Lissu kugombea uenyekiti wa Chadema Taifa
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amesema atawania uenyekiti wa chama hicho dhidi ya Mwenyekiti wake wa sasa Freeman Mbowe aliyekaa kwenye nafasi hiyo kwa miongo miwili.
Lissu ametangaza uamuzi huo leo Desemba 12, 2024 katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika ukumbi wa Mlimani jijini Dar es Salaam ambapo amesema ameshawasilisha rasmi kusudio la kuwania nafasi hiyo kwa Katibu Mkuu wa Chadema.
“Napenda kuwajulisheni rasmi kwamba nimeshawasilisha taarifa rasmi kwa katibu mkuu wa chama chetu ya kuondoa kusudio langu la kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti kwa upande wa Tanganyika nililowasilisha tarehe 6 Agosti 2024 na badala yake sasa nimewasilisha kwa katibu mkuu kusudio rasmi la kugombea nafasi ya mwenyekiti wa chama taifa katika uchaguzi ujao,” amesema Lissu.