa kikamilifu katika uhifadhi wa wanyamapori, ardhi.
Mtaalam huyo wa masuala ya ardhi anasema jambo lingine la kupunguza migogoro ya tembo na binadamu ni kuziboresha sheria zinazosimamia uhifadhi wa wanyamapori zikiwemo za mapitio ya wanyama (shoroba) kwa sababu baadhi ya shoroba zina makazi na shughuli za kiuchumi, jambo linaloibua utata kwa wananchi.
“Tunashauri vijiji viache yale maeneo wanayopita wanyama ili wapite katika shoroba zao kwa sababu zisipofunguliwa wanyama hao watasababisha madhara makubwa zaidi,” anasema Dk Nindi.
Pilipili inayotumika kufukuza tembo wasiingie kwenye mashamba ya wakulima wilayani Rufiji. Picha|WWF Tanzania.
Utaratibu mzuri na elimu kwa wananchi kufahamu umuhimu wa mapitio ya wanyama utasaidia wananchi kupunguza madhara na wao kuendelea kunufaika na ardhi.
Kwa sasa, shoroba zinasimamiwa na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009, ambapo changamoto za shoroba hutufautiana kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hivyo suluhu zinazobuniwa zinatakiwa kuzingatia ukubwa wa mapitio na mahitaji ya vijiji husika.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiambia Nukta kuwa tembo wanawasumbua wananchi kwa sababu wamejenga au wamelima kwenye mtawanyiko au maeneo ambayo zamani yalikuwa makazi ya tembo (shoroba) hivyo wanyama hao hupita katika maeneo yale ili kufuata malisho na vyanzo vya maji.
Anasema katika maeneo hayo, wanatumia askari wanyamapori kuwadhibiti tembo na wanatoa elimu ili wananchi wafahamu mtindo wa maisha ya wanyama hao na jinsi gani wanapaswa kuepuka shoroba ili wasiendelee kupata madhara.
Latest