Mapato yatokanayo na utalii wa kitaifa, kimataifa yapaa Tanzania

June 3, 2024 5:34 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mapato ya utalii wa kimataifa yamefikia 8.85 bilioni ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
  • Wizara yaanika vipaumbele vitakavyouza utalii nchini.

Dar es Salaam. Mapato yatokanayo na shughuli za utalii wa kimataifa yameongezeka kwa asilimia 161 kipindi cha miaka mitatu huku sababu zikitajwa kuwa ni kuimarishwa kwa miundombinu na mchango wa filamu ya ‘Royal Tour’.

Idadi hiyo ya mapato yatokanayo na utalii wa kimataifa imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1.3 sawa na Sh3.38 bilioni hadi Dola za Marekani milioni 3.4 sawa na Sh8.85 bilioni.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 leo Mei 31, 2024 bungeni jijini Dodoma amesema mapato ya utalii ya kitaifa pia yameongezeka kwa asilimia 279.


Soma zaidi:Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii 2024-25 yapungua kwa asilimia 47


“Pia, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Sh 46.3 bilioni mwaka 2021 hadi Sh175.3 bilioni Mwaka 2023 sawa na asilimia 279,” amesema Kairuki.

Waziri huyo pia amebainisha kuwa huenda mwishoni mwa mwaka 2023/24 Tanzania ikarekodi kiasi kikubwa zaidi cha mapato hayo jambo ambalo linaloweza kuchangia kukua kwa pato la Taifa.

Kwa mujibu wake hadi kufikia Aprili, 2024 wizara hiyo imekusanya Sh57.64 billioni  sawa na asilimia 73.54 ya lengo la mwaka utakaoishia Juni, 2024.

Wakati mapato yakiongezeka, Idadi ya watalii wa kimataifa nayo imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692  walioingia nchini mwaka 2021 hadi watalii 1.8 milioni mwaka  2023.

Aidha, idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 152, kutoka  watalii 788,933 hadi kufikia watalii 1,985,707 kwa mwaka 2023.

“Kwa hakika hii ni rekodi kubwa sana ambayo haijawahi kufikiwa katika nchi yetu,” ameongeza Kairuki wakati akiwasilisha takwimu hizo.

Waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali wakifanya utalii wa ndani na mafunzo  katika hifadhi ya misitu ya Amani – Nilo iliyopo wilaya ya Muheza mkoani Tanga.Picha|Daniel Mwingira/Nukta Africa.

Ili kuendelea kuvuna mapato na kuingiza watali wengi zaidi nchini, Waziri Kairuki aliainisha vipaumbele nane vya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 ambavyo ni pamoja na  kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia programu mbalimbali ikiwemo ‘Royal Tour’ katika mataifa mbalimbali

“Wizara itatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama ifuatavyo, kuendelea kutangaza utalii ndani na nje ya Nchi ikiwa ni mwendelezo wa programu maalum ya Tanzania the ‘Royal Tour’…

Filamu ya ‘Amazing Tanzania’ pamoja na mikakati mingine mikubwa kupitia matangazo katika ligi kuu za michezo mashuhuri duniani, matangazo kwenye ndege, misafara ya utangazaji utalii, matamasha makubwa ya kimataifa na mitandao mbalimbali ya kimataifa na vyombo vya habari,” amesema Kairuki.

Vipaumbele vingine ni kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi ili kuwezesha shughuli za utalii kufanyika.

Enable Notifications OK No thanks