Majaliwa awanyooshea kidole wataalam wa manunuzi, ugavi Tanzania
- Awaonya kutojihusisha na rushwa maana Serikali itawachukulia hatua kali.
- Watakiwa kufanya kazi kwa maslahi ya umma na wananchi wanyonge.
- Dk Mpango amesema uzalendo wa wataalam hao ni wa mashaka.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya wataalamu wa ununuzi na ugavi ambao bado wanaendekeza vitendo vya rushwa, upendeleo, kuingilia michakato ya ununuzi, waache mara moja kwani Serikali haitomhurumia yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Majaliwa ametoa onyo hilo leo Desemba 2, 2020 alipofungua kongamano la 11 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) linalofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
“Mjitahidi kuwa mstari wa mbele kuepuka vitendo viovu vinavyohusishwa na fani hii ya ununuzi na ugavi. Mtambue sheria kali zipo na kwamba Serikali haitakuwa na huruma kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa,” amesema Majaliwa.
Amesema manunuzi katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali ni zaidi ya asilimia 70, hivyo shughuli hiyo isipofanyika kwa kuzingatia weledi ni dhahiri kuwa wananchi hawataweza kupata huduma iliyokusudiwa na miradi haitatekelezwa kwa viwango kusudiwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi na bodi ya PSPTB ili kupunguza au kuondoa kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi kwani pesa nyingi za Serikali, zinatumika kupitia taaluma hiyo.
Pia, amezitaka taasisi zote za umma kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao kwa kupitia mfumo wa kisasa wa manunuzi (TANePS) ambao unasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji, uwazi, kupunguza gharama na mianya ya rushwa.
Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa manunuzi na ugavi wahakikishe wanatoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi kwa kuzingatia sheria na taratibu za manunuzi ya umma ili kupata matokeo yenye uthamani wa fedha iliyotumika.
“Simamieni vizuri uandaaji wa mikataba ya manunuzi ili kuepuka nyongeza ya kazi (Variations) na hivyo kuziepusha taasisi katika gharama zilizo nje ya bajeti kwa kuzingatia uwepo wa uwazi katika utayarishaji na utekelezaji wa zabuni ikiwemo kujiepusha na migongano ya kimaslahi,” amesema Majaliwa.
Zinazohusiana:
- Nsekela ateuliwa kurithi mikoba ya Dk Kimei
- BOT yashusha riba tena kwa benki za biashara Tanzania
- Sekta ya manunuzi kuboresha mfumo wa utoaji taarifa kwa umma
Kongamano la mwaka huu litajikita kujadili namna ya kufikia umahiri katika kusimamia mnyororo wote wa ununuzi na ugavi ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia, mbinu mpya za kuhakikisha manunuzi yanaendana na thamani ya fedha zilizotumika pamoja na mafanikio na changamoto za kutumia mfumo wa ‘force account’.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema maafisa ununuzi na ugavi hawazingatii maadili ya taaluma zao na kwamba uzalendo wao ni wa mashaka, wanatumia utaratibu wa ‘force account’ kama kichaka cha kuiba.
“Matumaini yangu ni kuwa kongamano hili litawatendea haki Watanzania hasa wanyonge, ambao fedha zao zinaibiwa kutokana na udhaifu mkubwa katika manunuzi na ugavi kwenye Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji.
“Mada ziwasilishwe kwa lugha ya kiswahili ili tuelewane vizuri katika jitihada za kufyeka kichaka cha wizi, ubadhilifu, rushwa na ufisadi kupitia ununuzi na ugavi,” amesisitiza Dk Mpango.
Latest



