Majaliwa: Wasaidieni wabunifu wachanga Tanzania

May 11, 2021 12:39 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ataka wabunifu wanaochipukia wawezeshwe kuziendesha kazi zao za ubunifu na uvumbuzi kibiashara.
  • Sekta binafsi yatakiwa kutumia teknolojia zinazozalishwa nchini. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi na mamlaka ambazo zinashiriki kuendeleza wabunifu nchini Tanzania zihakikishe zinawawezesha wabunifu wanaochipukia kuziendesha kazi zao za ubunifu na uvumbuzi kibiashara ili zichangia kupata ajira na maendeleo ya Taifa. 

 “Taasisi za sayansi na teknolojia; vyuo vikuu; taasisi za utafiti na maendeleo; na mamlaka mbalimbali kama SIDO (Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo), VETA (Mamlaka ya Ufundi Stadi Tanzania) na DON BOSCO ambazo kwa namna moja ama nyingine zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga ziwasaidie kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao,” amesema.

 Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Mei 11, 2021 wakati akifunga maonyesho ya Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

 Amesema kuwa uendelezwaji wa wabunifu na wavumbuzi ufanyike kwa kasi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha matunda ya jitihada zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwaibua na kuwatambua wabunifu wachanga zinazaa matunda.

 “Nitoe wito kwa taasisi zote kutumia ubunifu na uvumbuzi unaozalishwa nchini kama nyenzo muhimu wakati wa kuandaa na kutekeleza mipango mbalimbali inayoandaliwa katika sekta zote, iwe za huduma au uzalishaji ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo ya Taifa letu,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana:


Pia amezitaka taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti na maendeleo zishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, hasa ya viwanda ziweke utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Nia ya Serikali ni kuona ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia zinazozalishwa na wabunifu wachanga unatoa mchango mkubwa katika kuzalisha ajira mpya, kuongeza kipato kwa wabunifu na kuchangia katika pato la Taifa.” amesisitiza.

Akizungumzia mitaala ya elimu, Waziri Mkuu amesema ni vema iandaliwe kwa namna ambayo itawawezesha wahitimu kuwa wabunifu na mwisho wa siku waweze kutumia ubunifu huo kujitengenezea ajira zao wenyewe na ikiwezekana, wawaajiri wengine.

 “COSTECH tumieni nafasi yenu kuwaelimisha wabunifu umuhimu wa kuhakikisha kuwa ubunifu na uvumbuzi wao unatambuliwa na kupewa hatimiliki na hatimaye kubiasharishwa. Elimu kuhusu hakimiliki ni muhimu kwani itawawezesha wabunifu kulinda ubunifu wao. 

“Wekeni mikakati ya kuwaelimisha wabunifu wachanga husasan walioko katika sekta isiyo rasmi kuhusu umuhimu wa kuwa na hakimiliki,” amesisitiza.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV