Rais Samia atoa sababu za kuteua na kutengua wakuu wa mikoa
- Asema kigezo cha utendaji kazi ndiyo kimeamua.
- Asema Katiba imempa mamlaka ya kuteua watu.
- Walioteuliwa awataka kuchapa kazi.
Dar es salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa ikiwemo kuwafuta kazi tisa kwa sababu ya kutoridhishwa na utendaji wa baadhi yao huku akieleza kuwa ana mamlaka ya kuchagua watu anaotaka kufanya nao kazi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus katika taarifa yake iliyotolewa Julai 28, 2022 alisema Rais Samia alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya tisa, kuwahamisha vituo vya kazi saba na wengine 10 kubakia kwenye vituo vyao.
Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha makatibu tawala wa mikoa na wakuu wa mikoa leo Agosti 1,2022 ikulu jijini Dar es salaam amesema mabadiliko hayo aliyoyafanya yanatokana na tathmini ya utendaji wa viongozi hao aliyoifanya ambapo baadhi walionekana hawana sifa tena ya kuondelea katika nafasi zao.
“Tulikaa na tukaangalia performance (utendaji) ya kila mmoja wenu na tulireview (tulipitia) wakuu wa mikoa, ma DC (Wakuu wa Wilaya), ma RAC (makatibu tawala wa mikoa) na ma DED (makatibu tawala wa wilaya), tulitumia siku nzima lakini pia nikawaachia kazi wenzangu wakaenda kujifungia,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema pia mabadiliko hayo yanalenga kuboresha utendaji wa viongozi wa Serikali hasa kuwatumikia wananchi huku akisema zoezi la uteuzi linafanyika kwa haki bila kujali kabila, rangi au jinsia ya mtu.
Aidha, Rais samia ameeleza kuwa maamuzi yoyote ya uteuzi aliyoyafanya yeye ndiyo wa kulaumiwa iwapo kuna mtu anadhani kuwa haukuwa sahihi, kwenye kuteua wamsamehe, ila katiba ya Tanzania inampa mamlaka ya kufanya mabadiliko hayo.
“Teuzi hizi zinafanya kwa mamlaka aliyopewa Rais na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…kifungu hicho kinatoa mamlaka kwa Rais kuanzisha ofisi na kufanya teuzi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali.
“Mpaka jina linatoka ni kazi ya Rais kuteua kama kumefanyika vizuri ni mimi nabeba na kama kumefanyika vibaya ni mimi nimebeba siangalii chochote naangalia sifa na uwezo,” amesisitiza.
Amesema aliowachagua anaamini wana uwezo na uchungu wa Tanzania na wataweza kumsaidia kuwatumikia Watanzania.
Soma zaidi
Atoa maagizo
Rais Aamia ameiagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoa mafunzo kwa wakuu wa mikoa wateule ili kupunguza lawama na utendaji kazi ulio chini ya viwango.
“Kila watakaoingia wafanyiwe mafunzo ya aina watakayofanyiwa wakuu wa mikoa ili tukumbushane na mtu asiwe na sababu ya kusema sikujua hili,” ameongeza Rais Samia.
Sambamba na hilo amewataka wateule hao kuzingatia miiko ya kazi zao, kujikita katika kuwatumikia wananchi na kuimarisha kazi ya ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao.
“Nendeni mkawahudumie wananchi kwa moyo safi na kwa akili yako…na ukifanya vizuri Mungu anakupeleka pazuri,” amesisitiza.