“Mfalme Zumaridi” aendelea kusota rumande, wenzake wakiachiwa
- Waliachiwa kwa dhamana mpaka sasa ni 85.
- Mfalme Zumaridi kuendelea kukaa mahabusu.
- Wanabiliwa na kesi tatu ikiwemo kusafirisha binadamu.
Mwanza. Kesi inayomkabili Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi na wenzake 93 wamepandishwa tena kizimbani na kusomewa mashtaka yao huku washtakiwa nane wakiachiwa kwa dhamana.
Kwa idadi hiyo, waliachiwa kwa dhamana wamefika 85 kati ya 93 waliakamatwa awali huku washtakiwa wengine nane ambao dhamana zao ziko wazi wameendelea kubaki rumande.
Tofauti na siku za nyuma, leo Mfalme Zumaridi ametinga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kama mwali anayepokelewa ukweni akiwa amejitanda ushungi kuficha sura yake.
Mwendesha mashtaka wa Serikali wakili Emmanuel Luvinga ameitaja kesi namba 10, 11 na 12 ambapo kesi namba 10 ni usafirishaji haramu wa binadamu inayomkabili Zumaridi pekee, kesi namba 11 ni shambulio la kudhuru mwili na kuzuia maafisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao inayowakabilia Zumaridi na wenzake nane huku kesi namba 12 ni kusanyiko lisilokuwa halali inayowakabili wafuasi wae 84.
Katika siku hii pia kesi namba 10 ilikuja kwa ajili ya kutajwa kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kuisikiliza huku kesi namba 11 na 12 zikiletwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Soma zaidi:
Kutokana na Hakimu aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo kutokuwepo, Wakili Luvinga ameiomba mahakama hiyo kupanga tarahe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa ombi ambalo Hakimu Mkazi, Stella Kiama, aliliridhia na kupanga April 14 kwa ajili ya kesi namba 10 kutajwa na 11 na 12 kuanza kusikilizwa.
Wakati shauri hilo likiendelea wakili wa utetezi, Erick Mutta alimuomba hakimu kutoa karipio kwa waandishi wa habari kuacha tabia ya kumrekodi mteja wake akiwa kizimbani kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Ombi hilo ni baada ya kuona picha zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimwonyesha mteja wake akiwa kizimbani.
Nje ya mahakama pia, wakili Mutta aliwaeleza waandishi wa habari kuhusiana na afya ya mteja wake Diana Bundala kutokuwa nzuri kuwa anasumbuliwa na mguu mmoja na hiyo ni baada ya purukushani zilizotokea wakati wa ukamataji.
Latest