Mamlaka ya anga Tanzania yakusudia kulifuta shirika la ndege la Fastjet

December 18, 2018 10:52 am · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema limepoteza sifa ya kuendelea kutoa huduma ya usafiri na kutoa notisi ya siku 28 ya kuja na mpango mkakati kwanini wasifungiwe.
  • Ukiondoa masharti hayo shirika hilo limeambiwa lilipe madeni yote ambayo linadaiwa na wadau mbalimbali, na kama watafungiwa wazingatie sheria zote juu ya maslahi ya wafanyakazi wao.
  • Wananchi watakiwa kuchagua mashirika mengine kuendelea na safari zao kuepusha usumbufu utakaoweza kujitokeza.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga TCAA imesema shirika la ndege la Fast jet limepoteza sifa ya kuendelea kutoa huduma ya usafiri na kutoa notisi ya siku 28 ya nia ya kulifuta kabisa shirika hilo la ndege binafsi nchini.

Tamko la TCAA linakuja ikiwa zimepita siku chache, baada ya waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha kununua asilimia 64 ya hisa za kampuni ya ndege ya Fastjet Tanzania, hivyo kuongeza hisa zake kufikia asilimia 68 kutoka asilimia nne aliyokuwa akimiliki awali.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, Hamza Johari ametoa notisi hiyo leo (Disemba 17, 2018) jijini Dar es Salaam mara baada ya kutokea sintofahamu mbalimbali za umiliki wa shirika hilo na kusababisha kusuasua kwa huduma za usafiri.

Hali hiyo imejitokeza baada ya aliyekuwa mmiliki kutoka Uingereza kusitisha utoaji wa pesa za uendeshaji na kuliuza shirika hilo kwa watanzania.

“Baada ya mabadiliko hayo, shirika limetetereka kwa kiasi kikubwa na kupoteza sifa ya uthibitisho,” amesema Johari.

Ukiondoa kutokuwa na uthibitisho na ukiukwaji wa makubaliano ya uendeshaji biashara amesema bado shirika hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni mengi. Baadhi ya madeni hayo ni ya Sh.1.4 bilioni inayodaiwa na TCAA. 

Licha ya notisi hiyo ya siku 28, Fastjet imepewa masharti mbalimbali ikiwemo kuja na mpango mkakati kwanini wasifungiwe na kutakiwa kusitisha safari zake ilizopanga mwaka huu.

“Wasitishe mauzo kwa abiria, walipe fidia na waombe kwenye mashirika mengine kwaajili ya kusafirisha abiria ambao walishakata tiketi tayari,” amesemaJohari.


Zinazohusiana: Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’

                           Hatua zitakazokusaidia umalize mchakato wa ‘Airport’ bila usumbufu


Pia wametakiwa  kulipa madeni yao yote ambayo wanadaiwa na wadau mbalimbali, na kama watafungiwa wazingatie sheria zote juu ya maslahi ya wafanyakazi wao.

Pamoja hayo, Johari amewataka wananchi wachague mashirika mengine kuendelea na safari zao kuepusha usumbufu utakaoweza kujitokeza wakati changamoto za shirika hilo zikitafutiwa ufumbuzi.

“Ni jukumu letu kuhakikisha tunawaambia watu kuhusu wajibu wetu hivyo mtumiaji wa huduma ana haki ya kuchagua na chagueni mashirika mengine yapo,” amesema Johari.

Taarifa zilizopatikana zinasema kuwa tayari FastJet imesimamisha safari zake zote na tayari imeanza mchakato wa kurudisha nauli kwa abiria waliokuwa wasafiri December na January mwakani. 

(Taarifa zaidi zitakujia hapa hapa)

 

Enable Notifications OK No thanks