Jenerali Musuguri azikwa Butiama, Watanzania kumuenzi kwa kutunza amani

November 4, 2024 5:32 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuendelea kukumbukwa kama nguzo muhimu ya amani, mwalimu wa wengi na kiongozi mashuhuri nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko amewaongoza wanafamilia, viongozi wa Serikali, Maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na waombolezaji kuupumzisha mwili wa Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Musuguri katika kijiji cha Butiama mkoani Mara.

Jenerali Musuguri alifariki dunia Oktoba 29, 2024 akiwa na umri wa miaka 104 katika Hospitali ya Kanda Bugando jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu.

Biteko aliyekuwa akimwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliye ziarani nchini Marekani, amesema Jenerali Musuguri ameacha alama isiyofutika katika historia ya JWTZ, kwa kuacha urithi mkubwa wa ujasiri, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao utadumu milele katika kumbukumbu za Taifa.

“Katika maisha yake yote alijitolea kwa dhati kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa na amani, salama na yenye mshikamano, Jenerali Msuguri alikabiliana na changamoto nyingi kwa ujasiri mkubwa akionesha mfano uliotukuka na akitufundisha umuhimu wa mshikamano na moyo wa dhati wa kulinda nchi yetu,” amesema Biteko.

Biteko ameongeza kuwa Jenerali Musuguri aliyetumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 44 ataendelea kukumbukwa kama nguzo muhimu ya amani, mwalimu wa wengi na kiongozi mashuhuri nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali John Mkunda amesema Musuguri alitoa mchango mkubwa katika kuijenga JWTZ kwa kutumia uzoefu alioupata kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia akiwa miongoni mwa maafisa waanzilishi wa jeshi hilo lililoanzishwa Septemba mosi 1964 mara baada ya maasi.

“Sifa zote ambazo Jeshi letu limejizolea ndani na nje ya nchi tangu kuasisiwa kwake 1964 hadi sasa ni matokeo ya mchango mkubwa ya mzee wetu Jenerali David Musuguri, kama hakua peke yake lakini ni miongoni mwa majenerali walioliletea sifa kubwa jeshi letu, kamwe hatutosahau mchango wake mkubwa,” ameongeza Mkunda.

Aidha, Kiongozi Mkuu wa kabila la Wazanaki Chifu Wanzagi amesema Jenerali Musuguri alikuwa mtu aliyejali sana watu na kuwa karibu nao licha ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao huku akiwasaidia bila ya kujali tofauti za kijamii na kiuchumi.

“Aliyajua maeneo yote ya vijiji vyetu vya Zanaki, kuikumbuka na kuitambua mipaka yake vizuri sana na kwa uhakika, kwa jinsi hiyo ameyasaidia sana haya maeneo yetu kuondokana na migogoro kuhusu mipaka yetu na katika kumuenzi hili, naomba mipaka hiyo iendelee kuheshimiwa,” amesema Chifu Wanzagi. 

Jenerali Musuguri atakumbukwa zaidi kwa kuongoza majeshi ya Tanzania katika vita dhidi ya Idi Amin Dada wa Uganda Mwaka 1978, baada ya uvamizi wa eneo la Kyaka, Mkoani Kagera ambapo vita nyingine alizowahi kushiriki kwa mujibu wa JWTZ ni pamoja na ‘Battle of Madagascar’ (Mapambano ya Madagascar) na ‘Battle of Simba Hills’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks