Majaliwa azungumzia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania
- Asema kutakuwa na matukio mengi ya mvua kuliko yanayotokea sasa.
- Awashauri Watanzania kuchukua tahadhari ikiwemo kuhama katika maeneo ya mabondeni.
- Awataka kuendelea kufuatilia kwa ukaribu tahadhari zinazotolewa na TMA.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasisitiza Watanzania kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kupunguza athari zinazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Majaliwa ameyasema hayo leo (FebruarI 6, 2020) katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Zainab Vulu aliyehoji mkakati wa Serikali kuwasaidia watu walioathirika mvua zinazoendelea kunyesha na uboreshaji wa miundombinu iliyoharibika.
“Mwaka huu mvua ni nyingi sana na taasisi yetu ya hali ya hewa (TMA) imeendelea kutuhabarisha kwamba mvua ndiyo zinaanza. Sasa kama ndiyo zinaanza kwa hali hii, tutarajie tutakuwa na matukio mengi makubwa zaidi ya haya ambayo tumeyapata,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wanaokaa maeneo ya mabondeni kuondoka kwenye maeneo hayo na kupisha shughuli za kulisha mifugo na kilimo kufanyika huko.
Amesema, “tunapopata taarifa za wingi wa mvua mwaka huu, sisi wenyewe tunatakiwa tuchukue tahadhari kwani wanasema mvua bado inakuja,”
Zinazohusiana
- TMA yatoa ushauri, tahadhari ujio mvua za vuli Oktoba
- Kicheko kwa wakulima, TMA akitoa mweleko mvua za msimu
Licha ya kamati za maafa kuendelea kufanya kazi vizuri, amesema jambo la muhimu ni kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa wananchi na kuzingatia taarifa zinazotolewa na wataalam.
Jana Februari 5, 2020, TMA imetoa utabiri ambao unatahadharisha mvua kubwa kunyesha leo kwenye baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya, Rukwa na Iringa ambapo baadhi ya makazi yatazungukwa na maji.
Hata hivyo, wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka TMA na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na marejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.