Louis Favot bosi mpya Mixx Tanzania
- Favot anachukua mikoba ya Angelica Pesha ambaye amekuwa ndani ya kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 15 na kuhudumu kama CEO kwa miaka 6 tangu 2020.
Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za fedha kidijitali ya Mixx Tanzania imemteua Louis Favot kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa kampuni hiyo akichukua mikoba ya Angelica Pesha ambaye amekuwa ndani ya kampuni kwa zaidi ya miaka 15.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mixx Tanzania Favot ana uzoefu wa miaka 17 katika sekta za benki, mikopo midogo, fedha kwa njia ya simu na huduma za kifedha kidijitali, huku miaka 14 ya uzoefu wake ikiwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kabla ya kujiunga na Mixx Tanzania, Favot alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MVola, kampuni ya huduma za fedha kwa simu nchini Madagascar, ambako alisimamia mkakati wa kampuni na kuchangia katika mabadiliko yake kuelekea kuwa benki ya kwanza ya kidijitali nchini humo.
Zigo linalomsubiri
Uteuzi wa Favot unakuja wakati Mixx inaendelea kupanua huduma zake zaidi ya kutuma na kupokea fedha, ikijumuisha huduma za malipo, mikopo na akiba huku ushindani na teknolojia katika huduma za fedha vikikua na kuongezeka kwa kasi nchini Tanzania.
Kwa mantiki hiyo, Favot ana kibarua kizito mbele yake cha kuhakikisha Mixx inaendelea kushindana katika soko hilo kwa kuimarisha ubunifu wa bidhaa na kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha ili kuwapiga bao washindani wake.
Kwa mujibu wa TCRA, Mixx by Yas ni mtoa huduma wa pili kwa ukubwa katika soko la pesa mtandao nchini Tanzania, ikiwa na asilimia 32 ya akaunti za huduma hiyo, nyuma ya M-Pesa iliyokuwa na asilimia 40.6 katika robo iliyoishia Juni 2026.
Apokea kijiti cha Pesha
Favot anaingia madarakani akichukua mikoba ya Pesha, ambaye amekuwa sehemu ya safari ya biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 15 tangu enzi za Tigo Pesa, kabla ya huduma hiyo kubadilishwa na kuwa Mixx by Yas.
Pesha, ambaye alijiunga na Tigo Pesa mwaka 2011, amesimamia kipindi muhimu cha mabadiliko ya biashara hiyo kwa kipindi cha miaka sita tangu alipoteuliwa kuwa CEO mwaka 2020.
Mwaka 2025, kampuni hiyo iliripotiwa kuwa na zaidi ya watumiaji milioni 19, mawakala zaidi ya 200,000 na wafanyabiashara 450,000, huku ikiendelea kupanua huduma zake za kifedha kupitia teknolojia.