Mazao, bidhaa zilizotikisa mwaka 2018

December 31, 2018 11:34 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mitikisiko hiyo ilizua sintofahamu ya kuadimika na kupanda kwa bei ya mazao na bidhaa hizo kwa kipindi fulani.
  • Kahawa, korosho na mbaazi ni mazao ya biashara ambayo yanategemewa zaidi kuingizia nchi fedha za kigeni. 
  • Sukari na mafuta ya kupikia yanagusa moja kwa moja maisha ya watanzania na kukidhi mahitaji ya familia.
  • Serikali, wadau, wakulima wapo tayari kudhibiti mitikisiko ya namna hii mwaka 2019?

Ni kilele cha mwaka 2018 lakini yapo mengi ya kukumbuka ambayo yanatoa funzo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa wakati tukijiandaa kuingia mwaka 2019. 

Kuna kila sababu ya kutazama na hata kujikumbusha mtikisiko uliojitokeza juu mazao na bidhaa za korosho, kawaha, mbaazi, sukari na mafuta ya kula. Kimsingi kupatikana au kuadimika kwa bidhaa hizo kulileta gumzo katika jamii kwasababu zinagusa maisha ya watanzania wanaozitumia. 

Mwenendo wa bei wa bidhaa na mazao hayo ulikuwaje? Ni matukio gani yaliyojitokeza mpaka kupewa nafasi ya kuangaliwa kwa jicho la tatu ili mwaka unaofuata akawe wa neema zaidi?


Anguko bei ya mbaazi 

Mapema Aprili mwaka huu, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya aliwataka wakulima wa mbaazi kutafuta soko la ndani na kutumia zao hilo kwa chakula baada ya wanunuzi wakubwa toka nchi za nje kama India kusitisha mkataba na Tanzania wa kununua zao hilo katika mwaka wa 2016/2017. 

Bei ya Mbaazi iliimarika katika msimu wa mwaka 2015 ambapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,800 hadi Sh3,000 na msimu uliofuata wa 2016 uzalishaji uliongezeka zaidi lakini matatizo ya soko yakaanza kujitokeza. 

Mpaka kufikia msimu wa 2017, inaelezwa kuwa bei ilishuka takriban mara 20 hadi Sh150 kwa kilo na kuathiri wakulima wengi wao zao hilo nchini.

Oktoba 9 mwaka huu  Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba aliweka wazi kuwa viwanda vitatu vya  kuchakata mbaazi vinajengwa mkoani Arusha, Dar es Salaam na Morogoro katika eneo la Mtego wa Simba ili kujibu kero ya muda mrefu ya wakulima kukosa soko la uhakika la zao hilo.

Huenda kukamilika kwa viwanda hivyo kutaleta ahueni kwa wakulima wa mbaazi nchini. Ni suala la muda tu.


Zinazohusiana:


Sakata la kutoroshwa kahawa nje nchi

Kama ilivyo kwa mbaazi, bei ya kahawa ilitikisa mwaka huu hasa baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutangaza mfumo wa kuuza kahawa kwenye mnada wa pamoja unaofanyika kila mwaka. 

Katika mfumo huo mpya,  wakulima hawaruhusiwi tena kuuza kahawa kwa watu binafsi wanaowafuata mashambani au kupeleka nje ya nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali 

“Kahawa itauzwa katika minada tu na utaratibu wa kutoa vibali kwa wanunuzi wa kahawa kwenda vijijini marufuku kuanzia sasa, kama kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi,” alisema Majaliwa Aprili mwaka huu. 

Licha ya utaratibu huo kuwekwa wakulima wa kahawa hasa wa mikoa ya Kagera, Arusha na Kilimanjaro walikuwa wakivusha kahawa hadi katika nchi za Kenya, Burundi na Uganda ambako inasemekana kuna bei nzuri ya zao hilo la biashara nchini. 

Kufuatia hali hiyo, Oktoba 8, 2018, Rais John Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera Augustine Ollomi, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kyerwa Justine Joseph, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kyerwa Everist Kivuyo na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kyerwa Robert Marwa.

Viongozi hao wa Polisi walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya kahawa katika Wilaya ya Kyerwa pamoja na tuhuma nyingine.

Lakini ilipofika Novemba 10, 2018 Rais John Magufuli tena aliwafuta kazi mawaziri Dk Charles Tizeba wa Wizara ya Kilimo na Dk Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kile kinachodaiwa kushindwa kusimamia na kudhibiti utoroshaji wa kahawa. 

Mpaka sasa Serikali imeshikilia msimamo wake wa kuuza kahawa kwenye mnada wa pamoja ikiwa ni njia ya kudhibiti mdororo wa bei na upotevu wa mapato ya ushuru na kodi.

Kahawa kama zao la biashara nalo lilitikisa Serikali ambapo baadhi ya watendaji walisimamishwa kazi kwa madai ya kuhusika na magendo ya zao hilo. Picha| DailyNews.

Bei ya korosho iling’oka na mawaziri wawili

Taifa pia limeshuhudia sakata la kudorora kwa bei ya korosho katika msimu huu, jambo lilofanya wakulima kugomea bei iliyotangazwa na wanunuzi katika mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Ruvuma.

Katika msimu huu mpya wa mauzo wa mwaka 2018/2019 bei zilizokatawaliwa na  wakulima zilikuwa ni kati ya Sh1,771 na 2,717 kwa kilo moja, ambapo ni chini kwa takriban mara mbili ya zile zilizotumika mwaka jana zilizokuwa zimefikia hadi Sh4,128 kwa kilo. 

Serikali ilichukua jukumu la kununua korosho yote ya wakulima inayofikia tani 220,000 kwa bei ya Sh3,300 kwa kutumia vikosi vya Jeshi la na kuwazuia wanunuzi binafsi kununua zao hilo kwa bei waliyoitaka wao. 

“Nimeamua kusitisha mnada na sasa Serikali itanunua yenyewe kwa gharama ya Sh3,300 kwa kilo,” alisema Rais Magufuli  aliyekuwa akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri wapya Ikulu Novemba 12, 2018.

Lakini sakata hilo liliondoka na mawaziri wawili Dk. Tizeba na Mwijage na kuvunjwa kwa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Anna Abdallah kwasababu walishindwa kusimamia maslahi ya wakulima wa korosho. 

Juzi Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga aliiambia Nukta kuwa tayari Serikali imeshakusanya tani 188,799 na wakulima 100,534 wameshalipwa fedha zao kiasi cha Sh206.09 bilioni. Wakulima wengine wanasubiri uhakiki.

Hata hivyo, kuna kila dalili kuwa Serikali haitazichakata korosho zote kutokana na uwezo mdogo wa viwanda vya ndani na Waziri Hasunga anasema wapo tayari kupokea wanunuzi wakubwa watakaonunua zaidi ya tani 100,000 kwa bei nzuri na kuuza ziada ya takriban tani 150,000.

 Mawaziri Dk Charles Tizeba wa Wizara ya Kilimo (kulia) na Dk Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kabla ya kuondolewa katika nyadhifa zao. Picha] Wazo huru.

Kuadimika kwa mafuta ya kula sokoni

Mei mwaka huu mafuta ya kula yaliadimika mtaani baada ya   Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzizuia meli za mafuta kwa zaidi ya mwezi mmoja  kushusha mzigo mpaka wamiliki wake watakapolipa kodi.

Utata wa kulipa kodi iliyokuwa ikidaiwa na TRA, ulitokana na madai kuwa mafuta yaliyoingizwa ni safi ilhali wamiliki wakieleza ni ghafi.

Kwa utaratibu uliopo, mafuta safi ya kula yanayoingizwa kutoka nje ya nchi hulipiwa kodi ya asilimia 25 wakati ghafi yanatozwa asilimia 10.

Sakata hilo lililodumu kwa siku 10, lilimalizwa na Rais John Magufuli aliyeagiza kampuni tatu za mafuta kulipia ushuru wa matanki 43 na kuagiza kufanyika haraka kwa marekebisho ya sheria ya uingizaji wa mafuta ghafi nchini. 

 Sukari na mafuta ya kupikia yanagusa moja kwa moja maisha ya watanzania na kukidhi mahitaji ya familia. Picha|Dar24.

Bunge nalo lilitikiswa na tofauti ya bei ya sukari

Sakata hilo lilikuwa la aina yake katika kikao cha bunge kilichofanyika Mei 8, 2018 baada ya kuibuka mvutano kati ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Mbunge wa Mpendae, Salim Hassan Turky ambaye alitaka kujua ni kwanini bei ya sukari ni tofauti kwa pande mbili za Muungano.

Turky pia alitaka jibu la Serikali ni kwa nini sukari ya kilo 50 inauzwa kwa bei ya Sh110,000 Tanzania bara wakati Zanzibar kuna kiwanda cha sukari kinachouza kilo hizo wa bei ya Sh65,000. 

Hali hiyo ilienda sambamba na kuadimika kwa sukari mtaani huku Serikali ikidai baadhi ya wafanyabiashara wameficha ili kufaidika na bei kubwa wakati wa kipindi cha mfungo wa Ramadhan.

Wakati anajibu swali hilo, Mwijage alisema gharama za uzalishaji sukari kwa viwanda vya Tanzania ni kubwa kuliko kwa viwanda vya Zanzibar, jambo lililoibua kelele za wabunge kuonyesha kutoridhishwa na majibu ya waziri huyo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Majaliwa alitoa kauli na kuagiza wafanyabiashara waachilie sukari iliyofichwa na kuangalia upya kwa tofauti za bei ya bidhaa hiyo inayotegemewa na watazania wengi kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.

Lakini kama Taifa tumejipangaje kuhakikisha mitikisiko kama hii iliyogusa bidhaa muhimu haitokei tena mwaka ujao ili watanzania waendelee kufaidika na rasilimali zinazowazunguka? 

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV