Mfumo wa ‘mali kauli’ unavyowaumiza wanawake sokoni Tanzania
- Ni mabadilishano ya bidhaa na mazao bila maandishi.
- Husababisha wafanyabiashara kupata hasara na kuzua migogoro.
- Wadau waanzisha mfumo wa mikataba maalum.
Dar es Salaam. Ni saa nane za usiku wakati wengine wamelala, mama huyu yuko katika soko la Ilala mkoani Dar es Salaam ili kununua bidhaa kutoka kwa wakulima.
Leah Shigela, ambaye ameacha kitanda na kuwahi sokoni hapo ili kujipatia mzigo wa karoti na pilipili hoho kwa ajili ya kuziuza asubuhi sokoni.
“Nipe huo hapo, si upo vizuri lakini?,” anauliza Leah na “ndiyo!” anajibiwa na mfanyabiashara mwenye shehena kubwa ya mazao hayo ya shamba yanayotumika kwenye maandalizi ya mboga.
Huku akitabasamu, Leah anachukua bidhaa na kwenda kuweka kwenye kibanda chake sokoni hapo kwa shauku ya kutengeneza faida atakapouza kwa wateja wake.
Mategemeo yanakuwa sivyo kwani panapokucha, Leah anaanza asubuhi yake na machozi baada ya nusu ya mzigo wake wa karoti kukukuta umeharibika na hana sehemu ya kuupeleka zaidi ya kuutazama ukienda jalalani.
“Hela ya kumrudishia mkulima nitaitoa wapi?” anajiuliza, “Hawezi kunielewa nikimwambia mzigo ulikua umeharibika.”
Mfumo wa mali kauli ni maarufu masokoni hasa miongoni mwa wafanyabiashara wanaouza mali zinazouza. Picha| Gift Mijoe.
Hii ndiyo kiini cha tatizo
Hasara aliyopata mama huyu ni changamoto inayowakumba wafanyabiashara wengi wanaouza bidhaa zinazoharibika haraka kukosa mfumo wa makabidhiano unaowahakikishia usalama wa bidhaa wanaponunua kwa wakulima.
Utaratibu huo unafanya kazi katika masoko mbalimbali mkoani hapa yakiwemo ya Ilala, Buguruni na Kigogo Sambusa ambapo wafanyabiashara hupokea mizigo kutoka kwa wakulima kwa ‘makubaliano ya kauli’ bila kuandikishana popote.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa taasisi ya inayotoa msaada wa kisheria kwa wanawake sokoni (Calesoju), Consolata Kiza anasema baadhi ya wafanyabiashara hukopa bidhaa kutoka kwa madalali na wakulima kwa makubaliano ya kuwapatia pesa zao baada ya mauzo.
Hayo yote yanafanyika kwa mazungumzo ya mdomo na kujuana.
Kwa baadhi hujikuta kwenye sintofahamu pale bidhaa walizochukua kwa wakulima au madalali zinapokuwa zimeharibika na kutakiwa kulipa fedha.
Suala hilo huwaumiza vichwa wafanyabiashara kwa sababu wakati mwingine bidhaa zinakuwa zimeharibika na kutokujua wafanye nini.
“Ikifika jioni, mfanyabiashara anadaiwa, pesa yenyewe hana na wengine wanalazimika kutumia pesa zao binafsi kulipa madeni yao. Anabaki na hasara,” anasema Kiza ambaye pia huuza nyanya katika soko la Ilala.
Suala hilo huzusha ugomvi na udhalilishaji hasa kwa wanawake pale wanaposhindwa kulipa fedha za wakulima.
Pia huaribu mahusiano ya kibiashara na wasambazaji wa bidhaa ambao ni wakulima na madalali.

Mwanzo wa enzi mpya
Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni uelewa kwa wafanyabiashara umeanza kuongezeka baada ya Calesoju ambayo awali ilikuwa chini ya shirika linalotetea wanawake la Equality for Growth (EFG) kuwaelimisha wanawake kutumia mikataba katika biashara zao na kuachana na mali kauli.
