Mauzo ya nta yapaa kwa asilimia 83, asali yashuka

July 31, 2023 1:28 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yameongezeka kutoka kutoka Sh6.4 bilioni mwaka 2021 hadi Sh11.9 bilioni mwaka 2022.
  • Kupungua kwa maambukizi ya Uviko-19 kumechangia kupaa kwa mauzo hayo.
  • Serikali yajipanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki.

Dar es Salaam. Mauzo ya nta ya Tanzania katika masoko ya nje yameendelea kupaa hadi kufikia Sh11.9 bilioni huku mauzo ya asali yakiporomoka jambo linalofungua fursa kwa Watanzania kuongeza uzalishaji ili  kufaidika na soko la kimataifa la mazao ya nyuki.

Mazao makuu ya nyuki ni pamoja na asali, nta, chavua, gundi ya nyuki na sumu ya nyuki. Asali hutengenezwa na nyuki na kutumika katika shughuli mbalimbali za chakula, urembo na matibabu.

Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022, kinachotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) mauzo ya nta yamepaa kwa asilimia 83 kutoka Sh6.4 bilioni mwaka 2021 hadi Sh11.9 bilioni mwaka 2022.

Ongezeko hilo la mauzo ya nta ni sawa na Sh5.4 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Fedha hizo zimetokana na mauzo ya tani 793.5 za nta katika mataifa mbalimbali yenye uhitaji wa bidhaa hiyo inayotumika zaidi katika urembo, pamoja na utengenezaji wa madawa na mahitaji ya nyumbani.

Sababu kubwa iliyochangia kuongezeka kwa mauzo hayo ni kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa Uviko – 19 kulikosababisha kurejea kwa shughuli za kiuchumi.

Aidha, uhamasishaji uliofanyika kwa wauzaji wa ndani na nje umechangia kuongezeka kwa masoko mapya huku matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa mazao ya nyuki (Honey Traceability System) ukichangia kuongeza ufanisi zaidi.


Zinazohusiana


Mauzo ya asali yaporomoka

Wakati wauzaji wa nta wakifurahia kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi, mauzo ya asaliyameshuka kwa asilimia 21.3.

Mwaka 2021 kulikuwa na jumla ya mauzo ya Sh19.8 zilizopungua hadi kufikia Sh15.6 bilioni mwaka 2022.

Kwa mujibu wa NBS kupungua huko kwa mauzo katika zao la nyuki kulitokana na kuyumba kwa soko la asali katika soko la nje.

Hata hivyo uzalishaji wa zao hilo muhimu katika shughuli za afya, urembo na biashara uliongezeka kiduchu kwa asilimia 0.8 kutoka tani 31,442 zilzozalishwa mwaka 2021 hadi tani 31,695 mwaka 2022.

Kati hizo zilizouzwa ni tani 1,988 zilizoingiza Sh15.6 bilioni kutoka nchi za nje ukilinganishana tani 1,988 zenye thamani ya Sh19.8 bilioni  zilizouzwa mwaka 2021.

Licha ya kuporomoka huko kwa mauzo, bado asali inayozalishwa nchini ina ubora kiasi cha kushindanishwa na asali za mataifa mengine.

Mathalani mwaka 2022 asali inayozalishwa Tanzania ilishirika nafasi ya pili kwa ubora  katika mashindano yaliyofanyika kwenye Kongamano la Wafugaji Nyuki Kanda ya Afrika (African Symposium) nchini Afrika ya Kusini mwezi Machi, 2023.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, asali hiyo ni ile inayozalishwa kutoka katika miti jamii ya miombo iliyopo maeneo mengi nchini.

Wizara hiyo imesema mazao hayo ya nyuki (asali na nta) yaliyozalishwa nchini kwa mwaka 2022 yaliuzwa zaidi katika nchi za Marekani, Ujerumani, Japan, Poland, Ireland na New Zealand.

Serikali yajipanga kuimarisha uzalishaji wa mazao ya nyuki

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Nchengerwa aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya mapato na matumizi Bungeni kwa mwaka 2023/2024 amesema Serikali imejipanga  kutoa elimu na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uzalishaji na ufanyaji wa biashara hiyo.

“Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) atatoa elimu kwa wafugaji nyuki 1,228 kuhusu mbinu bora za ufugaji nyuki na kutengeneza mizinga 1,000 kwa ajili ya kuigawa kwa wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi, amesema Waziri

Sambamba na hayo, ili kuwezesha biashara ya uuzaji wa mazao ya nyuki kimataifa Wizara itaanza taratibu za kuandaa rajamu (branding) ya asali inayozalishwa nchini ili kuchochea soko la kimataifa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW