Ndugai na deni la Taifa: Nimekosa mimi, nimekosa sana
- Spika wa Bunge amuomba radhi Rais Samia pamoja na Watanzania.
- Amesema video zinazosambaa kuna “mambo yamekatwakatwa” na kupotosha ukweli.
Dar es salaam. Baada ya kuwepo mjadala mkali juu ya kauli yake kuhusu ongezeko la deni la Taifa, Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ameomba msamaha kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote akieleza kuwa kuna watu “walikatakata mambo” kwenye hotuba yake na kupotosha ukweli.
Mapema wiki iliyopita kulikuwa na video iliyosambaa mtandaoni ikimwonyesha kiongozi huyo wa Bunge akionya kuhusu kuongezeka kwa deni la Taifa na kueleza ipo siku “nchi itapigwa mnada”.
Video hizo zinazoonyesha kuwa Ndugai anapinga uchukuaji wa mikopo unaofanywa na Serikali ikiwemo trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani( IMF) zimezua mjadala mkubwa hasa katika mitandao ya kijamii na kusabanisha Spika huyo kuitisha mkutano na wanahabari kufafanua.
Katika ufafanuzi wake kwa wanahabari jijini Dodoma leo Januari 3, 2022, Ndugai amesema hakuna mahali ambapo amepinga jitihada za Serikali ikiwemo kuchukua mkopo huo wa IMF unaolenga kukabiliana na athari za Uviko-19 kijamii na kiuchumi.
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai wakati akizungumza na wanahabari jijini Dodoma. Picha| Millard Ayo.com
Ndugai amewaeleza wanahabari kuwa watu wanaosambaza video za baadhi ya mazungumzo yake katika mkutano wake na kikundi cha “Mikalile Ye Wanyausi” cha jamii ya wagogo jijini Dodoma Desemba 26 mwaka jana hawakumuelewa vizuri kile alichozungumza bali alilenga kuhamasisha kujenga uchumi kwa kulipa kodi, tozo na ushuru ili nchi iweze kujitegemea.
“Nimeona tukutane niweke sawa jambo hilo lilivyokuwa…hapakuwa na lolote la kukashifu au kudharau juhudi zozote za Serikali. Serikali ni baba yetu, Serikali ni mama yetu. Tunahitaji Serikali. We ‘need government’ (tunaihitaji Serikali) na tunaiunga mkono,” amesema Ndugai kwa upole.
Ndugai, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa, ameeleza kuwa hawezi pinga suala la mikopo kwa kuwa hata jimbo lake limefaidika katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba 150 vya madarasa ya kisasa yaliyogharimu takriban Sh3 bilioni.
- Mfumo wa ‘mali kauli’ unavyowaumiza wanawake sokoni Tanzania
- Deni la Serikali lazidi kupaa, Tanzania ikisisitiza kuendelea kuchukua mikopo
“Kwa hiyo nilitaka nifafanue hilo kwa kutaka ieleweke leo na ieleweke siku zote kwamba nchi nzima inafurahia kwa jinsi ya mkopo huu (wa IMF) ulivyokwenda na uwazi wake na tunatoa wito hata mikopo inayokuja huko mbele iende kwa taratibu za namna hiyo,” amesema Ndugai akibainisha kuwa hakuna mgongano wowote baina yake na Serikali.
Katika mkutano huo na wanahabari, Ndugai amesema hana nia ya kumvunja moyo Rais Samia katika jitihada zake za kuiletea nchi maendeleo.
“Kwa mara nyingine tena, kwa wale wote walioguswa visivyo nawaomba sana radhi lakini niwahakikishie mimi ni yule yule uimara wangu upo pale pale…na hili twende ndio maana mimi nimebeba yote na kusema nimekosa mimi nimekosa sana, nimekosa mimi Mungu anisamehe, Watanzania nisameheni, asanteni sana,” amesema.
Ndugai kwa wiki sasa amekuwa akishambuliwa mtandaoni na baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi kwa kauli yake hiyo huku baadhi wakieleza kuwa anaipinga Serikali.