Deni la Serikali lazidi kupaa, Tanzania ikisisitiza kuendelea kuchukua mikopo
Dar es Salaam. Deni la Serikali ya Tanzania limeongezeka kwa takriban asilimia 14 katika kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ndiyo kiwango cha juu kabisa katika miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka 2020/21 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), deni la Serikali ya Tanzania limefikia Sh64.4 trilioni katika mwaka 2020/21 unaoishia mwezi Juni kutoka Sh56.5 trilioni ya mwaka 2019/21.
Hilo ni sawa na ongezeko la Sh7.9 trilioni au asilimia 13.9 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ulioopita.
Kiwango hicho ni cha juu kabisa ikilinganishwa na miaka mingine kati ya mwaka 2016/17 na 2020/21.
Kuongezeka kwa deni hilo kumetokana na kupokelewa kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo hususan inayochochea ukuaji wa uchumi.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli ya kisasa (SGR) na bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere katika mto Rufiji.
Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mpana kuhusu kuongezeka kwa deni la Serikali huku baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na wasoni wakionya kuwa deni likiwa kubwa linaweza kuiweka nchi rehani.
“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya ku-run nchi (kuongoza nchi) hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” alihoji Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai Desemba 28, 2021 kwenye mkutano huo wa kimila wa kabila la Wagogo mkoani Dodoma.
Hata hivyo, siku iliyofuata Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itaendelea kukopa mikopo yenye masharti nafuu ili kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na siyo kutoa fedha za ndani ikiwemo kodi.
“Tutaendelea na ujenzi wa miradi, kuna jitihada za kutuvunja moyo katika mikopo, hata hizo nchi zilizoendelea zina mikopo mikubwa kuzidi ya kwetu…,tutakopa tumalize miradi ya maendeleo,” alisema Rais Samia baada ya baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora Ikulu Jijini Dar es Salaam.