Mauzo ya asali nje ya nchi yaongezeka zaidi mara nne, nta ikishuka

June 17, 2019 2:08 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mauzo hayo yameongezeka kutoka tani 240.8 mwaka 2017 hadi tani 1,095.9 mwaka jana na kuipatia Tanzania Sh9.34 bilioni. 
  • Kiasi kinachosafirisha ni kidogo ukilinganisha na asali inayovunwa. 
  • Mauzo ya nta ambayo ni zao la nyuki yaporomoka kwa asilimia 29.8. 
  • Serikali imesema inaendelea kujipanga kuyafikia masoko ya kimataifa.

Dar es Salaam. Mauzo ya asali nje ya nchi yameongezeka zaidi ya mara nne ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jambo linalofungua fursa kwa Watanzania kuongeza uzalishaji na kufaidika na soko la kimataifa la mazao ya nyuki.

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, mauzo hayo yameongezeka kutoka tani 240.8 mwaka 2017 hadi tani 1,095.9 mwaka jana na kuipatia Tanzania Sh9.34 bilioni. 

Kitabu hicho, kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kinaeleza kuwa ongezeko la thamani ya mauzo ya asali nje ya nchi lilitokana na kuimarika kwa bei ya asali katika soko la kimataifa na hivyo asali ya Tanzania kupata fursa ya kuuzwa kwa wingi. 

Mafanikio hayo pia yalichangiwa na kuimarika kwa uzalishaji wa asali ambayo inatokana na nyuki ambapo uzalishaji mwaka jana uliongezeka mara mbili hadi tani 30,340 za asali ikilinganishwa na tani 14,082 za mwaka 2017.

Hata hivyo,  bado kiasi kilichosafirisha nje ya nchi ni kidogo ikilinganishwa na kiasi cha  tani 29,244.1 mbazo hazikusafirishwa nje nchi mwaka jana, jambo linakwamisha nchi kufaidika na fedha za kigeni ambazo ni muhimu katika uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi. 


Zinazohusiana: 


Wakati mauzo ya asali yakiongezeka, mauzo ya nta ambayo ni miongoni mwa mazao ya nyuki yameshuka kwa asilimia 29.8 ndani ya mwaka mmoja. 

“Aidha, tani 1,440 za nta zilizalishwa mwaka 2018 ikilinganishwa na tani 728 mwaka 2017. Kati ya kiasi hicho, tani 143 za nta zenye thamani ya shilingi milioni 1,287.1 ziliuzwa nje mwaka 2018 ikilinganishwa na tani 203.9 zenye thamani ya shilingi milioni 6,879.2 zilizouzwa mwaka 2017,” inasomeka sehemu ya kitabu hicho na kuongeza kuwa;,  

“Kiasi cha nta kilichouzwa nje ya nchi kilipungua kwa mwaka 2018 licha ya uzalishaji kuongezeka kutokana na kubadilika kwa bei ya nta katika soko la dunia.”

Mwenendo wa mauzo ya asali na nta nje ya nchi yanatoa changamoto kwa wazalishaji na Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza juhudi za uzalishaji na kuyafikia masoko ya kimataifa, ikizingatiwa kuwa kiasi cha mazao hayo kinachosafirisha ni kidogo ukilinganisha na kile kinachobaki nchini. 

Inakadiriwa kuwa, Tanzania ina masoko takriban 24 ya mazao ya nyuki duniani zikiwemo nchi za Afrika Kusini, Botswana, India, Canada, Namibia, Dubai, Kuwait na Iran lakini bado wakulima hawajafaidika kikamilifu na fursa hiyo kutokana na changamoto mbalimbali.

Mazao makuu ya nyuki ni pamoja na asali, nta, chavua, gundi ya nyuki na sumu ya nyuki. Asali hutengenezwa na nyuki na kutumika katika shughuli mbalimbali za chakula, urembo na matibabu. 

Mazao makuu ya nyuki ni pamoja na asali, nta, chavua, gundi ya nyuki na sumu ya nyuki. Asali hutengenezwa na nyuki na kutumika katika shughuli mbalimbali za chakula, urembo na matibabu. Picha|Mtandao. 

Mikakati ya Serikali kukuza mazao ya nyuki

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2019/2020 alisema wanaendelea kujenga uwezo wa taasisi na mafunzo ya misitu na ufugaji nyuki, kuwezesha wananchi kunufaika na misitu na uhifadhi wa misitu ya mazingira asilia.

“Elimu kwa umma juu ya uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki, itaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye maonesho ya Saba Saba, Nane Nane, Siku ya Kupanda Miti Kitaifa, Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa, Siku ya Mazingira Duniani na Siku ya Utumishi wa Umma,” alisema Dk Kigwangalla. 

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema wizara yake  itafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki na Sheria ya Misitu ili kufungua fursa zaidi kwa nchi kunufaika na mazao ya nyuki. 

Enable Notifications OK No thanks