Yaliyojificha nyuma ya mahusiano, ndoa zinazoanzia mtandaoni

February 24, 2021 12:57 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Licha ya kuwa wapo waliofanikiwa kupata wenzi wao kwa njia ya mitandao ya kijamii, bado baadhi ya wadau wanasita kuona hilo linawezekana. 
  • Viongozi wa dini wasema siyo jambo baya, lakini maadili na taratibu za mahusiano ya kidini lazima zifuatwe. 
  • Wataalamu washauri umakini, na kufanya utafiti binafsi kabla ya kumuamini mtu uliyekutana naye mtandaoni.

Dar es Salaam. Kwa sasa, unaweza kupata mwenzi wa maisha yako mahali popote. Iwe ni sokoni, kanisani na hata katika usafiri wa umma. Ni wewe kutumia vizuri fursa.

Wapo wanaokutana na wenzi wao kwenye sehemu za starehe, katika mashindano ya kukimbia, sehemu za maonyesho na hali inashangaza kuwa wapo waliopata wenzi wao kwa kukosea namba ya simu.

Orodha ya sehemu za kukutana na mwenzi sasa imeenda hadi katika mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram, Twitter na mitandao ya kutafuta wenzi (dating apps) ambako baadhi yao wameenda mbali zaidi na kufunga pingu za maisha. Bila shaka umewahi kukutana na hilo.

Miongoni mwa watu waliopata wenza wa maisha kupitia mitandao ya kijamii ni Aziza Mohammed, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye alifunguka ndoa na Hamisi Mruma Septemba mwaka 2019.

Aziza ambaye ni mtaalamu wa masoko alikutana na Mruma kwenye mtandao wa Twitter ndipo walipoona wana kila sababu ya kufunga pingu za maisha.

“Baada ya mwezi mmoja, tulikutana kwa mara ya kwanza. Alikuwa kama nilivyomuona kwenye picha sema tu mwili ulikua mdogo kiasi tofauti na kwenye picha. Hata baada ya kuonana, bado alisema hajabadili mawazo yake juu  yangu,” amesema Binti Mohammed ambaye pia ni mjasiriamali wa biashara ya mtandaoni. 

Ndani ya miezi mitatu ya kufahamiana, mahari ilitolewa, binti Mohammed akavalishwa pete na ndoa ikafungwa Septemba 27, 2020 mkoani Tanga na safari ya maisha ya wawili hao ikaanza rasmi.

Kukutana na watu mtandaoni siyo kibaya ilimradi wote mkiwa na lengo thabiti. Picha| Tulipe Media.

Stori za watu kukutana kwenye mitandao ya kijamii na kufunga ndoa, kwa sasa siyo kitu kigeni kwa sababu majukwaa hayo yanayotoa fursa pana ya watu kuwasiliana kwa karibu hata kama hawafamiani. 

Akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz), mwandishi wa vitabu kutoka Tanzania, Neema Ndanshau anasema anamfahamu binamu yake ambaye ameolewa na mtu aliyekutana naye kupitia mtandao wa Facebook.

Ndanshau amesema binamu yake na mumewe walikutana Facebook na walikua wakiishi majimbo tofauti tofauti wakati wakiwa Marekani.

“Walikuwa marafiki kwa muda mrefu na walioana baada ya miaka mitatu. Hadi sasa wapo kwenye ndoa ambayo imedumu kwa miaka 11,” anasimulia Ndanshau.

Wanaoanzisha mahusiano mtandaoni wanaongeza kila siku

Tovuti ya toptal.com katika andiko lake la “Tasnia ya kutafuta wenza: Biashara ya Mapenzi” inaeleza kuwa matumizi ya huduma za kukutanisha wapenzi mtandaoni ziliongezeka mara tatu zaidi kutoka mwaka 2013 hadi mwaka 2015 huku watumiaji wakubwa wakiwa watu walio na miaka kati ya 18 na 24.

Kwa mujibu wa toptal, kufikia mwaka 2015 kulikuwa na majukwaa zaidi ya 1,500 duniani yanayokutanisha wapenzi mtandaoni ambayo ni mbali na Twitter, Facebook na Instagram.

Baadhi ya majukwaa hayo maarufu ni Tinder, Plenty of Fish na eHarmony.

“Tinder ina watumiaji takriban milioni 57 kutoka nchi 190 duniani. Watumiaji milioni 5.9 wanalipia Sh23,164 kila mmoja kwa mwezi kutumia mtandao huo,” inasomeka sehemu ya chapisho la tovuti ya businessofapps.com.

Huenda miaka ijayo, mtandao utakuwa  ni nyenzo muhimu ya watu kupata wenza wao. 


Soma zaidi:


Ni sahihi kutafuta mwenza mtandaoni?

Licha ya jambo hilo kupata umaarufu duniani, bado kumekuwa na mitazamo tofauti ya watu. Wapo wanaolichukuliwa jambo hilo kuwa ni jema lakini wengine wanaona siyo njia sahihi ya kumpata mwandani wa maisha yako. 

Kwa ambao wanaikataa dhana hiyo, wanabainisha kuwa mtu anaweza kukutana na mke au mume wake popote pale lakini siyo mtandaoni ambako inaweza kuwa changamoto kufahamu undani wa mtu. 

Mfanyabiashara wa viatu jijini Dar es Salaam, Zipporah Zealot ambaye anasema inampa wakati mgumu kuhusu mahusiano yanayoanzia mtandaoni hadi watu kufunga ndoa. 

“Kwangu ni hatari kwa sababu unakuwa haujamfahamu mtu. Picha zinadanganya. Simshauri sana mtu wakutane tu kwenye mtandao. Wachukue muda kujuana na kufahamiana nje ya mtandao,” anasema Zipporah.

Changamoto nyingine inayojitokeza kwa mahusiano hayo ni baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuficha uhalisia wao, jambo linaloweza kutatiza mahuasiano siku za mbeleni endapo mtaoana. 

Mkazi wa jijini Dar es Salaam Paschal Mhina amesema changamoto kubwa zaidi ipo kwa wanaume kwani picha wanazoweka wanawake kwenye mitandao ya kijamii wakati mwingine huwa ni tofauti na uhalisia wao.

“Saa zingine unakuwa ni kweli umempenda mtu na uko tayari kuanzisha naye mahusiano. Wengine unaona haposti vitu vya ajabu anajiposti mwenyewe amevaa vizuri lakini sasa ukisema ukutane naye ana kwa ana, ni magharibi na mashariki. Tofauti!,”  anasema Mhina.

Hata hivyo, waliobahatika kupata wenza kwenye mitandao ya kijamii, wanaeleza kuwa mitandao hiyo inatumika kama jukwaa la kukutanisha na mtu na baada ya hapo inatakiwa zifanyike jitihada kumfahamu muhusika nje ya mtandao.

“Ulimwengu umebadilika, muda mwingi tunashinda mtandaoni kuliko mtaani. Basi ni rahisi kumpata unayempenda huko maana watu wanaingilia sana,” anasema John Juma, mkazi wa Mbeya ambaye anatumia zaidi Instagram.

Viongozi wa dini na wazazi wana lao

Mkazi wa jijini Mwanza Lucia Dotto amesema hawezi kumwacha mtoto wake aingie katika mahusiano yaliyoanzia mtandaoni kwani hana imani na mitandao.

“Kuwa kwenye mahusiano ni muhimu umfahamu mtu katika uzuri wake na hata ubaya wake. Kipindi cha ujana wetu, mahusiano yalikuwa yakijengwa baina ya watu wanaojuana unakuta kila siku mnapishana wakati unaenda kuchota maji, au kukata kuni. 

“Sasa huyo wa mtandaoni utamjuaje hata sura yake ya kuamka?” anahoji Dotto ambaye anaona mitandao siyo sehemu sahihi ya kupata mwenza wa maisha. 

Kupitia kumfahamu mtu katika uhalisia wake, anasema mama huyo kuwa ndiyo ilikuwa chachu ya kudumu kwa ndoa nyingi za zamani kwani mtu alimpenda mtu bila ya kuwa na matarajio.

“Kumpata mtu mtandaoni, siyo kitu kibaya lakini hizi kamera zinadanganya. Unaweza ukawa unatarajia ukutane na binti au kijana mweupe unashangaa unakutana na mtu mweusi kama mimi hapa,” ameeleza Dotto.

Nao viongozi wa dini ambao wamekuwa wakifungisha ndoa katika madhehebu yao, wanaona mitandao ni kama nyenzo tu ya kuwatanisha watu, lakini mahusiano mazuri hujengwa katika upendo, nidhamu na maadili mema bila kujali wapendanao wamekutana wapi. 

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Hamis Mataka ameiambia Nukta Habari kuwa “mitandao ni kama silaha na ina hali mbili nazo ni kutumika vizuri na kutumika vibaya.”

Kwa mujibu wa Sheikh Mataka, katika mahusiano na kujuana mitandao inapotumika huku maadili mema yakizingatiwa basi ni jambo jema kwani wakati huo itakuwa ni jukwaa la kuwafanya watu wajuane na ni jambo la msingi kwa mwanadamu.

“Mitandao inapokuwa kilinge cha kuchochea na kurahisisha mahusiano yanayowaangamiza wahusika na kuwatumbukiza katika mambo haramu kama uzinzi na kadhalika basi tatizo si mtandao bali ukosefu wa maadili mema miongoni mwa watumiaji wa mitandao,” amesema Sheikh Mataka.

Naye, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutoka jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, haijalishi umempata wapi mpenzi wako, jambo la muhimu ni kukubaliana katika masuala ya imani, dini ili kuepuka migongano hapo baadaye. 

“Sidhani kama kupata mpenzi mtandaoni ni tatizo. Tatizo ni dhumuni la wewe kumtafuta mpenzi huyo. Siyo jambo baya ikiwa unazingatia kilicho sahihi mbele ya Mungu, Unaweza kumuomba Mungu na akakuongoza kumpata mwenzi wako wa maisha hata ikiwa kwa njia ya mtandao,” amesema Mchungaji huyo.

Viongozi hao wa dini wameshauri kuwa mitandao ya kijamii iwe kichocheo cha kuendeleza maadili mema yanayofundishwa kwenye dini na siyo kuwatoa katika misingi na miongozo ya mahusiano na ndoa ambayo wamefundishwa. 

Inashauriwa kuwa makini kwani wapo watu wanaotumia mtandao kwa ajili ya kuibia na kudhulumu wengine. Picha| Royal Dating Club.

Ufanye nini unapoanzisha mahusiano mtandaoni?

Hata hivyo, wataalam wa mahusiano wanaeleza kuwa jambo muhimu katika mahusiano yaliyoanzia mtandaoni au sehemu yoyote ni mtu kuwa mwangalifu kabla ya kuchukua maamuzi ya kukubali kuingia kwenye ndoa.

Josephine Tesha ambaye ni mwanasaikolojia anasema kwa sasa mitandao ya kijamii imekuwa ni majukwaa muhimu ya watu kupata wenzi wao na hakuna shida yeyote katika hilo.

“Wapo watu wanaotumia mitandao ya kijamii kudanganya, kuiba na kudhulumu wengine. Hauwezi kuwapangia watu na malengo yao katika mitandao ya kijamii lakini unaweza kubadili namna ya kukabiliana nao kwa kuwa makini,” anasema Tesha.

Anashauri kuwa unapokutana na mtu mtandaoni, ni vyema kuchukua muda kufahamiana, kutana katika maeneo ya wazi na kutokuharakisha kuingia kwenye mapenzi ya karibu au ndoa. 

Muhimu kuliko yote kwa mujibu wa mtaalam huyo ni kutumia mitandao ya kijamii kwa umakini huku watu wakibaki na uhalisia wao na kutokuamini mtu yeyote hadi pale utakapokuwa umejiridhisha kwani wapo ambao wanatumia nafasi hiyo kufanya utapeli.

Enable Notifications OK No thanks