Mbinu za kuongeza kasi ya intaneti nyumbani, ofisini
- Kama unatumia”router”, hakikisha iko karibu na eneo lako la kazi.
- Jaribu kuizima na kuiwasha router au simu yako ili kuipumzisha kidogo.
- Tumia intaneti ya waya kupunguza vikwazo vya intaneti kupenya kwenye kompyuta yako.
Dar es Salaam. Hakuna anayefurahia intaneti yenye kasi ya ndogo. Kila mtu anatamani apakue filamu ndani ya dakika tano au chini ya hapo na kuperuzi na kutafuta vitu kwa haraka mtandaoni mara baada ya kubofya tovuti.
Lakini kile kiduara kizungukacho wakati unasubiri kuingia kwenye mitandao kama YouTube ama kugoma kwa ile video unayoitazama kwenye Instagram, hakika ni kero kwa watumiaji wengi wa simu janja na kompyuta.
Tatizo hilo linasababishwa na intaneti yenye kasi ya kobe au ndogo. Zipo sababu nyingi zinazochangia hali hiyo ikiwemo kuweka vifaa vya kusambaza intaneti sehemu ambayo siyo rafiki na kuzuia kifaa chako kufikia kasi yake ya intaneti.
Unawezaje kuboresha kasi ya intaneti yako wakati ukitumia simu au kompyuta?
- Badilisha sehemu unayoweka router yako
Kifaa hicho kinatumika kugawa intaneti kwa watu waliopo eneo moja kutoka kwa watoa huduma za mtandao huo..
Mtaalamu wa masuala ya kompyuta kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) Mike Roosevelt amesema kifaa hicho kinaweza kisikupatie intaneti inayoeleweka kwa sababu mara nyingi kinaathiriwa na vikwazo vikiwemo ukuta, miti na majengo marefu.
Amesema kama unatumia kifaa hicho nyumbani, hakikisha unakiweka sehemu ambayo unakuwepo muda mwingi au karibu na eneo unalofanyia kazi ili kurahisisha upatikanaji wa intaneti.
“Kama unatumia muda wako mwingi sebuleni, weka router yako kwenye sehemu ambayo haina vikwazo na kama ni chumbani, basi fanya hivyo hivyo,” amesema Roosevelt.
Hakikisha unaweka router yako sehemu ambayo unakuwepo muda mwingi au karibu na eneo unalofanyia kazi ili kurahisisha upatikanaji wa intaneti. Picha| Giphy.
- Tumia intaneti ya waya
Intaneti isiyotumia waya (wireless) mara nyingi inakutana na vikwazo lakini ukitumia intaneti ya waya kutoka kwenye kifaa husika, changamoto ya kasi ya intaneti utaisikia kwa majirani tu.
“Router nyingi huja na chaguo la kutumia waya au la, ukichagua kutumia waya hautapata vikwazo vya kasi ya intaneti yako kama yule anayetumia waya,” amesema Roosevelt kuwa mfumo huu unafaa kwa watu wa ofisini na hata wanaofanya kazi wakiwa nyumbani.
- Tumia intaneti ya makampuni binafsi
Zipo kampuni ambazo zinajishughulisha zinatoa huduma ya intaneti kwa taasisi na watu binafsi ikiwemo ya Raha Telecom.
Kupitia njia hii, itakuwa ni rahisi kwako kupata intaneti yenye uhakika japo Roosevelt ameshauri kufanya utafiti kabla ya kukurupuka kuchagua kampuni ya kukupatia huduma za intaneti.
- Weka simu yako kwenye kasi ya mwisho
Kwa ambao wanatumia intaneti isiyo ya waya hasa ya kampuni za mawasiliano ya simu, unashauriwa kuweka kasi ya intaneti hadi mwisho kutokana na jinsi simu yako inavyoruhusu.
Endapo simu yako inaruhusu intaneti yenye kasi ya 4G, ni vizuri ukaiweka kwenye kasi hiyo kwani kupunguza kasi yake, kunaathiri utendaji kazi wako.
“Unaweza ukakuta unalalamika simu yako au mtandao wako hauna kasi ya intaneti ukilinganisha na wenziko kumbe wenzako wanatumia 4G na wewe umeng’ang’ana na 3G yako,” amesema Roosevelt.
Zinazohusiana
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
- Fahamu haya kuhusu matumizi ya intaneti, mitandao ya kijamii duniani
- Huu ndiyo mtandao ghali zaidi wa intaneti Tanzania
- Pumzisha simu au router yako
Tovuti ya reviews.org imeandika kuwa, simu na router ni kama vifaa vingine vya kielektroniki vikitumika muda mrefu hupunguza kasi ya utendaji jambo linaloweza kuathiri upatikanaji wa intaneti kwa ajili ya kazi zako.
Unashauriwa kuizima na kisha kuipumzisha walau kwa dakika tano hadi kumi na kuiwasha tena. Utakuwa umeipatia muda wa kupumua.
Na hata kama hauitumii intaneti ya simu au router hauna haja ya kuendelea kuiacha imewashwa.
Kama bado unapata changamoto ya kasi ndogo ya intaneti ni vema umjulishe mtoa huduma wako ili kubaini ni nini kinasababisha hali hiyo.
Kuwa huru kutembelea kurasa zetu za mitandao ya kijamii na kutuambia ni nini unahitaji kufahamu.