Kupitia Calesoju, wajasiriamali 6,618 wameelimishwa juu ya matumizi ya mikataba sokoni huku asilimia 47 au takriban nusu ya wajasiriamali hao wakiwa ni wanawake kutoka masoko ya Ilala, Buguruni na Kigogo Sambusa.
Elimu hiyo pia imewezesha kuandaliwa kwa mkataba ambao wafanyabiashara wanasainishana na wakulima ili kuhakikisha bidhaa iliyotolewa imekidhi vigezo vya ubora unaohitajika sokoni.
Mkataba huo ni karatasi moja tu ambayo inasainiwa ili kuhakikisha haki kati ya mjasiriamali na dalali au mkulima zinazingatiwa. Kwenye karatasi hiyo kuna taarifa za mzigo uliochukuliwa, marejesho na wahusika waliopo na husainiwa kati ya mkulima au wakala, mjasiriamali na shahidi.
Licha ya wanawake wengi kufikiwa na elimu hiyo ikilinganishwa na wanaume, bado muitikio wao hauridhishi, jambo linalowafanya waendelee kupata hasara na kunyanyasika.
Kwa nini muitikio ni mdogo?
Kwa mujibu wa mjasiriamali wa ndizi kutoka soko la Ilala, Mariam Rashid, mikataba inakuwa na ugumu kutekelezwa kwa wajasiriamali wa bidhaa zinazoharibika mapema.
“Mali kuoza hazina bei maalumu. Ukipokea mzigo wa Sh3 milioni, ukaingia mkataba na mkulima, kisha ukaja sokoni ukapata Sh1.5 milioni jela inakuhusu, wauzaji wa mali kuoza wengi wanaogopa,” anasema Saidi.
Hilo linawaacha wengi kubaki na matumizi ya “mali kauli” ambapo hukopa mzigo na kuuza kisha utalipa ukimaliza kuuza.
Saidi anasema mikataba inafanya kazi vizuri kwa ambao bidhaa zao haziharibiki ikiwemo wauza mitumba, batiki na vitenge.
Ugumu mwingine unaotokea katika kutumia mikataba hiyo ni kuwa shughuli za kubadilishana bidhaa hufanyika kwa haraka na hakuna mfumo unaowapa fursa wafanyabiashara na wakulima kujadiliana kwa upana.
“Haiwezekani mkulima aanze kukusaini mkataba wewe wakati ana wafanyabiashara wengine wanamsubiri awahudumie. Wapo wachache wanaotumia lakini siyo mara zote,” anasema Mwenyekiti wa Soko la Buguruni, Said Habibu.
Mariam Rashid kutoka soko la Ilala amesema mikataba inafanya kazi zaidi kwa watu wanaouza mali zisizooza. Picha| Gift Mijoe.Serikali, wadau waingilia kati
Licha ya kuwepo kwa changamoto za kutumia mikataba hiyo, Afisa Mradi wa Equality for Growth (EFG), Susan Sitta anasema wataendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuweka mfumo utakaorahisisha mikataba kupewa kipaumbele sokoni ili kuwalinda wanawake.
Katika kipindi hiki ambacho mikataba hiyo haijapata muitikio mkubwa, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha wafanyabiashara na wakulima wanauziana bidha kwa maelewano ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Karume anayesimamia soko la Ilala, Geraldina Bakalile anasema ofisi yake imekuwa ikipokea kesi nyingi hasa za wafanyabiashara kushindwa kuwalipa wakulima fedha zao lakini wamekuwa wakitumia njia ya mazungumzo kumaliza kesi hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu anasema Serikali inaendelea na utekelezaji wa maboresho ya maeneo ya kazi hasa kwenye masoko kuhakikisha migogoro iliyopo inatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Serikali imeweka mipango ya uendelezaji wa masoko. Baadhi ya masoko yamejengwa kipindi kulikuwa na idadi ndogo ya watu. Halmashauri imelenga kuyajenga kwa ukubwa kuendana na wingi wa wafanyabiashara,” amesema Shaibu.
Maboresho hayo, Shaibu anasema, ni pamoja na ujenzi na upanuzi wa masoko ambayo yameelemewa kwa wingi wa wajasiriamali, jambo ambalo linasababisha migogoro ikiwemo kukosa sehemu za kufanyia kazi na kusababisha migogoro.
Latest
