Maumivu kwa wanawake, Serikali ikipendekeza kutoza ushuru mawigi
- Inakusudia kutoza ushuru wa asilimia 10 kwenye mawigi yanazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwa nywele hizo zinazoagizwa nje ya nchi.
- Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.
Dar es Salaam. Watumiaji wa nywele bandia maarufu kama mawigi huenda wakatoboa zaidi mifuko yao kuanzia Julai mwaka huu baada ya Serikali kupendekeza kutoza ushuru bidhaa hizo zinazopendwa zaidi na kina mama kwa ajili ya urembo.
Katika pendekezo hilo, Serikali inataka kutoza asilimia 10 kwenye nywele bandia (Mawigi) zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 ya ushuru kwa nywele hizo zinazoagizwa nje ya nchi ili kuongeza mapato ya Serikali.
Uamuzi huo wa Serikali huenda ukaongeza bei ya nywele hizo bandia za ndani na nje ya nchi na kuwafanya wanawake kuvunja zaidi vibubu ili kuendeleza sifa za urembo waliokuwa nao awali kabla ya kuanzishwa kwa ushuru huo.
Mawigi yamekuwa yakitumika na wanawake kufunika vichwa vyao ikiwa ni sehemu ya urembo na kuboresha muonekano wao mbele ya macho ya jamii.
Kusudio hilo limetangazwa leo bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2019/2020, ambapo amesema ushuru utakaotozwa katika bidha hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza mapato.
“Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali,” amesema Dk Mpango na kufuatiwa na shangwe za wabunge wakionyesha kufurahishwa na pendekezo hilo la Serikali inalokusudia kulitekeleza katika mwaka wa fedha ujao.
Shangwe hizo zilimlazimisha Waziri Mpango kusimama kwa muda huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akisikika akisema “hata kucha bandia ziongezewe ushuru.”
Zinazohusiana:
- Acha kuwaza kuwa mfanyabiashara, anza kufanya biashara
- Serikali yaeleza masimamo biashara ya kubandika kucha bandia
Mapendekezo hayo yanakuja ikiwa imepita miezi miwili tu tangu Serikali iliposema haina mpango wa kufunga biashara za saluni za kubandika kucha bandia baada ya kutokuwepo taarifa zozote za madhara ya matumizi ya kucha hizo zinazopendwa zaidi na baadhi ya wanawake nchini kwa ajili ya urembo.
Msimamo huo ulitolewa na Bungeni Aprili 29, 2019 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Khasim Ahmed aliyedai kuwa baadhi ya wanawake wameathirika sana na dawa za kuongeza makalio pamoja na matumizi ya kope na kucha bandia.
Saluni zinazotoa huduma za kubandika kucha bandia na mawigi, zimekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa wanawake na vijana nchini.
Kumekuwepo na msukumo mkubwa miongoni mwa jamii hususan bungeni katika kudhibiti matumizi ya bidhaa bandia kwa ajili ya urembo ili kudhibiti madhara yeyote ya kiafya yanayoweza kutokea kutokana na matumizi hayo.
Latest