Dk Faustine Ndugulile kuzikwa Kigamboni Disemba 3, 2024

November 28, 2024 3:35 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Mwili wake kwasili kesho Novemba 29, katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.
  • Rais Samia kuongoza zoezi la kutoa heshima za mwisho 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Dk Faustine Ndugulile anatarajiwa kuzikwa Disemba 3, 2024 Kigamboni jijini Dar es Salaam kufuatia kifo chake kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 akiwa anapata matibabu India.

Kwa mujibu wa Ratiba ya mazishi iliyotolewa na ofisi ya Bunge la Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan atawaongoza viongozi na wageni mbalimbali kutoa heshima za mwisho katika viwanja vya Karimjee Jumatatu Desemba 2, 2024, ambayo ni siku moja kabla ya mazishi.

Ratiba hiyo imeongeza kuwa mwili wa Dk Ndugulile utawasili kesho Novemba 29,  katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam ambapo utapokelewa na naibu spika, katibu wa bunge, wawakilishi wa chama pamoja na wawakilishi wa Serikali na kwenda kuhifadhiwa katika hospitali ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Lugalo.

Disemba 02 mwili wa marehemu utapelekwa Kanisa la St. Immaculate – Upanga kwa ajili ya Misa Takatifu na baadaye kupelekwa katika viwanja vya Karimjee ambapo viongozi mbalimbali watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho wakiongozwa na Rais Samia na kisha utapelekwa nyumbani kwake Kigamboni.

Jumanne Desemba 3, mwili wa marehemu Dk Ndugulile utapelekwa katika viwanja vya Machava kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho na kisha utapelekwa katika Kanisa la Bikira Maria Consolata kwa ajili ya Misa ya Mazishi na baadaye mwili wake utapumzishwa katika makaburi ya Mwongozo Kigamboni.

Enzi za uhai wake Dk Ndugulile alipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika anga za kimataifa baada ya Agosti 27 mwaka huu kutangazwa mshindi katika zoezi la upigaji kura lililofanywa na nchi 19 kutafuta Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika.

Matokeo ya ushindi wake yalitangazwa usiku wa Agosti 27 mwaka huu katika mkutano wa afya uliofanyika Congo Brazzaville.

Baada ya ushindi huo Dk Ndugulile alipewa miezi sita ya kuandaa mpango kazi kabla ya kuanza majukumu yake mapya mwezi Machi mwaka 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks