Mchuano mkali iPhone, Samsung mauzo ya simu 2024

December 3, 2024 9:00 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Samsung yaongoza kwa mauzo ikifuatiwa kwa karibu na simu za iPhone.
  • Xiaomi na Oppo nazo zachangamsha soko.

Dar es Salaam. Kama umekuwa ukijiuliza ni nani atafunga mwaka 2024 kibabe kwa mauzo ya simu duniani, fahamu kuwa kampuni za Apple na Samsung ndio vinara. 

Apple inayotengeneza simu za iPhone inachuana vikali na Samsung katika mauzo ya simu huku mshindi akiwa bado hajapatikana. 

Hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2024 inayoishia Septemba, Samsung ilkuwa inaongoza kwa mauzo ya simu duniani.  

Ripoti ya utafiti kuhusu mauzo ya kampuni za simu duniani uliofanywa na kampuni ya utafiti na masoko ya Counterpoint, katika kipindi cha miezi tisa iliyopita inaonyesha kuwa Samsung imeuza simu milioni 57.5 ikishika nafasi ya kwanza duniani. 

Ripoti ya Counterpoint imeeleza kuwa mafanikio ya Samsung yamechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya simu za A-series na utendaji bora wa toleo la Galaxy S24. 

Simu aina ya Samsung S24, iliyofanya vizuri kwa mauzo kutoka kampuni ya Samsung mwaka 2024. Picha|zdnet

Licha ya Samsung kuongoza kwa mauzo ya simu, mauzo yake yameshuka kwa asilimia 2 ikilinganishwa na mwaka jana. Samsung inamiliki asilimia 19 ya soko la simu duniani. 

Apple imeshika nafasi ya pili baada ya kuuza simu milioni 54.5 na kumiliki soko la simu duniani kwa asilimia 16 chini kidogo ya mshindani Samsung, kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Korea Kusini.

Kampuni ya Apple ya Marekani imetajwa kama chapa (brand) kubwa zaidi duniani, ikisaidiwa na uzinduzi wa iPhone16, licha ya mauzo ya simu hizo kubaki kiwango kile kile cha mwaka jana.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Apple inatarajia mahitaji ya iPhone16 yataendelea kuwa thabiti kutokana na idadi kubwa ya watumiaji wa iPhone waliopo sasa. 

Xiaomi ikishikilia nafasi ya tatu imendeleza kasi yake nzuri ya ukuaji ambapo imeuza simu milioni 42.8 na kumiliki soko kwa asilimia 14 ikiongezeka kutoka asilimia 8 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kampuni hiyo ya China pia ilitawala kwa muda nafasi ya pili katika orodha ya makampuni yanayoongoza kwa mauzo ya simu Agosti 2024.

Oppo imekamata nafasi ya nne na kuweka rekodi ya mauzo yake ya juu zaidi tangu robo ya tatu ya mwaka 2023. Oppo inamiliki asilimia 9 ya soko la simu huku mauzo ya jumla katika kampuni hiyo yakishuka kwa asilimia 3.

Vivo imezidi kushinda washindani wake, ikikua kwa kasi zaidi mwaka hadi mwaka kati ya kampuni tano bora katika robo ya tatu ya mwaka 2024. Vivo sasa imekuwa mtengenezaji na mzambazaji namba moja (OEM) katika masoko mawili makubwa zaidi ya simu za mkono duniani ya China na India.

Makampuni kama Tecno, Infinix, Itel na mengineyo kwa pamoja yanamiliki asilimia 34 ya soko la simu duniani. 

Ripoti ya Counterpoint inaeleza kuwa soko la simu za mkono duniani kwa robo tatu ya mwaka 2024 limeongezeka kwa asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka jana, huku jumla ya simu milioni 310 zikiingizwa sokoni.

Ukuaji huu wa soko unatokana na uboreshaji wa bidhaa, mipango mizuri ya bei na mahitaji makubwa ya simu za kiwango cha chini na kati, hasa katika masoko yanayoendelea kama Afrika, Amerika ya Kusini, na Asia-Pasifiki. 

Kampuni kubwa za simu zinaendelea kubuni mbinu mbalimbali ili kubaki katika ushindani wa soko la simu duniani kwa kuvutia kuvutia watumiaji wapya  na kuboresha uwezo na muonekano wa vifaa hivyo vya mawasiliano.

Simu aina ya iPhone 15, iliyoongoza kwa mauzo robo ya tatu ya mwaka 2024. Picha| TechRada

Ni aina gani ya simu imeuzwa zaidi mwaka huu?

Utata juu ya suala la toleo gani la simu limeuza zaidi kwa robo ya tatu ya mwaka 2024 umemalizika mara baada ya takwimu kuhusiana na mauzo ya matoleo ya simu kwa makampuni mbalimbali kuwekwa wazi.

Counterpoint Research inaeleza kuwa katika robo ya tatu ya mwaka 2024, iPhone 15 ndio simu iliyouzwa kwa wingi ikifuatiwa na iPhone 15 Pro Max na iPhone 15 Pro.

Hata hivyo, katika mauzo ya jumla, Apple imeshika nafasi ya pili ikitanguliwa na Samsung ambayo simu yake aina ya Galaxy S24 imeshika nafasi ya 4 miongoni mwa simu zilizonunuliwa zaidi miezi tisa iliyopita.

Galaxy S24 imekuwa maarufu kutokana na mkazo mkubwa wa masoko kuhusu uwezo wake wa GenAI na teknolojia ya kisasa katika maeneo kama kamera na muundo. Nafasi ya tano hadi ya 10 ilishikiliwa na simu za Samsung na kufanya orodha ya 10 bora kushikiliwa na kampuni mbili tu yaani Apple na Samsung.

Wataalam wa masuala ya teknolojia duniani wanaeleza kuwa matumizi ya GenAI katika simu za mkono limekuwa kipengele muhimu kinachowavutia wateja, na kampuni hizi mbili zinatarajiwa kuendelea kutawala soko katika kipindi kijacho.

Enable Notifications OK No thanks