Mbinu zitakazowasaidia wanawake kuinua biashara zao sokoni

January 3, 2022 4:24 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wapatiwe elimu ya biashara na mitaji.
  • Wajengewe miundombinu rafiki ya kufanya biashara.
  • Kujiunga kwenye vikundi kunaweza kuwasaidia.

Dar es Salaam. Zubeda Saidi, mfanyabiashara wa vifaa vya urembo katika soko la Kinyerezi jijini Dar es Salaam ana ndoto ya kuikuza biashara yake ikiwemo kumiliki maduka kadhaa na kutoa ajira kwa wanawake wenzake.

Huenda ikachukua muda mrefu kwa ndoto ya Zubeda kutimia kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili katika biashara yake. 

Moja ya changamoto hizo ni ukosefu wa wateja wa uhakika na wa kudumu kununua bidhaa katika banda lake lilipo katika soko hilo lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

“Wateja huwa tunapata jumatatu siku ambapo kunakuwa na gulio. Baada ya hapo, kuwaona wateja ni hadi alhamisi ambao vitu vinakuwa vimewaishia ndani,” anasema binti huyo anayepata wateja kwa nadra. 

Zubeda ni miongoni mwa wanawake wengi ambao wameonyesha juhudi ya kujikwamua kiuchumi kupitia biashara ndogo ndogo katika masoko ya jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wanahitaji maarifa, ujuzi na usaidizi wa kisheria na kifedha ili kuzikuza biashara zao na kupata faida itakayosaidia kuboresha maisha yao na familia. 

Miongoni mwa mbinu zitakazowasaidia wanawake wafanyabiashara hao ni elimu ya kuendesha biashara masokoni ikiwemo utunzaji wa fedha, namna ya kupata wateja, huduma kwa mteja na bidhaa bora zinazoweza kufanya wateja watoke mtaa mwingine kuja kwenye maduka yao.

Mfanyabiashara wa soko la Kinyerezi, Stella Mwandri anasema wafanyabiashara ndani ya masoko bado wanahitaji elimu ya matumizi ya fedha na elimu ya mikopo na jinsi ya kuipata mikopo hiyo.

“Tumefundishwa mengi lakini bado tumefanya tuliyofundishwa hayajatusaidia kupata mikopo. Waje watufundishe hadi wahakikishe tumepata mikopo,” anasema Mwandri, aliyepata mafunzo ya uendeshaji wa biashara kutoka shirika linalotetea wanawake la Equality for Growth (EFG).

Baadhi ya mabanda yaliyofungwa kwa kukosa wateja kwenye soko la Kinyerezi. Picha| Gift Mijoe.

Kupata mikopo na mitaji 

Ili wanawake wanaofanya biashara masokoni waendelee wanatakiwa kupatiwa mitaji na mikopo yenye masharti nafuu. Kwa kutambua hilo. Serikali na sekta binafsi zimekuwa zikitoa mikopo kwa fanyabiashara.

Licha ya kutolewa kwa mikopo hiyo, wanawake bado wanapata changamoto ya kuipata mikopo hiyo kwa sababu ya kukosa elimu ya kuandaa andiko la biashara na jinsi ya kuitumia.

Mwenyekiti wa kitengo cha mikopo kutoka Benki ya DCB tawi la Kinyerezi, Fatuma Sudi anasema wanawake wanachangamkia mikopo lakini ni wachache wao wanaokuwa na ufahamu wa kuandika mawazo bora ya biashara yanayoweza kufanya maombi yao yapewe vipaumbele.

“Mikopo kweli wanaomba lakini wengi wakipata wanaishia kulipa madeni na siyo kujiendeleza. Wanabaki wanadaiwa halmashauri na mwishowe biashara zao zinakufa kwa kuelemewa au kukosa mitaji,” anasema Sudi.

Anasema elimu itolewe zaidi kwa wanawake waliopo sokoni ili kuwawezesha kufaidika na mikopo wanayopata.

Kuunda vikundi vya kusaidiana

Kwa mwanamke yeyote, bila shaka atakubali jinsi vikundi vya kusaidiana  (Vicoba) vilivyopata umaarufu miongoni mwa watu hivi karibuni. Vikundi hivyo vya kusaidiana kwa njia ya kuchangiana fedha vimewawezesha baadhi kufungua hadi kampuni zao.

Kufahamu umuhimu wa vikundi hivyo, baadhi ya wadau likiwemo shirika linalotetea wanawake la Equality for Growth (EFG) wamekuwa wakitoa elimu kwa wanawake ya kuunda vikundi kwenye ngazi ya masoko ambayo siyo tu imewasaidia kiuchumi na bali kuzijua haki zao na kuzipambania.

Mwakilishi wa EFG kwenye soko la Kigogo Fresh, Tatu Lazaro anasema EFG imewafundisha wanawake kuunda vikundi ambavyo vimewasaidia kushikana mkono ikiwemo kutetea haki za wenzao.

“Mwenzetu akipatwa na changamoto, wanawake tunashikilia kibanda chake hadi atakaporudi zamani ilikuwa ukipatwa na shida usipoonekana siku mbili, tatu unakuta sehemu yako kapewa mwingine,” anasema Lazaro.

Wanawake wakipata elimu na fursa za mikopo wanaweza kuinua biashara zao na kuboresha maisha Picha| Gift Mijoe.

Mikataba ya biashara

Kati ya changamoto zinazochangia unyanyasaji wa kijinsia sokoni ni pamoja na makabidhiano ya bidhaa kwa kauli tu bila mikataba, jambo ambalo limekuwa likiwaweza wanawake katika wakati mgumu. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa taasisi ya inayotoa msaada wa kisheria kwa  wanawake sokoni (Calesoju), Consolata Kiza anasema baadhi ya wafanyabiashara hukopa bidhaa kutoka kwa madalali na wakulima kwa makubaliano ya kuwapatia pesa zao baada ya mauzo. 

Hayo yote yanafanyika kwa mazungumzo ya mdomo na kujuana.

Kwa baadhi hujikuta kwenye sintofahamu pale bidhaa walizochukua kwa wakulima au madalali zinapokuwa zimeharibika na kutakiwa kulipa fedha.

Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni uelewa kwa wanawake wafanyabiashara umeanza kuongezeka baada ya Calesoju ambayo awali ilikuwa chini ya EFG kuwaelimisha wanawake kutumia mikataba katika biashara zao na kuachana na mali kauli.

Mikataba ambayo wafanyabiashara wanasainishana na wakulima inatoa uhakika kwa  bidhaa iliyotolewa kama imekidhi vigezo vya ubora unaohitajika sokoni.

Miundombinu rafiki kwenye masoko

Wanawake wanahitaji mazingira rafiki ya kufanyia biashara waki wa sokoni ikiwemo kuwepo kwa huduma muhimu kama vyoo, mitaro ya kupitisha maji na barabara ili kuvutia wateja.

Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu anasema Serikali inaendelea na utekelezaji wa maboresho ya maeneo ya kazi hasa kwenye masoko kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mazingira mazuri na migogoro iliyopo inatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Serikali imeweka mipango ya uendelezaji wa masoko. Baadhi ya masoko yamejengwa kipindi kulikuwa na idadi ndogo ya watu. Halmashauri imelenga kuyajenga kwa ukubwa kuendana na wingi wa wafanyabiashara,” anasema Shaibu.

Maboresho hayo, Shaibu anasema,  ni pamoja na ujenzi na upanuzi wa masoko ambayo yameelemewa kwa wingi wa wajasiriamali na kuhakikisha inakuwa na miundombinu muhimu ikiwemo vyoo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW