Mbivu, mbichi wagombea urais Chaumma kujulikana Agosti 7, 2025

July 31, 2025 10:42 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na uombea kwa afasi ya Urais wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimetangaza ratiba rasmi ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wake kwa nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwemo nafasi ya Urais wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi ya Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, John Mrema, mchakato huo umeanza Julai 29 hadi Agosti 4, 2025 ambapo wanachama wenye nia ya kugombea Urais wa Tanzania na Zanzibar wanapaswa kuwasilisha barua kwa katibu mkuu wa chama.

Ifikapo Agosti 5, 2025, Sekretarieti ya chama itakutana kuchakata matokeo ya utafiti wa maoni ya watu mbalimbali waliopendekezwa kugombea nafasi hizo, huku kamati kuu na halmashauri kuu zikitarajiwa kupokea taarifa na kutoa mapendekezo kati ya Agosti 6 hadi 7, 2025.

Aidha, chama hicho pia kimetoa ratiba ya uteuzi wa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani ambapo kulingana na ratiba hiyo Agosti 15, 2025 ni mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo kupitia ofisi za chama ngazi ya mikoa na taifa.

Agosti 16 mpaka 17, 2025 kamati za utendaji za mikoa zitaketi kuchakata taarifa za wagombea na kuwasilisha mapendekezo kwa Sekretarieti ya Taifa. Na Agosti 17 mpaka 18, 2025 Sekretarieti itapitia taarifa hizo na kuziwasilisha kwa Kamati Kuu.

Kamati kuu itakutana kuandaa mapendekezo ya mwisho ya uteuzi na kuyawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya Taifa Agosti 20 mpaka 21, 2025.

Chaumma ni moja kati ya vyama vya siasa nchini vilivyojizolea umaarufu mkubwa hivi karibuni mara baada ya baadhi ya wanachama kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujiunga na chama hicho kutokana na kutounga mkono msimamo wa Chadema wa kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2025 (No Reforms, No Election)

Kutoka kwa ratiba ya Chaumma kunadhihirisha kupamba moto kwa shughuli za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 baina ya vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Itakumbukwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia kimekwisha anza mchakato wake wa kupata wagombea kwa nafasi hizo na tayari uteuzi wa awali wa wagombea umekwisha tangazwa. 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks