Majaliwa: Hakuna mkulima wa mkonge atakayedhulumiwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi, baada ya kuzindua rasmi Jengo la Mamlaka ya Mkonge mkoani Tanga akiwa katika ziara ya siku moja ya mkoa huo, kukagua maendeleo ya zao la mkonge, Juni, 1, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Amesema atahakikisha mali zote za wakulima wa zao la mkonge nchini Tanzania zinarudishwa mikononi mwao.
- Watanzania watakia kulima kwa wingi mkonge maana Serikali iko nyuma yao.
- Ataka wananchi wapewe pembejeo na ardhi walime zao hilo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema itahakikisha mali zote za wakulima wa zao la mkonge nchini Tanzania zinarudishwa mikononi mwao na hakuna mtu yeyote atakayeonewa huku akiagiza wananchi kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo.
Mkonge ni miongoni mwa mazao ya mkakati ambayo Serikali ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa pembejeo na masoko ya ndani na kimataifa.
Majaliwa, aliyekuwa akizungumza Jumatatu (Juni 1, 2020) wakati akifungua jengo la Bodi ya Mkonge Tanzania lililopo jijini Tanga, amesema Serikali imedhamiria kurudisha heshima ya wakulima wa mkonge ili wafaidike kiuchumi.
“Tutarudisha mali zote za wakulima na ninawahakikishia hakuna mtu yoyote atakayeonewa, kama tulivyorudisha hizi mali za Bodi ya Mkonge Tanzania tutafanya hivyo hivyo kote bila kumuonea yeyote na kuanzia leo bodi hii ya mkonge imethibitishwa kuwa bodi kamili.
“Mkonge ni fedha, halmashauri wekeni vitalu mzalishe mbegu muwape wananchi bure. Kama unashamba kubwa hujaliendeleza, kulingana na muda uliowekwa, tutalichukua,” amesema.
Amesema wananchi hususani wa mkoa wa Tanga wajipange katika kuyafufua mashamba yao na kuanzisha mapya na Serikali itawasaidia kuhakikisha mbegu bora na pembejeo zinapatikana.
Zinazohusiana:
- Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima wapewa changamoto kuongeza uzalishaji zao la mkonge
- Rasmi: Tabora ndiyo ‘makao makuu’ ya kuku wa kienyeji Tanzania
Aidha, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi katika kila mkoa wenye ardhi nzuri ambayo inastawi zao hilo waanzishe kilimo cha mkonge walime na Serikali itawasaidia bila kujali ni mtu mmoja mmoja, wakulima wa kati na wakubwa.
“Wakuu wa wilaya waondoeni maafisa kilimo waliopo ofisini waende vijijini wakawasaidie wakulima namna nzuri ya kulima zao hili kwa faida, mkonge ni pesa, Serikali yenu itasimamia. Tunataka mkonge urudi kwenye nafasi yake. Endeleeni kuwahamasisha walime mkonge, tunataka kila tunapopita tuone mashamba ya mkonge,” amesisitiza Majaliwa.
Ameiagiza bodi hiyo kufanya utambuzi wa mashamba na wayarudishe kwa watu walime sambamba na mapori yote makubwa yaliyoko kwenye halmashauri ambayo hayatumiki nayo yatambuliwe na waishauri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kumshauri Rais John Magufuli kwa ajili ya kugawa kwa wananchi waweze kulima.
“Nendeni Benki ya Kilimo (TADB) mkachukue mikopo,” amesema Majaliwa kwa wakulima wasio na mitaji.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu zao hilo lilikuwa linalimwa na mikoa zaidi ya 12 na kuzalisha nusu ya mahitaji ya dunia lakini sasa limeachwa kwenye mikoa minne tu.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, kinaeleza kuwa uzalishaji wa zao uliongezeka kwa asilimia 11.2 hadi tani 40,635 mwaka 2018 kutoka tani 36,533 zilizorekodiwa mwaka 2017.
Latest