Maoni mchanganyiko ukuaji wa biashara ya mtandaoni Tanzania
- Wafanyabiashara waitumia kutangaza na siyo kuuza bidhaa.
- Wengine wanaogopa kutapeliwa.
- Washauriwa kuchangamkia biashara hiyo kufaidika nayo.
Mwanza. Wakati biashara ya mtandaoni ikishika kasi duniani, wafanyabiashara mkoani Mwanza wamekuwa na maoni tofauti kuhusu aina hiyo ya biashara huku baadhi yao wakisema wanaitumia kutangaza na siyo kuuza bidhaa na huduma, jambo linalowafanya wapishane na fursa lukuki za mtandaoni.
Biashara ya mtandaoni (E-commerce) huusisha uuzaji, ununuzi na utangazaji wa bidhaa na huduma kwa mifumo ya kidijitali ikiwemo simu na kompyuta bila kujali mipaka ya nchi.
Ukuaji wa biashara hii duniani umechangiwa na maendeleo makubwa ya teknolojia na mawasiliano yanayofanyika mtandaoni na hivyo kurahisha usambazaji wa bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali.
Wakati Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazotumia aina hiyo ya biashara, watu wanaohudhuria maonyesho ya 16 ya wafanyabiashara wa Afrika Mashariki (TCCIA) jijini Mwanza wamekuwa na maoni tofauti kuhusu ukuaji wa biashara ya mtandaoni nchini.
Yusuph Almakasusi ni mfanyabaishara wa bidhaa za kitamaduni (Culture) amesema zamani kabla simu janja hazijawa nyingi hakukuwa na ulazima wa kutangaza bidhaa na mara nyingi walitumia maonyesho na semina mbalimbali kwenda kuuza bidhaa hizo.
“Lakini sasa hali ni tofauti, biashara na matangazo ya karne ya 21 yanategemea sana takonolojia katika kujitangaza na kutafuta masoko,” amesema Almakasusi na kuongeza kuwa kwa sasa wanawafikia kirahisi wateja wao na kwa muda mfupi.
“Ukweli ni kwamba usipofanya matangazo ya biashara kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa biashara yako yote uifanyayo itaishia kwa watu wachache tu wanaokuzunguka,” amesema.
Wafanyabiashara waliozungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) katika maonyesho hayo wamesema kwa sehemu kubwa wanatumia mitandao kutangaza bidhaa zao ili ziwafikie watu wengi huku wakiendelea kuimarisha mifumo ya asili ya mauzo katika maeneo yao.
“Tuligundua upo utapeli na biashara za mtandaoni ni ngumu. Wapo wachache waaminifu ambao wanaweza kufikisha bidhaa kwa wahusika, hivyo tukaona ni bora tukatumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa na ofisi zinakopatikana ili watu wafike huko kununua,” amesema Floriane Melone, mfanyabiashara wa bidhaa za nyumbani na za mazoezi jijini hapa.
Huenda wafanyabiashara hao wanapishana na fursa lukuki kwa wao kutumia mtandao kutangaza bidhaa tu na siyo kutumia kuuza na kuwafikishia wateja wao katika maeneo waliyopo.
Mfanyabiashara wa vyombo vya jikoni, Emirida Samson amesema dhana ya biashara ya mtandaoni ni pana inategemeana na uelewa na uwezo kuitumia ili ilete faida.
Amesema yeye anafikiri biashara hiyo imefungua wigo wa kutangaza bidhaa ili zifahamike na watu wengi na siyo kutumia mifumo ya kidijitali kuuza.
“Tunatumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zetu na maeneo tunayopatikana lakini sio kusafirisha kama wengine wanavyofanya, kikubwa ni kujitangaza ili watu wajue tunafanya nini na tunapatikana wapi ili wenye uhitaji wafike kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kujipatia bidhaa,” amesema Emirida.
Mwonekano wa mabanda katika maonyesho ya wafanyabiashara wa Afrika Mashariki (TCCIA) yanayoendelea katika viwanja vya Rock Mall. Maonyesho hayo yanatarajiwa kufungwa Septemba 5 mwaka huu. Picha| Mariam John.
Hata hivyo, inahitajika elimu kwa wafanyabiashara jinsi ya kutumia mifumo ya mauzo ya mtandaoni ili kuongeza wigo wa mapato kuliko kusubiri wateja waje katika maeneo yao.
Aliyewahi kuwa Meneja Uhusiano wa Jumia, Godfrey Kijanga amesema biashara kwa njia ya mtandao bado ni ngeni miongoni mwa Watanzania kutokana na kuzoea mifumo ya asili ya manunuzi ambayo imejengeka katika jamii kwa muda mrefu.
“Watanzania wengi bado wamekumbatia mifumo yao ya asili ya kufanya biashara na manunuzi. Wafanyabiashara bado wanategemea wateja kuja moja kwa moja madukani mwao na wateja nao bado wanaamini ili kupata bidhaa sahihi lazima uione, uiguse, uikague au kuichunguza pamoja na kuijaribu kama ikibidi,” amesema Kijanga.
Watanzania wanapaswa kujiandaa na kutumia teknolojia ya manunuzi ya mtandaoni na kutumia fursa hiyo kuboresha maisha na kuachana na dhana ambazo hazina tija kwao.
Mtaalamu wa kujitegemea wa programu za kompyuta, Florian Kaboda amesema kuwa muamko mdogo wa watu kutumia huduma ya biashara ya mtandaoni unatokana na Watanzania wengi kutogundua fursa zilizopo mtandaoni ambazo zinaweza kurahisisha maisha.
“Hata kama watumiaji wa intaneti wameongezeka, watu wengi hawajui fursa zilizopo wanaishia kwenye mitandao ya kijamii tu. Tunapasa kuitokomeza fikra ya aina hiyo,” amesema Kaboda.
Latest