Majaliwa awatoa hofu wakulima, wanunuzi wa pamba

July 16, 2019 9:19 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema hadi kufikia Julai 30 mwaka huu, pamba yote iliyoko katika mikoa mbalimbali nchini itakuwa imeshanunuliwa.
  • Wanunuzi wapewa dhamana na BoT ya mikopo ya ununuzi wa pamba.
  • Rais Magufuli asisitiza bei elekezi ya Sh1,200. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Julai 30 mwaka huu, pamba yote iliyoko katika mikoa mbalimbali nchini itakuwa imeshanunuliwa na wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao.

Hivi karibuni kumetokea hali ya sintofahamu kuhusiana na ununuzi wa zao hilo baada ya kutangazwa kwa bei elekezi ya Sh1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.

Bei elekezi ya pamba kwa msimu huu ilitangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga na ilitakiwa ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019. 

Hata hivyo, ununuzi wa zao hilo umekuwa wa kusuasua kutokana na kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia, jambo lililowafanya wanunuzi wasitishe ununuzi wa zao hilo la biashara kutoka kwa wakulima kwa hofu ya kupata hasara.

Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Julai 15, 2019) akiwa ziarani katika wilaya ya Igunga kwa lengo la kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba, amesema baada ya kufanya mashauriano, pamba yote itakuwa imenunuliwa ifikapo Julai 30. 

Amesema Serikali imeamua kuingilia kati suala la ununuzi wa zao hilo kutokana na kusuasua kwa soko lake ambapo imetoa dhamana ili kuwawezesha wanunuzi kukopeshwa fedha na benki mbalimbali kwa ajili ya kununua pamba kutoka kwa wakulima.

“Hofu ya wanunuzi ilikuwa ni hasara na kushindwa kurejesha mikopo benki na taasisi nyingine za fedha; tatizo hilo sasa limeisha baada ya Serikali kupitia BoT kukubali kutoa dhamana ya mikopo hiyo,” amesema Majaliwa. 

Waziri Mkuu, Kasism Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Katibu na Meneja wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga kuhusu pamba iliyokusanywa na wakulima kwenye ghala la ushirika huo, Julai 15, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa changamoto walizokutana nazo wakulima wa pamba ni mapito tu na Serikali itahakikisha inashughulikia suala hilo ili kuwapatia tija na haki yao. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu,  amewasihi wakulima wa zao hilo na wakulima wa mazao mengine nchini wahakikishe mara baada ya kuuza mazao yao wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo watakazozitumia katika msimu ujao.

Kushuka kwa bei ya pamba duniani, kunatajwa kusababishwa na mgogoro baina ya China na Marekani ambapo nchi hizo zimekuwa zikiwekeana vikwazo vya ushuru wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mzao ya kilimo.

China ndiyo mnunuzi mkubwa wa pamba na mmiliki wa viwanda vya nguo lakini Marekani imekuwa ikigomea kununua nguo za China. 

Licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya bei katika soko la dunia, Rais John Magufuli akiwa Mwanza jana, amesisitiza kuwa pamba itanunuliwa kwa bei elekezi ya Sh1,200 na siyo vinginevyo. 


Soma zaidi:


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema Serikali itahakikisha inaendelea kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa masoko kwa mazao yao na hivyo kujiongezea tija.

Waziri huyo amesema mbali na kutafuta masoko, Serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali vya nguo hapa nchini ili kuwawezesha wakulima wa zao la pamba kuwa na soko la uhakika. 

“Kuhusu suala la maghala tunatambua tatizo hilo na tutahakikisha tunayaboresha ili pamba iweze kuhifadhiwa katika mazingira bora,” amesema Hasunga katika ziara ya Waziri Mkuu. 

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV